Waridi wa BBC: 'Ndoa yetu imetokana na mapenzi ya dhati'

Wanandoa Susan Njogu Erin na Philiph Elin

Chanzo cha picha, Susan Njogu Elin

Maelezo ya picha, Wanandoa Susan Njogu Eling na Phillip Eling
    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili

Tangu Susan Njogu Eling alipoamua kufunga ndoa, amekuwa akishambuliwa na wengi kutokana na uamuzi wake.

Wengi hudai alifanya uamuzi huo kutokana na tamaa ya pesa, jambo ambalo kamwe anasema halikumuingia akilini.

Erin, 28, ameishi na Phillip Eling kama mume na mke kwa miaka miwili sasa.

Uamuzi huo ni jambo ambalo linalozungumziwa zaidi na baadhi ya marafiki zake wa karibu.

'Sikutarajia itakuwa gumzo'

Kiini kikuu hasa kimelenga maumbile ya mume wake kwani sio kama ya mwanamume wa kawaida.

Mume wake anaishi na ugonjwa ambao unaathiri misuli na viungo vyake.

Hali hii inajulikana kama Bethlem Myopathy - na kwa kweli hali hiyo imeashiria kuwa mume wake ana ulemavu kwa kiasi kikubwa.

Wanandoa Susan Njogu Erin na Philiph Elin

Chanzo cha picha, Susan Njogu Elin

Maelezo ya picha, Mume wake anaishi na ugonjwa ambao unaathiri misuli na viungo vyake

Bwana Phillip hawezi kutumia mikono yake wala miguu yake na hata sehemu ya shingo lake.

Mume wake hawezi kutembea, kuinua chochote wala hata kujihudumia mwenyewe kwa mfano kula chakula au hata kuchana nywele zake mwenyewe.

Kimsingi ni kuwa maisha ya mume wake yanazungukia kukaa kwa muda mwingi katika kiti cha magurudumu.

"Sikudhani kuwa uamuzi wangu wa kibinafsi kumpenda mume wangu ungekuwa gumzo mitaani," anasema.

"Maoni yaliouma zaidi ni yale yalioelekea kuwa nilikubali kuolewa na Phillip kwa sababu yeye kutoka asili ya kizungu na ana fedha nyingi."

Kwa mtu anayekutana na Susan na mume wake Phillip kwa mara ya kwanza atagundua kuwa wachumba hawa wawili wanamapenzi ya ajabu.

Haipiti dakika nyingi kwa wapenzi hawa wawili kabla hawajakumbatiana na kupeana busu.

Susan analitaja kama jambo la kawaida katika maisha ya wanandoa hawa wawili.

Ila safari ya ndoa yao kwa upande mwengine ni kielelezo chanya katika jamii hasa wakati unapokutana na mwanamke ambaye hana matatizo yeyote ya maumbile na anakubali kumpenda na kumtunza mume mwenye ulemavu mkuu maishani mwake.

Kukutana kwa njia isiyo ya kawaida

Susan Njogu Elin

Chanzo cha picha, Susan Njogu Elin

Maelezo ya picha, "Sikudhani kuwa uamuzi wangu wa kibinafsi kumpenda mume wangu ungekuwa gumzo mitaani"

Susan alisafiri kutoka kaunti ya Nakuru nchini Kenya hadi nchini Austalia akitafuta masomo maalum katika fani ya matibabu.

Alipofika nchini humo alibadilisha kusudi lake na kuanza masomo spesheli ya kuelewa maisha ya watu wanaoishi na ulemavu.

Baada ya kuhitimu, aliamua kutafuta ajira katika kampuni moja iliyokuwa inashughulika na maswala ya walemavu.

Aliandika maombi ya kazi na kuyatuma.

Siku mmoja aliitwa kwenye usaili na hapo ndipo alipokutana na mume wake mara ya kwanza akiwa mmoja wa wale waliokuwa kwenye jopo la kumhoji kikazi.

Baada ya hafla hio Susan alirejea nyumbani kusubiri uamuzi.

Baada ya siku mbili hivi alipokea barua pepe ya kibinafsi kutoka kwake Philiph iliyokuwa inakusudia kumwalika kwa mkutano wa kirafiki.

Kukutana kwao katika ukaribu mkuu na hapo ndipo penzi lilianza kuota na kukolea kati ya wapenzi hawa wawili.

Bwana Philiph hawezi kutumia mikono yake wala miguu yake na hata sehemu ya shingo yake

Chanzo cha picha, Susan Njogu Elin

Maelezo ya picha, Bwana Philiph hawezi kutumia mikono yake wala miguu yake na hata sehemu ya shingo yake

"Kusema ukweli tangu nikiwa binti nilikuwa najipata nikiwa na umakini sana nilipokuwa karibu na watu waliokuwa wanaishi na ulemavu. Nilijipata nikitaka kuwa wa msaada au kuwafanyia mema watu waliokuwa na upungufu wa mwili sehemu yoyote nilipokuwa," anakumbuka Susan

Na kwa hio sio ajabu kuwa urafiki wake na Phillip haukukumbwa na changamoto hiyo ya yeye kujiuliza ni vipi wataishi kama mume na mke na mtu ambaye alikuwa kila wakati anaishi kwenye kiti cha magurudumu.

Baada ya muda Phillip alikuwa amemtambulisha kwa jamaa zake na pia alikuwa tayari alikuwa amemuomba wafunge ndoa.

Kufunga ndoa

Susan hakuwa na budi ila kuwaeleza jamaa zake nchini Kenya mpango wake.

