Matokeo ya uchaguzi Tanzania 2020: Changamoto gani inamkabili Rais mpya wa Zanzibar?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
Asubuhi ya leo, Alhamisi Oktoba 2, 2020 Dkt Hussein Mwinyi amekula kiapo cha urais wa visiwa vya Zanzibar.
Dkt Mwinyi anakuwa kiongozi wa nane kuiongoza Zanzibar ambayo ni sehemu ya Tanzania.
Siku ya Alhamis Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilimtangaza Dkt Mwinyi kuwa mshindi wa kiti cha Urais katika visiwa hivyo kwa 76% dhidi ya mpinzani wake wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad aliyepata 19% ya kura hizo. Huu ni mpishano mkubwa sana wa kura kwa kuzingatia matokeo ya chaguzi zilizopita za Zanzibar.
Ni ushindi mnono kwa Chama cha Mapinduzi (CCM). Ukiwahakikishia miaka mengine mitano ya kuzishika hatamu kuiongoza Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kabla ya kumwangalia Dkt. Mwinyi wakati akielekea Ikulu, kwanza tudurusu mazingira ya uchaguzi wenyewe.
Sura ya uchaguzi uliomuweka madarakani
Kauli ya Ubalozi wa Marekani kuhusu uchaguzi wa Tanzania, imegusia malalamiko muhimu juu ya uwepo wa kura feki, vitisho, kukamatwa kwa waandamanaji na wagombea, watu kupigwa vibaya pamoja na taarifa za mauwaji.
Pia, imeangazia kuzuiwa kabisa na kutatizwa huduma za mitandao ya kijamii, madai ya masanduku ya kura kuwekwa kura kabla upigaji kura kuanza na kuzuiwa mawakala wa vyama vya siasa kufanya majukumu yao katika vituo.
Kauli juu ya matukio ya namna hiyo haijatolewa na Ubalozi pekee, vyama vya upinzani kile cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema na ACT Wazalendo na baadhi ya vyama vingine vya upinzani vimeelezea mambo yanayofanana na hayo kwamba yalitendeka katika uchaguzi upande wa Bara na visiwani.
Hata hivyo madai hayo yamekanushwa na mamlaka, huku waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki wakisema uchaguzi umefanyika katika mazingira yaliyotakiwa.
Katika kisiwa cha Pemba uchaguzi huu umegubikwa na malalamiko ya watu kupigwa, kujeruhiwa na kuvamiwa katika majumba yao. Kwa mujibu wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, zaidi ya watu kumi wameuwawa Pemba na Nungwi, Unguja.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wakaazi, vikosi vya usalama vilisambazwa kwa wingi usiku na mchana vikifanya doria. Baadhi ya doria ndizo ambazo wananchi wanaeleza zilizalisha maafa kwa wapendwa wao.
Jeshi la Polisi kupitia IGP Simon Sirro limekanusha kutokea kwa mauwaji. Lakini halikufafanua juu ya picha na video zinazosambaa katika mitandao zinazoelezwa kuwa ni maiti zilizopigwa risasi Pemba.
Pia, serikali ya SMZ haijoa kauli yoyote kuhusu majeruhi wa vipigo na risasi ambao taarifa zinaeleza wako katika hospitali za serikali wakipatiwa matibabu. Matukio yote yenye sura ya ukiukwaji wa haki za binaadamu yana hitaji majibu ya kuridhisha.

Changamoto kubwa inayomkabili
Dkt. Mwinyi ni kiungo imara na muhimu kati ya serikali ya Zanzibar na ile ya Muungano. Hili lina maana kuwa muundo uliopo wa Muungano utaendelea kuwa katika mikono salama ya viongozi wa pande zote mbili.
Wakati Waziri huyo wa zamani wa Ulinzi katika serikali ya Muungano, akiwa na uungwaji mkono mkubwa kutoka serikali hiyo, na chama chake kwa upande wa Zanzibar; mtihani mkubwa uliopo mbele yake ni kuiunganisha Zanzibar na kuwafanya Wazanzibari kuwa kitu kimoja.
Upinzani haujaridhika namna uchaguzi ulivyokwenda, na wala haujakubaliana na matokeo ya uchaguzi wenyewe. Hivyo serikali ya umoja wa kitaifa ambayo huleta ahueni ya kisiasa, iko katika kitendawili cha ikiwa itakuwepo au la.
Inapokosekana serikali ya muundo huo huifanya Zanzibar kuzama katika migogoro na chuki za kisiasa. Chuki ambazo huzalisha matukio yasiyo ya kawaida, sanjari na kuwepo kwa jamii iliyogawika katika shughuli za kawaida na hata uhusiano wa mtu na mtu.
Taarifa za mauwaji na watu kupigwa katika kisiwa cha Pemba, zimeacha si madonda ya mwili pekee, pia madonda katika mioyo ya wale walioathirika na matukio au vitendo vya shari vilivyotokana na kinyang'anyiro cha uchaguzi.
Hizi ndizo zile nyakati ambazo watu hususia maduka, usafiri, shughuli za kijamii ikiwemo mazishi na harusi, kwa sababu wanaamini mchakato wa kuchagua haukutoa haki katika matokeo yake. Hali hiyo hujirudia mara kwa mara baada ya uchaguzi kumaliza.
Mshairi na mtunzi maarufu wa Riwaya aliyeishi karne ya 20 chini Uingereza, Eric Blair anasema, "katika siasa daima utawala ndio hukumbana na swali; katika mazingira haya na yale, utafanya nini? Lakini upinzani hauwajibiki kuchukua hatua wala kufanya maamuzi".
Kwa kuzingatia kauli hiyo na hali ilivyo Dkt. Mwinyi ana kazi ya ziada kuutatua huu mparaganyiko uliopo. Ana wajibu wa kujiuliza atafanya nini. Lengo liwe kutengeneza historia nzuri ya utawala wake pamoja na kuirudisha jamii ya Wazanzibari katika maisha ya kawaida.
Historia yake
Rais mteule Dkt. Hussein Mwinyi yuko katika shughuli za kisiasa tangu mwaka 2000. Ametumikia nafasi ya ubunge pande zote za Muungano, alikuwa Mbunge katika jimbo la Mkuranga, mkoa wa Pwani kabla ya kuwa Mbunge wa Kwahani, Unguja.
Huyu ni mtoto wa Rais mstaafu wa awamu ya pili ya serikali ya Jamhuri ya Mungaano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi. Katika siasa Dkt. Mwinyi amefuata nyayo za Baba yake kuhudumu pande zote mbili za Muungano.
Mwanasiasa huyo ataiongoza serikali akiwa na faida ya wawakilishi wengi wa chama chake katika Baraza. Kisiasa sura hiyo ya baraza itamsaidia pakubwa kupitisha mambo mbali mbali bila kuwepo upinzani wowote
Kwa wagombea wa Ubunge, Udiwani na Uwakilishi ambao hawajaridhika na matokeo ya uchaguzi, bado wanayo nafasi ya kwenda mahakamani. Ingawa kwa upande wa matokeo ya Urais hata Malaika hawana uwezo wa kuhoji ushindi huo, seuze mahakama.













