Je, ni nani kuwa Makamu wa Rais Tanzania?

    • Author, Markus Mpangala
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania

Baada ya kumaliza shughuli za mazishi ya aliyekuwa rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli Machi 26 mwaka huu, macho na masikio ya wananchi sasa yanaelekezwa katika uteuzi wa nafasi ya Makamu wa Rais ambayo ipo wazi tangu Machi 19 baada ya Samia Suluhu Hassan kuapishwa kushika wadhifa wa Urais wa Jamhuri ya Muungano.

Kisiasa na kikatiba mchakato wa kumpata Makamu wa Rais unazihusisha taasisi mbili, chama tawala CCM na Bunge la Tanzania.

Rais Samia na chama chake cha CCM wana kibarua cha kuteua jina la mwanasiasa mmoja anayefaa kisha kuliachia Bunge kupitisha jina hilo ili awe Makamu wa Rais kusaidiana kazi na Rais wa sita katika kipindi cha miaka minne ijayo (2021-2025).

Taarifa zinabainisha kuwa Kamati Kuu ya chama tawala CCM inatarajiwa kukutana siku chache zijazo kuzungumzia ajenda za makabidhiano ya uongozi katika nafasi za Uenyekiti wa chama ambayo itachukuliwa na Rais Samia na kupata Makamu wa Rais.

Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania jina la Makamu wa Rais linatarajiwa kupendekezwa na rais Samia Suluhu Hassan baada ya mashauriano na chama chake kisha jina hilo hupelekwa bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura ili kukidhi vigezo vya kikatiba.

Maswali yanayotawala katika anga za siasa baada ya mazishi ni;

  • Je ni mwanasiasa yupi ataibuka kuwa Makamu wa Rais?
  • Je Makamu huyo anaweza kutoka katika kundi gani kati ya vijana, viongozi wastaafu na wazee, jinsia, ukanda, muungano au dini?

Hayo na mengine ni sehemu ya mchakato wa kukabidhiana madaraka kwa njia ya amani jambo ambalo linachora taswira ya kipekee kwa Taifa hilo.

'Makamu Mwanadiplomasia'

Baadhi ya viongozi wa chama na serikali wamemwambia mwandishi wa makala haya kuwa vigezo vya Makamu wa Rais ni yule mwenye uwezo kiutendaji, uelewa wa diplomasia, uelewa wa mipango na mikakati ya marehemu John Magufuli.

Kwamba kigezo hicho kinamtaka Makamu ambaye atakuwa na majukumu ya kushughulikia diplomasia na ushirikiano wa Tanzania na Jumuiya za Kimataifa. Hili ni eneo mojawapo kati ya mengi yanayoangaliwa kupatikana kwa kiongozi huyo.

"Maneno ni mengi, mchakato unafanywa kwa usiri kidogo, ingawaje upo uwezekano wa kufikishwa mezani majina matatu. Hayo ndiyo yanayosumbua kwa sasa hivi lakini siasa zina njia nyingi, yapo makundi yanajadili majina mengine, ila litakuwa jina la kushangaza. Vigezo ni lazima awe imara na mwelewa katika masuala ya diplomasia, kuelewa mipango na mikakati ya JPM na lazima awe mtii kwa Rais wetu. Juu ya mivutano na makundi ndani ya chama cha siasa ni sehemu ya michakato ya kisiasa, litapita salama hili kama walivyosema viongozi wakuu wa nchi wa Majeshi na serikali kule Chato (Geita), tutajua hivi karibuni," kiongozi mmoja mwandamizi wa serikali amemwambia mwandishi makala haya.

Wanasiasa vijana

Wanasiasa wa kundi hili wanatajwa kuwa na sifa za kuteuliwa kuwa Makamu wa rais. Hata hivyo wanadaiwa kuwa na ndoto au safari ndefu ya kisiasa hivyo kukosa fursa ya kutupiwa jicho la nani anafaa kuteuliwa kushika wadhifa huo mkubwa wa pili baada ya Urais.

Kundi hili linatajwa kuweza kuleta mgongano ifikapo mwaka 2025 ikiwa Rais Samia ataamua kugombea urais kipindi kingine kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 40(4).

Miongoni mwa wanasiasa wanaotajwa katika kundi hili ni January Makamba, Nape Nnauye, Mwigulu Nchemba na Emmanuel Nchimbi kwa kuwataja wachache. Nchemba na Makamba wote walikuwa kati ya watia nia 42 wa urais mwaka 2015 hivyo kwa umri wao bila shaka yoyote wanaweza kutia nia hiyo tena mwaka 2025.

Upande wa pili, kundi hili limetajwa katika duru za kisiasa kuwa kiunganishi cha vijana ambao wanaunda idadi kubwa ya wananchi wa Tanzania. Kwamba kuwaletea Makamu wa rais kijana kutakuwa na chachu ya kuunganisha kundi la wazee na vijana ambao ni viongozi wa wajao, wana nguvu, ari, kasi na maarifa ya kisasa.

Viongozi wastaafu wa chama na serikali

Kundi la viongozi wastaafu wa chama na serikali ambao ni wanachama wa CCM linatajwa kuwa kigezo cha kuteuliwa.

