Urusi na China zajibu vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi

Urusi na China kwa pamoja wameshutumu vikwazo vya nchi za Magharibi, siku moja baada ya Umoja wa Ulaya, Marekani na Canada kupiga marufuku baadhi ya maafisa waandamizi wa China kwa madai ya unyanyasaji wa haki za binadamu dhidi ya kabila la Uighur.

Madai hayo ya pamoja yamewadia wakati ambapo waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ametembelea Guilin kusini mwa China.

Alisema kuwa "maamuzi ya pamoja ya "EU yalikuwa "yameharibu" uhusiano na Urusi.

Mwenzake wa China, Wang Yi, alisema enzi ya kuingilia masuala ya ndani ya China "imepitwa na wakati kabisa".

Ni mara ya kwanza EU imeweka vikwazo vipya dhidi ya China juu ya madai ya unyanyasaji wa haki za kibinadamu tangu mwaka 1989 katika kamata kamata iliyotokea uwanja wa Tiannanmen.

Waliolengwa na vikwazo vya nchi za Magharibi

Hata hivyo, washirika wa nchi za Magharibi wamewawekea vikwazo maafisa wa Urusi walio karibu na Rais Vladimir Putin juu ya masuala kadhaa ikiwemo:

  • Mwaka 2014, Urusi ilitwaa rasi ya Crimea nchini Ukraine
  • Mgogoro wa mashariki mwa Ukraine
  • Urusi ilidaiwa kuingilia uchaguzi wa urais wa Marekani mwaka 2016
  • Aliyekuwa afisa wa ujasusi wa zamani nchini Urusi Sergei Skripal alishambuliwa kwa sumu sawa na mpinzani wa Putin Alexei Navalny.

Hata hivyo Urusi imekanusha madai hayo.

Akitembelea Nato nchini Brussel Jumanne, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani State Antony Blinken pia amesisitiza kupinga vikali mpango wa Urusi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Bahari ya Baltic Urusi hadi Ujerumani.

Ujerumani iko katika hatari ya kuwekewa vikwazo juu ya mpango huo ambao uko karibu kukamilika wakati ambapo serikali ya Marekani inauchukulia mradi huo kama unaotumiwa na Urusi kugawanya Ulaya hata zaidi. Bomba hilo la gesi litapita Ukraine na Poland - ambazo zinapanga kupinga mpango huo vikali.

China imewashikilia karibu Waighur milioni moja - wengi wao wakiwa waumini wa dini ya Kiislamu - katika kambi za kaskazini magharibi mwa eneo la Xinjiang, ambako madai ya watu kuteswa, utumikishwaji na unyanysaji wa kingono yamejitokeza.

China imekanusha madai ya nchi za Magharibi na kusema kuwa kambi hizo ni vituo vya "kuelimisha" vinavyotumika kukabiliana na ugaidi.

Aidha, China imejibu kwa kuwawekea vikwazo maafisa wa Ulaya, siku ya Jumatatu.

Bwana Wang alisema nchi zenye nguvu "hazistahili kuingilia masuala ya ndani ya nchi zingine kwa kuzingatia viwango vyao, au kutumia bango la demokrasia na haki za binadamu kujenga nguvu yao".

Madai ya kujitetea kupitia chanjo

Urusi chini ya Rais Putin imeendeleza uhusiano wa kiuchumi, kijeshi na kisayansi na China. Katika kipindi cha karne moja iliyopita, walikuwa maadui wa Vita Baridi.

Wote Bwana Lavrov na Bwana Wang wamekataa madai kutoka baadhi ya nchi za Magharibi kwamba Urusi na China zilikuwa zinatumia "chanjo" ya kukabiliana na janga la Covid-19 ili kupata uungwaji mkono duniani.

Nchi nyingi zimepokea dozi za chanjo ya Sinopharm ya China na ile ya Sputnik V ya Urusi kwa haraka zaidi na kwa gharama ya chini kuliko chanjo kutoka nchi za Magharibi.

Katika baadhi ya visa nchini China - chimbuko la janga la corona - chanjo imetolewa bure.

Bwana Lavrov alisema kuwa uuzwaji wa chanjo ya Sputnik V nje ya nchi hiyo kunaongozwa na misingi ya "ubinadamu" na "kuokoa maisha", wala sio siasa au maslahi ya kibiashara.

Bwana Wang alisema lengo la China kuanzia mwanzo lilikuwa ni "kuwezesha watu wengi zaidi kupata chanjo haraka iwezekanavyo" na "kusaidia dunia nzima".