Wanasayansi wabaini watu wanaoweza kudhibiti virusi vya HIV nchini DR Congo bila kutumia dawa

Wanasayansi wanaamini kwamba huenda wanakaribia kupata tiba ya virusi vya HIV kufuatia matokeo ya utafiti yaliotolewa siku ya Jumanne.

Utafiti ulitathmini sampuli zilizokusanywa 1987 na 2019 na kubaini kwamba asilimia nne ya watu wanaoishi na virusi vya HIV katika taifa la Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC , waliweza kukandamiza kiwango cha virusi hadi kufikia kiwango cha chini zaidi bila kutumia dawa.

Kulingana na mwandishi wa BBC, Rhoda Odhiambo kwa miaka kadhaa sasa wanasayansi wamekuwa wakifanya kazi ya kutafuta kinga ya HIV.

Na sasa utafiti mpya , uliofanywa na kampuni ya Afya kwa jina Abbott umewapatia tabasamu wanasayansi.

Ni kuhusu kundi dogo la watu kwa jina ''HIV Controllers''{ Wadhibiti wa HIV}.

Ni watu ambao wameonesha kukandamiza virusi vya ugonjwa huo kutokana na jeni zao zisizo za kawaida.

Utafiti huo ulibaini kwamba idadi ya watu wanaoishi na HIV nchini DR Congo kati ya 1987 hadi 2019, asilimia nne walikuwa na uwezo wa kudhibiti virusi hivyo.

Dkt. Mary Rodgers ,kiongozi wa utafiti huo aliambia BBC kwamba wanasayansi tayari wanajua kuhusu kundi hilo.

Lakini hawajawahi kuona viwango kama hivyo vya juu katika taifa moja.

Asilimia nyengine moja ya watu wanaoishi na HIV nchini Cameroon pia walibainika.

Hatahivyo, utafiti wao haukuonyesha jinsi wanavyoweza kukandamiza virusi hivyo kwa hali ya kawaida.

Kwa sasa watu wanaoishi na HIV wanalazimika kutumia dawa kila siku ili kuweza kuafikia hilo.

Dkt Rodgers alisisitiza umuhimu wa kufanya utafiti zaidi kuhusu idadi hii ya watu na katika mataifa mengine , baada ya utafiti wa awali kuonyesha kwamba watu hawa wanaweza kupoteza kinga huku Ugonjwa huo ukiendelea kuwaathiri.

HIV iligunduliwa DRC miongo minne iliopita .

Na sasa kufuatia utafiti huu, wanasayansi wanaamini kwamba taifa hili linaweza kuwa na majibu kudhibiti ugonjwa huo ambao unawaathiri wanawake wengi walio na umri mdogo na wasichana katika eneo la jangwa la sahara barani Afrika.