Fahamu jinsi WhatsApp inavyopata faida kubwa kwa kutumia maelezo yako

Chanzo cha picha, Getty Images
Umewahi kujiuliza ni vipi wamiliki wa mtandao wa kijamii wa WhatsApp wanavyopata faida ilhali huduma hiyo inatolewa bure kwa watumiaji?
"Facebook na Instagram ndizo madirisha ya duka ilhali WhatsApp ndio rejista ya kuchukua malipo'
Hilo ndio jibu alilotoa afisa mkuu wa oparesheni wa WhatsApp Matt Idema akieleza muundo wa kibiashara wa mtandao huo wa kijamii .
Chini ya Facebook ambayo ndio kampuni kuu inayomiliki whatsapp kampuni hiyo iliacha kutengeza pesa kupitia malipo ya matumizi kutoka kwa wateja wake na sasa malipo yanatolewa kutoka tozo za kufanyia malipo kupitia WhatsApp Business na huduma kwa kampuni nyingine .
Kampuni kadhaa na hasa nchini India zinaweza kutangamana na wateja kupitia mtandao huo na nyingine zinatumia Whatsapp kama kituo cha kibiashara na kufanya mauzo .

Chanzo cha picha, Getty Images
Mpango huo umeonyesha ishara za kuboreka zaidi na watalaam ambao BBC Mundo imezungumza nao wamesema utarejeleza mjadala kuhusu jinsi Facebook inavyotumia maelezo ya wateja wake kujipa faida . Maghala ya data ya WhatsApp yamehifadhi maelezo binafsi ya watu bilioni 2 .
"WhatsApp ni bure kwa watumiaji kwa sababu hakuna itakavyojitangaza kama bidhaa' amesema mchambuzi wa masuala teknolojia Pilar Sáenz akizungumza na BBC Mundo.
Ununuzi wa Mabilioni
Mfumo huo wa kutuma jumbe unaotumika sana ulimwenguni sasa upo katika mataifa 180 .Mtandao huo ulianzishwa mwaka wa 2009 na ulinunuliwa na Facebook mwaka wa 2014 kwa kima cha takribani dola milioni 20,000 za kimarekani .
Wakati huo jaribio lilifanywa la kutoza dola moja ya kimarekani kama ada ya matumizi ya kila mwaka lakini pendekezo hilo lilipuuzwa kama 'Lililopitwa na wakati'.
Wakati kuinunua WhatsApp Zuckerberg aliahidi kutii nguzo mbili muhimu kuu za sera ya mfumo huo wa ujumbe: Kutojumuisha matangazo na kutotumia maelezo ya watumiaji .
Kisha,kama anavyoeleza Sáenz ,tangu mwaka wa 2016 ahadi hiyo ikaanza kuvunjwa na kuruhusu muunda mpya wa kibiashara wa mtandao huo
"Facebook ilifanya ununuzi huo ikijua kwamba ulikuwa na ghala kubwa la maelezo ya watu na lingepanuliwa na ndio maana kuanzia mwaka wa 2016 Whatsapp imeanza kutoa maelezo ya watumiaji.
Data hii kwa kweli ndio inayolisha muundo wa kibiashara wa Facebook' anasema Saenz, ambaye ni mratibu wa mipango wa Wakfu wa Karisma ,shirika ambalo linafuatilia shughuli na ustawi wa teknolojia mpya lenye makao yake Colombia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Facebook ilifanya uwezekaji mwingine mara mbili mwaka wa 2020 na kuifanya thabiti WhatsApp kama sajili ya pesa zake .
Ilitumia dola bilioni 5.7 za kimarekani kununua kampuni ya kidijitali ya India Jio Plattforms na muda mfupi baadaye ikatoa dola bilioni moja kununua Kustomer, kampuni inayofanya ununuzi na uuzaji mtandaoni .
Dhamira kulingana na wataalam ni kufanikisha kutumiwa kwa WhatsApp kama kituo cha malipo na bila shaka kutengeza faida zaidi .












