Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kifo cha Rais John Poimbe Magufuli: Je Rais Samia atafanya nini na Jumuiya ya Afrika Mashariki?
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi Tanzania
RAIS Samia Suluhu Hassan wa Tanzania anaanza urais wake katika wakati ambapo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inapita katika changamoto lukuki - na nchi yake ikitajwa kama mojawapo ya zile ambazo "ari" yake katika jumuiya inatia shaka.
Changamoto kubwa ambayo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) huwa inapitia kila wakati ni kwamba mara nyingi uimara na udhaifu wake hutegemea aina ya viongozi waliokuwepo madarakani katika wakati husika.
Ndiyo sababu, ni muhimu kumtazama Samia binafsi na Tanzania yake kwa sababu anachukua nafasi ya mtangulizi wake, hayati John Magufuli, ambaye staili yake ya uongozi na mtazamo wake kuhusu jumuiya hiyo umeacha athari - hasi na chanya, katika taasisi hiyo.
Bahati ya EAC wakati inaanzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1967 ilikuwa kwamba waliokuwa viongozi wa nchi wanachama waanzilishi wakati huo - Julius Nyerere (Tanzania), Jomo Kenyatta (Kenya) na Milton Obote (Uganda); wote walikuwa ni watu walioamini kwa dhati katika dhana ya Umajumui wa Afrika.
Wakati inavunjika mwaka 1977 - Obote hakuwepo madarakani, Kenyatta alikuwa ameanza kuzeeka na kupoteza ushawishi wake na Nyerere hakuwa anapatana kabisa na Idi Amin Dada, aliyechukua nafasi ya Obote.
Wakati EAC inafufuliwa mwaka 1997, waliokuwa marais wa nchi wanachama; Yoweri Museveni (Uganda), Daniel Arap Moi (Kenya) na Benjamin Mkapa (Tanzania), walikuwa pia ni watu walioamini katika umoja na jamii ya utandawazi - lakini pia walioshuhudia kwa macho yao uzuri wa kuwa na EAC na hasara iliyopatikana baada ya kuvunjika kwake.
Samia, aliyekuwa Makamu wa Rais wakati wa utawala wa Magufuli - kwa sababu ya historia ya nyuma ya viongozi wa nchi wanachama, naye ataacha alama zake kwa namna anavyoitazama na kushughulika na jumuiya hiyo yenye nchi wanachama watano; Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Kenya na Sudan Kusini.
Nini utakuwa mchango wa Samia kwenye EAC?
Jambo la kwanza kulifahamu kumhusu Samia ni kwamba kwa tabia ni mtu anayeamini katika umoja na mtangamano wa Afrika Mashariki. Mzaliwa wa Zanzibar, Rais huyu wa sita wa Tanzania, amekulia katika eneo ambalo limezoea kupokea wageni na kimsingi wageni ni sehemu ya historia ya kwao.
Mtoto wake pekee wa kike, Wanu Hafidh Ameir - ambaye sasa ni Mbunge wa Bunge la Tanzania, alipata kusomea nchini Uganda na hili linakupa picha ya uhusiano wa familia hiyo na nchi jirani za Afrika Mashariki.
Mmoja wa watu waliowahi kufanya kazi naye kwa muda mrefu ameniambia kwamba Rais Samia anaamini kwa dhati katika EAC na kwamba ni wazi jumuiya itaanza kuona ari mpya kutoka Tanzania katika siku chache zijazo.
" Samia ni mtu anayeamini katika umoja. Unajua Wazanzibari, kwa tabia tu, ni watu waliozoea kuishi na kufanya kazi na watu wa mataifa tofauti. Lakini katika EAC, Samia ataleta ari mpya kwa sababu anajua fursa zilizopo katika ushirikiano," alisema ofisa huyo wa serikali.
Baadhi ya changamoto za Tanzania na jirani zake zilizojitokeza wakati wa utawala wa Rais Magufuli ulikuwa ni mtazamo binafsi wa Rais huyo wa tano wa Tanzania kuhusu EAC na pia viongozi wenzake katika jumuiya hiyo.
Kwa mujibu wa maelezo ya mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania - Magufuli hakuwahi kuwaamini kwa asilimia 100 baadhi ya viongozi na nchi wanachama wa EAC.
" Kwa miaka mingi kumekuwa na hali ya kutokuaminiana baina ya Watanzania na baadhi ya jirani zao katika nchi za EAC. Hayati Rais Magufuli ni Mtanzania na alikuwa akiamini katika baadhi ya dhana hizo. Naamini Wakenya na Waganda nao wana dhana kama hizo na wakati mwingine hicho huwa ni kikwazo kikubwa," alisema ofisa huyo.
Bahati ya kwanza ambayo Samia anayo sasa ni kwamba Magufuli alimpa nafasi kubwa ya kushiriki katika baadhi ya mikutano muhimu ya EAC na ndiyo sababu hata wakati wa msiba wa kitaifa wa kiongozi huyo wa zamani wa Tanzania, alisema anajuana vizuri na viongozi wenzake hao ambao aliwaita "kaka zake".
Changamoto za EAC
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, EAC imekumbwa na changamoto kubwa tatu za msingi; uhusiano usioridhisha baina ya nchi wanachama, wanachama kutochangia bajeti ya uendeshaji wa jumuiya na hali ya usalama ya Sudan Kusini.
Kumekuwa na hali ya sintofahamu kati ya nchi za Rwanda na Burundi, Rwanda na Uganda na migogoro ya mara kwa mara kati ya Tanzania na Kenya - mara nyingi ikihusu eneo la biashara.
Hali ya uhusiano ilikuwa mbaya kiasi kwamba tangu kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, kitokee, taifa hilo limekuwa likilegalega kwenye kuhudhuria mikutano ya viongozi wa jumuiya na kwenye michango.
Samia atakuwa mpatanishi?
Samia alianza kujulikana na Watanzania wengi baada ya kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba la Tanzania. Bunge hilo lilikuwa na wajumbe zaidi ya 500 kutoka katika makundi tofauti kama wakulima, wanasiasa, wafugaji, wanaharakati na makundi mengine na kazi yake kubwa ilikuwa kuongoza mikutano hiyo.
Uzoefu huu - na kwa taswira yake kama mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo katika jumuiya hiyo, unampa nafasi ya kuwa mpatanishi na mtatuzi wa migogoro ya chinichini inayoendelea kuigubika jumuiya.
Kitendo cha wakuu wa nchi za EAC kuhudhuria msiba wa Magufuli kwa wingi - akiwamo Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambaye nchi yake pia imeomba kuwa mwanachama wa EAC, kimetoa picha ya mwanzo mzuri.
Kama Samia ataikumbatia EAC kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake kama Nyerere, Mkapa na Jakaya Kikwete - kuna uwezekano mkubwa wa kushuhudia jumuiya inayokwenda vizuri kuliko hii ya sasa.