Mapinduzi ya Myanmar: Aung San Suu Kyi afunguliwa mashitaka baada ya kuondolewa madarakani

Aung San Suu Kyi anasalia chini ya mikono ya jeshi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Aung San Suu Kyi anasalia chini ya mikono ya jeshi

Polisi nchini Myanmar wamefungua mashtaka kadhaa dhidi ya kiongozi wa kiraia mteule, Aung San Suu Kyi baada ya mapinduzi ya kijeshi ya siku ya Jumatatu.

Amerudishwa rumande hadi Februari 15, hati za polisi zimeonesha

Mashtaka yanahusisha ukiukaji wa sheria za uingizaji na usafirishaji, umiliki wa vifaa vya mawasiliano kinyume cha sheria.

Haijulikani yuko wapi, lakini imeripotiwa kuwa anashikiliwa kwenye makazi yake, Nay Pyo Taw.

Rais aliyeondolewa Win Myint pia ameshtakiwa, nyaraka zinaonesha - katika kesi yake kuhusu kukiuka sheria zinazopiga marufuku mikusanyiko wakati wa janga la Covid. Pia amerudishwa rumande kwa wiki mbili.

Si Rais wala Bi. Suu Kyi waliosikika tangu jeshi lichukue madaraka mapema tarehe 1 mwezi Februari.

Mapinduzi, yaliyoongozwa na mkuu wa majeshi Min Aung Hlaing, yameshuhudia kuwekwa kwa jeshi kutawala chini ya hali ya dharura ya mwaka mmoja.

Wanajeshi walihalalisha kitendo chake kwa madai ya udanganyifu katika uchaguzi uliopita wa mwezi Novemba, ambapo chama cha National League for Democracy (NLD) cha Bi Suu Kyi kilishinda

Yapi maelezo ya mashtaka hayo?

Mashtaka hayo yamo kwenye hati ya polisi - inayoitwa Ripoti ya Kwanza ya awali - iliyowasilishwa kortini.

Inadai kwamba Bi Suu Kyi aliagiza na kutumia vifaa vya mawasiliano visivyo halali - vilivyopatikana nyumbani kwake Nay Pyi Taw.

Hati ya polisi inaonesha mashtaka dhidi ya Aung san Suu Kyi

Chanzo cha picha, MYANMAR POLICE

Alirudishwa rumande "kuhoji mashahidi, kuomba ushahidi na kutafuta wakili wa kisheria baada ya kumhoji mshtakiwa," hati hiyo inasema.

Bw.Win Myint anashtakiwa, chini ya sheria ya udhibiti wa majanga ya kitaifa, kwa kukutana na wafuasi katika msafara wa magari 220 wakati wa kampeni na kukiuka masharti ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

Kuna upinzani gani kwenye mapinduzi?

Madaktari katika eneo la Mandalay walitumia saluti ya vidole vitatu kuonesha kutofurahishwa kwao na mapinduzi hayo

Chanzo cha picha, MPA

Maelezo ya picha, Madaktari katika eneo la Mandalay walitumia saluti ya vidole vitatu kuonesha kutofurahishwa kwao na mapinduzi hayo

Wanaharakati nchini Myanmar wameitisha mgomo.

Wahudumu wengi wa hospitali wanaacha kufanya kazi au wanaendelea na kazi wakiwa wamevalia ishara za kuonesha mgomo na ghadhabu kuhusu ukandamizaji wa demokrasia nchini Myanmar.

Wafanyakazi wa idara za afya wanashinikiza kuachiwa kwa Bi.Suu Kyi.

Wanavaa utepe mwekundu au nyeusi zikiwa na picha ya alama za vidole vitatu alama iliyotumiwa na waandamanaji mwaka jana nchini Thailand.

Mitandaoni, wengi walibadili picha za utambulisho kwenye mitandao ya kijamii kuwa rangi nyekundu.

''Mgomo ni moja ya njia ambazo vijana nchini Myanmar wanatumia kama kampeni nchi nzima, mwanzilishi wa mtandao wa vijana wa Yangon, Thinzar Shunlei aliiambia BBC.

''Wanatoa wito hasa kwa wafanyakazi wa Umma, kuacha kufanyia kazi serikali, na jeshi la junta.''

Kundi la mtandao wa Facebook limekuwepo kwa ajili ya kuratibu kampeni hiyo.

Lakini kumekuwa na viashiria vichache vya maandamano makubwa. Siku ya Jumanne usiku, madereva walipiga honi katika mji wa Yangon, na wakazi waligonga vyombo vyao vya kupikia.

Myanmar imekuwa kimya baada ya maandamano, huku wanajeshi wakiwa kwenye doria na kutekelezwa kwa marufuku ya kutotoka nje nyakati za usiku.

Pia kumekuwa na maandamano ya kuunga mkono jeshi-watu karibu 3,000 wanashiriki, shirika la habari la AP limeripoti.

Aung San Suu Kyi

Chanzo cha picha, Getty Images

Nchi nyingine zimesema nini kuhusu mapinduzi?

Kundi la nchi saba zilizo na nguvu kiuchumi limesema ''linasikitishwa'' na tukio la mapinduzi nchini humo na kutoa wito wa kurejea kwa demokrasia.

''Tunatoa wito kwa jeshi kumaliza hali ya dharura iliyowekwa, kurejesha mamlaka kwa serikali iliyochaguliwa kidemokrasia, kuwaachia huru waliokamatwa na kushikilia bila haki na kuheshimu haki za binadamu,'' taarifa iliyotolewa jijini London ilieleza.

Nchi hizo saba ni Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani.

Lakini jitihada za Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kufikia makubaliano huku China pekee ikiwa haikuridhia. China ni moja ya wanachama wa kudumu wenye kura ya turufu kwenye baraza hilo.

China imekuwa ikitahadharisha kuwa kuweka vikwazo au shinikizo za kimataifa kutafanya mambo kuwa mabaya zaidi nchini Myanmar.

Beijing imekuwa ikilitetea taifa hilo kutokana jicho la jamii ya kimataifa. Inalitazama taifa hilo kuwa muhimu sana kiuchumi na ni moja wa rafiki akubwa wa Myanmar .

Urusi imekuwa ikiilinda Myanmar dhidi ya ukosoaji ndani ya Umoja wa Mataifa kuhusu udhibiti wa jeshi dhidi ya jamii ndogo ya Kiislamu ya Rohingya.