Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini hali ya usalama imeendelea kuwa tete nchini DRC?
- Author, Maryam Dodo Abdalla
- Nafasi, BBC SWAHILI
Mkasa wa hivi karibuni wa kuuawa balozi wa Italia nchini DRC, Luca Attanasio pamoja na walinzi alioandamana nao kutoka mji wa Goma - Kivu ya kaskazini, kumezusha upya mjadala kuhusu usalama au ukosefu wa usalama katika taifa hilo lililoathirika na mizozo ya ndani na vita vya miaka mingi.
Balozi Attanasio alikuwa miongoni mwa watu 7 waliosafiri katika magari mawili ya Umoja wa mataifa WFP kutoka Goma kukagua miradi ya utoaji chakula katika shule kadhaa huko Rutshuru.
Katibu mkuu Antonio Guterres ameshutumu vikali shambulio hilo na kutaka serikali ya Congo ifanye uchunguzi kwa wepesi.
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ilifuatia taarifa hizi kwa kutangaza masharti ya usafiri.
Serikali imepiga marufuku usafiri wa mabalozi na wajumbe wakuu wa kidiplomasia nje yam ji mkuu Kinshasa pasi kuarifu mamlaka awali.
Kwa upande wake Umoja wa mataifa nao umetangaza kuwa utaidhinisha uchunguzi wa kina dhidi ya mauaji hayo.
Swali kubwa ni je hatua hizi litaibadili hali ya usalama Congo?
Mauaji yalivyojiri:
Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa, kundi hilo liliondoka Jumatatu mwendo wa saa tatu asubuhi.
Kundi la watu waliojihami kwa silaha lilisimamisha magari waliokuwemo balozi na wenzake mwendo wa saa nne na robo na kuwalizimisha abiria kushuka garini.
Mojawapo wa madereva aliuawa papo hapo.
"Abiria wengine sita walilazimishwa kuingia katika kichaka kilichokuwa karibu wakishikiwa bunduki ambapo kulizuka ufyetulianaji wa risasi", WFP lilisema.
Ni katika makabiliano hayo ndipo balozi Attanasio na mlinzi wake Vittorio Lacovacci, walijeruhiwa vibaya na kufariki.
Ahadi ya Tshisekedi
Ukosefu wa usalama ni moja wapo ya changamoto kubwa anayokabiliana nayo rais Tshisekedi nchini Congo huku akijaribu kumaliza vurugu katika eneo la mashariki mwa taifa - jambo ambalo pia ni ahadi kuu aliyoitoa wakati wa kampeni zake za kuchaguliwa kuwa rais.
Wakati wa kuapishwa, rais Tschisekedi aliahidi "kujenga Congo imara, na kuifanya kuwa ya maendeleo, amani na usalama ".
Zaidi ya mwaka mmoja leo baada ya Tshisekedi kuingia uongozini, wananchi bado hawajihisi salama zaidi ya hali ilivyokuwa awali.
Wanaharakati wa haki za kibinadamu na mashirika ya kiraia wanasema kuwa ikiwa serekali itafanikiwa kutokomeza mashambulizi katika maeneo hayo, basi itakuwa ushindi mkubwa kwa Tshisekedi.
Kuendelea kuwepo kwa waasi.
Mashambulio yamekuwa yakiendelea. Jimbo la Kivu ya kaskazini sehemu ambako shambulio hilo limetokea nimojawapo ya maeneo yalio na hatari kubwa nchini Congo linalopakana na Mbuga ya kitaifa ya Virunga.
Ni eneo lililo na makundi ya waasi wa ndani na hata nje ya nchi kama vile Rwanda na Uganda.
Kundi la FDLR nimojawapo wa makundi hayo, ambalo lilitekeleza mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994 na wapiganaji wake kukimbilia DRC.
Kundi jingine lijulikanalo kutekeleza mashambulio dhidi ya raia katika eneo hilo ni lile la ADF ambalo wafuasi wake ni wa kutokea nchini Uganda.
Yapo na mengine makundi madogo yalioundwa na raia kwa dhamira ya kuzikinga jamii dhidi ya mashambulio ya wasi wa nje, lakini kadri muda ulivyosogea dhamira yao ilibadilika na baadhi wakaanza kutekeleza uhalifu kwa maslahi yao.
Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ndio sehemu ilioathirika pakubwa na ukosefu wa usalama.
