Ilunga Khalifa: Mwanamuziki wa Tanzania maarufu CPWAA kutoka kundi la Parklane aaga dunia

Muda wa kusoma: Dakika 1

Msanii wa Tanzania Ilunga Khalifa maarufu CPwaa amefariki mapema siku ya Jumapili katika hopsitali ya kitaifa ya Muhimbili ambapo alikuwa akipatiwa matibabu.

Kulingana na gazeti la The Citizen nchini humo, CPwaa alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo akiugua homa ya mapafu iliosababisha kifo chake.

CPwaa aliyewahi kujishindia tuzo kadhaa alianza muziki katika kundi la Park Lane lililoshirikisha msanii Suma Lee.

Wawili hao waliachilia vibao vilivyogonga vichwa vya habari kikiwemo kile cha 'Nafasi Nyingine' na 'Aisha'.

Hatahivyo wawili hao walitengana na kuachilia vibao Action, Problem, So Pwaa, Six in the Morning, miongoni mwa vinginevyo.

Wengi wa wafuasi wake katika mitandao ya kijamii waliomboleza kifo chake.

Wanamuziki wenzake kama vile Profesa Jay pia walimuomboleza

CPwaa alikuwa miongoni mwa wanamuziki waliokuwa na ushawishi mkubwa wa mtindo wa Hip Hop kutoka Marekani nchini Tanzania.

Alitoa albamu kwa jina 'The Album' mwaka 2013 ambayo ilikuwa na nyimbo 15.

Nje ya muziki Cpwaa alivutiwa sana na kazi za Teknolojia akiwa na hamu katika masuala ya ICT, VAS, kazi za kidijitali , miongoni mwa masuala mengine ya teknolojia.