Alitaka sana kujua iwapo baba na mama mzazi wangemkubali afunge ndoa na mtu aliyekuwa anaishi na ulemavu.

"Kwa bahati nzuri nilipowaeleza wazazi wangu hawakupingana na chaguo langu , wala hakuna siku walinidunisha kutokana na uamuzi wangu ila walinipa ushauri wa kuendelea mbele ikiwa mimi na mchumba wangu wakati huo tulikuwa tumefanya uamuzi," Susan anakumbuka

Mwaka wa 20018 Susan na Phillip walifunga ndoa na wachumba hawa wawili walionekana kujawa na furaha na msisimko mkuu wa kuwa pamoja.

Tangu Susan Njogu Elin alipoamua kufunga ndoa, amekuwa akishambuliwa na wengi kutokana na uamuzi wake.

Chanzo cha picha, Susan Njogu Elin

Maelezo ya picha, Tangu Susan Njogu Eling alipoamua kufunga ndoa, amekuwa akishambuliwa na wengi kutokana na uamuzi wake.

Kushambuliwa katika mitandao ya kijamii

Kizazaa kilianza pale walipoweka picha zao kwenye mtandao wa kijamii kila aina ya semi na jumbe zilifurika kwenye mitandao yao.

Wengi walilenga kumdunisha na kumyooshea kidole cha lawama kwa kuchukua hatua ya kuolewa na 'mlemavu'.

"Mtandao wa kijamii ulifurika na mambo ambayo yalinishangaza mno, kwa mfano kuna wale waliosema bila aibu kuwa mimi nilikubali kufunga ndoa kama tiketi ya kupata fedha na pia viza ya kuishi Australia. Wengine nao walikuwa wanasema kuwa niliingia kwenye ndoa hio kwa lengo la kumuua mume wangu kwani yeye anahitaji usaidizi wa hali ya juu kutoka kwa watu waliokaribu naye,"Susan anakumbuka

Susan Njogu Elin

Chanzo cha picha, Susan Njogu Elin

Siku za kwanza baada ya kufunga ndoa, zilikuwa za wawili hawa kujenga mikakati ya kukabiliana na maoni ya uchochezi na matusi yaliyokuwa yanaibuliwa kutoka mitandao wa kijamii.

"Maoni kwenye mitandao ya kijamii yalinisukuma kujiuliza iwapo niliufanya uamuzi wa busara au la, ila kila wakati nilipokuwa na mtizama mume wangu nilihisi amani na furaha. Nilipiga moyo konde na kuamua kufunga masikio yangu na macho yangu iliniweze kuishi kwa ndoa yangu bila uchochezi wa watu ," Susan anasema

Kulingana na Susan kueleza mapenzi aliyonayo kwa mume wake Phillip kwa dunia sio jambo ambalo atafaulu kulifanya - ila yeye anahisi kuwa hakuna kizingiti chochote ambacho kinaweza kumtenganisha na mume wake.

"Wengi ni wale ambao huniuliza maswali mengi kuhusu chaguo langu, wameniuliza maswali kama ikiwa nilikuwa timamu nikifanya uamuzi wa ndoa , ila kwa watu wa jamii yangu na pia kwa upande wa mume wangu hakuna aliyenyoosha kidole cha lawama kwetu," Susan anasema

Mwanadada huyu anasema kuwa ndoto na pia azma walizonazo pia zimeongezea ladha ya ndoa yao kwani kwa upande mmoja Susana anafanya kazi na watu wanaoishi na ulemavu nchini Austalia.

Mumewe Phillip naye amekuwa balozi anayetetea maswala mbalimbali yanayohusu walemavu nchini humo.

Susan Njogu Elin

Chanzo cha picha, Susan Njogu Elin

Kuelewa matatizo

Susan anasema kuwa alifahamu alichokuwa amechagua tangu alipokubali kuchumbiwa na mume wake - hali anayoishi nayo Phillip Bethlem myopathy - humfanya muathirika kuzidi kupoteza nguvu ya misuli na pia kuathiri viungo vya mwili kwa kiasi kuwa kila kuchao huzidi kuwa vigumu mno.

Kwa mfano utapata kuwa mikono yake mumewe haina uwezo wa kufunguka au kunyooka vyema. Vivyo hivyo sehemu za miguu yake.

waridi

Kwa hivyo inahitaji Susan kuhakikisha kuwa anamsaidia mumewe kila kuchao katika shughuli kama kupiga mswaki, kuchana nywele na pia kumpa chakula.

"Ninaposikia watu wakizungumza kuhusu maisha yangu na Phillip mimi husikia uchungu mno kwa kuwa Phillip ni mume hodari mno licha ya mapungufu yake mimi nimejitolea kuhakikisha kuwa changamoto za ugonjwa anaoishi nao zimepungua," anasema Susan.

Mwanadada huyu amesema kuwa alikutana na mume wake akiwa tayari anapambana kuishi na hali hiyo, na aliona jinsi familia yake ilivyokuwa imemtunza kwa kila hali.

Susan anasema kuwa kwa kuishi karibu na Phillip anaelewa na kung'amua matatizo ya walemavu.

Hasa anasema kuwa kumuona mumewe na uchungu humpa machozi na kamwe anasema kuwa hatachoka kumpenda na kumhudumia licha ya maswali na maneno ya watu .

Susan na Phillip pia waliamua kudhihirishia ulimwengu jinsi wanavyoishi kwa kufungua akaunti katika mtandao wa YouTube.

Huwa wanaangazia matukio na masuala mbalimbali kuhusu maisha yao hapo.