Hawa ni wanasiasa ambao hawana matamanio ya kuwania nafasi ya Urais ifikapo mwaka 2025 hivyo kuepusha mgongano wa Ibara 40(4) ikiwa Rais Samia atawania kipindi kingine.

Kisiasa kundi hili linatazamwa kama nyenzo ya kuunganisha taifa kutokana na kukubalika kwao na pande zote.

Miongoni mwao ni Jaji Joseph Warioba, Mizengo Pinda, Abdulrahman Kinana, Wilson Masilingi, Profesa Mark Mwandosya, Balozi Khamis Kagasheki na wengine wa kaliba yao.

Utamaduni wa Muungano

Kwa 'utamaduni' wa kawaida anakotoka Rais hakupaswi kutoa Makamu wa rais. Badala yake makamu rais anatakiwa kutoka upande mwingine.

Ndiyo kusema kigezo hiki kwa vile Rais Samia Suluhu Hassan anatoka Zanzibar kwahiyo makamu wake atatoka Tanzania Bara. Kigezo hiki kinawaweka wima wanasiasa wa upande wa Tanzania Bara hivyo kuifanya nafasi ya umakamu wa urais kuwa inayowindwa zaidi kwa sasa.

Makamu wa Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli wote walitoka Zanzibar.

Hoja ya ukanda

Duru za kisiasa zinabainisha kuwa kumekuwa na tetesi nyingi kuhusu wanasiasa kadhaa wanaotajwa katika nafasi ya umakamu wa Rais wakihushishwa na ukanda wanakotoka.

Hilo huitwa mgawanyo wa madaraka.

Miongoni mwa majina hayo ni Kassim Majaliwa na Emmanuel Nchimbi, lakini kwa kuzingatia nafasi za ukanda yenye kuunganisha taifa jambo hili haliwezekani, ni mpaka pale Rais atakapoamua kutoendelea na Waziri Mkuu wa sasa ndipo Nchimbi anaweza kuingia kwenye chekecho kwa vile wote wanatokea Mikoa ya kanda ya kusini.

Aidha, rais aliyepita ametoka kanda ya ziwa, inaelezwa kuwa upo uwezekano pia kanda hiyo kuibua Makamu wa Rais kwa kigezo cha kuponya vidonda vinavyowakabili wananchi wake tangu kifo cha Rais Magufuli.

Hata hivyo hoja hiyo inaweza kutupiliwa mbali kwa kigezo kuwa nafasi ya Umakamu wa Rais ni ya watanzania wote kwa usawa. Kwa vile Rais bado hajaunda serikali yake hivyo basi inabaki kuwa lolote linawezekana kutokea.

Kigezo cha dini

Kimsingi kumekuwa na utamaduni wa kuunganisha taifa, hivyo suala la kuzingatia uwiano wa dini ni jambo linalofahamika.

Iwapo rais ni Muislamu hivyo kwa vyovyote makamu wake atakuwa mkristo kwa sababu ndizo imani zenye kuwatoa wanasiasa wengi nchini humo.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema hoja hiyo inaweza kuachwa kwa kuangalia mfano wa rais mstaafu Jakaya Kikwete ambaye Makamu wake Dkt.Gharib Bilal wote walikuwa waumini wa dini moja.

Aidha, mfano wa pili wa rais mstaafu Jakaya Kikwete ambaye alianza na makamu Dkt. Mohammed Shein, hivyo inawezekana Rais Samia Suluhu Hassan kupendekeza jina la Kassim Majaliwa au mwanasiasa mwingine yeyote wa dini hiyo akiwa na vigezo vyote muhimu vya utendaji kazi, utii na uzalendo kwa Tanzania.

Kundi la jinsia

Zipo taarifa kutoka ndani ya Kamati Kuu ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kwamba iliazimia kwa kauli moja kuwa ni muhimu kuwa na uwiano wa jinsia katika nafasi za Rais na Makamu wake. Ilikubaliwa kuwa ikiwa Rais ni mwanaume basi Makamu wake atakuwa mwanamke.

Vilevile ikiwa Rais ni mwanamke basi makamu wake atakuwa mwanaume. Hoja hiyo ndiyo iliyotumika kumpitisha Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza wa CCM, na ndiyo dira ya chama hicho katika siasa za ushindani nchini Tanzania.

Kwa msingi huo rais wa sasa ni mwanamke kwa kushirikiana na chama chake wanalo jukumu la kupendekeza mwanaume atakayekuwa Makamu wa Rais.

Uteuzi wa kushangaza

Ipo dhana moja muhimu katika siasa kuhusu nafasi nyeti za uteuzi.

Licha ya majina kadhaa kutajwa kuwa ndiyo yanapigiwa upatu lakini anaweza kuibuka mwanasiasa ambaye hakubashiriwa awali.

Katika kundi hili chaguo la Makamu wa Rais linaweza kutoka kwa mwanasiasa atakayeshangaza.

Hoja hii inabakuliwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali pamoja na wataalamu wa sayansi ya siasa, kwamba kuibuka jina la mwanasiasa wa kushangaza ni sehemu ya kawaida ya michakato ya kisiasa ikitolewa mfano uteuzi wa wagombea wa urais ndani ya chama cha CCM.

Huyu ni mwanaisiasa wa akiba.

Na sasa swali ni moja tu; Je ni nani atakuwa Makamu wa Rais nchini Tanzania