Waziri Jafo: Tunaanza kampeni ya kupiga nyungu juma zima

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa, Selemani Jafo ametangaza kuanza kampeni ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona juma lijalo.

Waziri Jafo ameyasema hayo akiwa katika ziara ya Rais wa Tanzania John Magufuli mkoani Tabora, katikati mwa Tanzania, alipokuwa akitoa salamu kwa wakazi wa mkoa huo.

Akizungumzia janga la virusi vya corona amesema siku ya Jumatatu kampeni ya kupambana na janga hilo itaanza.

''Hapa corona haina nafasi, tutaendelea kumuomba Mwenyezi Mungu, kama Mh.Rais ulivyotuelekeza na umesema watu wajifukize sana, Na Rais naomba nikwambie Jumatatu tunaanza kampeni nyingine ya juma zima season three (awamu ya tatu), nyungu kama kawaida, tunajifukiza, tunakula matunda, tunamuomba Mungu, tunaanza tarehe moja mpaka tarehe saba, hatupoi kazi inaendelea, uchumi wetu lazima usimame'' Alisema Waziri Jafo.

Kauli hii imekuja wakati kukiwa na aina mpya ya virusi vya corona aina ya Afrika Kusini, ambavyo vimekuwa vikienea katika nchi za Kiafrika.

Siku ya Ijumaa, msemaji Mkuu wa serikali nchini Tanzania Dkt. Hassan Abbas alisema Tanzania inazingatia miongozo yote ya tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona na hata wakati huu ambao dunia inapambana na wimbi la pili la maambukizi ya virusi hivyo.

Akihojiwa na kitoa cha redio cha EFM kilichopo jijini Dar es salam, Dkt. Abbas alisema "Sisi Tanzania msimamo wetu ni ule ule,tunafahamu tatizo lipo duniani na dunia inahangaika lakini cha kwanza watanzania waondoe hofu wizara ya afya ilishatoa miongozo, ile miongozo bado ipo haijawahi kufutwa kuna tahadhari za kuchukua hivi wewe kunawa mikono mpaka covid? Alihoji Dkt Abbas.

'' Tulikuwa tuna nawa sana shule baadaye tukaacha kwahiyo kuna zile tahadhari kama alivyosema juzi Mh Rais tuendelee kuzichukua lakini Tanzania tunaamini tumedhibiti haya maambukizi kwa njia zetu za kisayansi na kumshukuru Mwenyezi Mungu''.

''Unajua Tanzania watu wanasahau wanafikiri tulidharau sana huu ugonjwa tulichukua hatua zote dunia ilizokuwa inataka isipokuwa kujifungia ndani maana kuna watu wanatamani sana kufungiwa ndani sijui kuna nini huko ndani" Alisema Bw. Abbas.

WHO ilisema nini hapo awali?

Siku moja baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kutaka wizara ya afya kutokimbilia chanjo ya corona bila kujiridhisha, Shirika la Afya Duniani WHO liliitaka nchi hiyo kujiandaa na chanjo ya Corona kama mataifa mengine duniani.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao,mkuu wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshdiso Moeti amesema kuwa Tanzania inatakiwa kutumia mwanya wa upatikanaji wa chanjo kwa faida ya wananchi na kanda ya Afrika mashariki kwa ujumla.

''Tumeanza kuwasiliana upya na ngazi za juu za uongozi, na tunatoa mchango wetu kama ilivyokua hapo mwanzo, na tunataka kushirikiana na Tanzania, kwa niaba ya watu wa Tanzania, nchi jirani na dunia kwa ujumla. Sehemu ya mawasiliano yetu na Tanzania ni kukumbusha serikali kuwa, hii ni sehemu ya makubaliano ya kanuni za afya za kimataifa ambapo nchi wanachama wamekubali kwa pamoja kuzuia kusambaa kwa magonjwa'' anasema Dkt. Moeti.

WHO inasema kuwa imekua ikitoa mchango na kuwasiliana na serikali ya Tanzania kuanzia mwanzo wa janga hili la Corona.

Shirika hilo pia limesisita Tanzania kutoa takwimu za mwenendo wa Corona nchini Tanzania ili iwe rahisi katika kupambana na kuzuia maambukizi mapya.

''Moja ya makubaliano ya wanachama ni kutoa takwimu za mwenendo wa ugonjwa, nimewakumbusha serikali ya Tanzania na ninayo kumbukumbu kwa maandishi kuwa wao ni sehemu ya wanachama hivyo wanatakiwa kuitikia wito huu. Tuna imani kuwa mawasiliano yetu kuhusu chanjo yatazingatiwa ili kukabili maambukizi ya virusi," ameongezea Dkt. Moeti.