Shirika la Umoja wa mataifa linalowashughulikia wakimbizi limetaja kwamba Zaidi ya raia 2000 wameuawa na makundi ya waasi waliojihami kaskazini na kusini mwa Kivu pamoja na katika jimbo la Ituri mwaka uliopita.
Serikali ya Congo imewashutumu waasi wa FDLR kutekeleza mauaji ya balozi wa Italia na wenziwe sita.
Hatahivyo msemaji wa kundi hilo la waasi ameieleza BBC kwamba kuna Zaidi ya makundi 100 yanayohudumu katika eneo hilo, na haelewi kwanini kundi lake ndilo lililotuhumiwa kwa shambulio hilo.
"Hatukuhusika katika mauaji hayo maovu," Cure Ngoma wa kundi la FDLR ameielezea BBC.
Kadhalika kundi hilo limeongeza kwamba uchunguzi utakaofanywa unapaswa kuzingatia kwamba eneo ambako shambulio limetokea ni sehemu ambapo majeshi ya Congo na Rwanda yalikuwa yakihudumu.
Mmojawapo ya mapendekezo ambayo yametolewa katika juhudi za kujaribu kupata suluhu la kiuslama la kudumu ni serikali kufanya mazungmzo na wapiganaji hasa wale wa kundi la ADF.
Mchanganuzi wa maswala ya kisiasa na kijamii katika mji wa Goma bwana Apollo Msambia anaamini kwamba wakati umewadia kwa serikali ya Kinshasa kuanzisha mazungmzo ya amani na utawala wa rais Yoweri Museveni wa Uganda kuhusu waasi wa ADF.
"Rais Tshishekedi anatakiwa kuanzisha mazungumzo na mwenzake Museveni na kuona jinsi waasi hawa wa ADF wanavyoweza kutoka kaskazini mwa DRC na kurejea Uganda, kwa vile sasa imeonekana kwamba wameshindwa kukabiliana nao kijeshi" asema Bw. Msambia.
Ushindi wa FARDC
Jeshi la serikali FARDC kwa ushirikiano na vikosi vya Umoja wa mataifa MONUSCO, limekuwa likiendeleza operesheni dhidi ya waasi, kujaribu kuirudisha amani, utulivu na kuondosha hofu nchini.
Hatahivyo, sio kwamba hakujakuwa na changamoto ndani ya jeshi lenyewe.
Rais Félix Tshisekedi, amefanya mageuzi katika muundo wa jeshi.
Kadhalika aliagiza jeshi kuhamishia ngome katika mji wa Beni, ambao umekuwa kitovu cha mashambulizi ya waasi wa ADF.
Baadhi ya wanajeshi wamebadilishwa, na hivyo kuleta nguvu mpya katika mapambano dhidi ya wanamgambo.
Mabadiliko haya huenda yanadhihirisha kudorora kwa hali ya usalama katika eneo hilo la mashariki.
Vikosi vya FARDC na MONUSCO vimewatambua, kuwashambulia, kuwakamata na hata kwa kiasi Fulani kufanikiwa kuzidhibiti ngome kuu za waasi wa ADF.
Jukumu la Monusco
Kikosi cha kulind amani cha Umoja wa mataifa kimekuwepo Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo tangu 1999.
Ni mojawapo ya operesheni kubwa za kulinda amani duniani inayojumuisha maafisa takriban 18,000.
Vikosi vya MONUSCO vimeanza kuhudumu Julai 2010, kilipopokea jukumu kutoka kikosi cha kulinda amani kilichokuwepo awali cha Umoja wa mataifa nchini Congo (MONUC).
Umoja wa maatifa umebaini kwamba kuna mipango kwa MONUSCO kuondoka kwa awamu, kutoka nchini humo iwapo utulivu utakuwepo.
Serikali ya DRC inalikubali hilo, licha ya kwamba haijulikani ni muda gani itachukua kwa utawala kuimarisha miongoni mwa mengine, taasisi zake za ulinzi, ili kudumisha kikamilifu usalama wa nchi.
Na wakati mipango hii ya kuondoka kwa vikosi vya kulinda amani kutoka DRC inaendelea, baraza la usalama la Umoja wa mataifa linaeleza kwamba kazi kubwa inasalia kuiweka nchi hiyo katika muelekeo wa utulivu wa muda mrefu, na maendeleo ya kudumu.