Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Donald Trump hakulipa ushuru katika miaka 10 ya kipindi cha miaka 15 iliyopita
Gazeti la New York Times limesema Donald Trump amelipa dola 750 (£587) tu kama ushuru mwaka 2016, mwaka aliogombea urais Marekani na mwaka wake wa kwanza akiwa Ikulu.
Gazeti hilo ambalo linasema lilipata rekodi ya ushuru wa Bwana Trump na kampuni zake kwa zaidi ya miongo miwili - pia limedai kwamba hakulipa ushuru kabisa katika kipindi cha miaka miaka 10 kati ya 15 iliyopita.
Rekodi hiyo imeng'amua hasara kubwa na miaka kadhaa ya kukwepa kulipa ushuru", limesema.
Hata hivyo Bwana Trump amesema kuwa "ripoti hiyo ni ya uwongo".
"Ukweli ni kwamba nililipa ushuru. Na utaona kwamba mapato yangu ya ushuru - yanachunguzwa, yamekuwa yakichunguzwa kwa muda mrefu," aliwaambia wanahabari baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo Jumapili.
"Huduma ya Mapato ya ndani [IRS] hainipendi inanichukulia vibaya sana. Kuna watu IRS - wananichukulia vibaya," amesema.
Bwana Trump amekuwa akikabiliana na changamoto kwa kukataa kuwashirikisha wengine kutazama nyaraka zake kuhusiana na utajiri na biashara zake.
Ni rais wa kwanza tangu mwaka miaka 1970 ambaye hakusema hadharani kuhusu malipo yake ya ushuru, ingawa hili sio lazima kisheria.
Gazeti la Times limesema kwamba taarifa ya ripoti yake "ilitolewa na chanzo ambacho kinafahamu sheria".
Ripoti hiyo inawadia siku kadhaa kabla ya mahojiano ya kwanza ya Bwana Trump na mpinzani wake wa chama cha Democratic Joe Biden na pia ni wiki kadhaa kabla ya uchaguzi utakaofanyika Novemba 3.
Madai ya msingi ni gani?
Gazeti la Times limesema kuwa lilipitia mapato ya kodi yenye kuhusishwa na Trump na kampuni za shirika la Trump kuanzia miaka ya 1990 pamoja na taarifa za malipo binafsi ya kodi ya mwaka 2016 na 2017.
Aidha, ripoti hiyo ilisema rais alilipa ushuru wa dola 750 tu kama malipo ya mwaka 2016 na 2017, na pia hakulipa ushuru wowote kwa kipindi cha miaka 10 kati ya 15 iliyopita, "kwa madai kwamba alipata hasara kubwa zaidi ya malipo aliyopata".
Kabla ya kuwa rais, Bwana Trump alikuwa anafahamika kama mfanyabiashara mashuhuri.
Lakini gazeti hilo limesema ripoti yake kwa huduma ya IRS iliashiria mfanyabiashara anayepata mamia ya mamilioni ya madola kwa mwaka ilihali ameitumia kuonesha anapata hasara kubwa na kutumia hilo kukwepa kulipa ushuru".
Katika ofisi ya umma ya uwasilishaji kosi, Rais Trump alionyesha kwamba alipokea angalau dola milioni 434.9 mwaka 2018.
Gazeti hilo halikubaliani na taarifa hiyo, na kudai kwamba malipo yake ya kodi yanaonesha rais Trump badala yake alikuwa amepata hasara ya dola milioni 47.4.
Shirika la Trump liliungana na rais kukanusha madai ya ripoti hiyo.
Ofisi ya mkuu wa sheria, Alan Garten, iliiambia gazeti la Times kuwa "taarifa nyingi, ikiwa sio zote, sio sahihi".
"Kwa kipindi cha mwongo mmoja uliopita, Rais Trump amelipa makumi ya mamilioni ya madola kama kodi binafsi kwa serikali, ikiwemo kulipa mamilioni kama kodi binafsi tangu alipotangaza kugombea urais mwaka 2015," amesema.
Je ripoti hiyo inasema kipi kingine?
Gazeti hilo linadai kwamba biashara nyingi kubwa kubwa za Trump - kama vile viwanja vya kuchezea gofu na mahoteli - "zinaripoti kupata hasara, kama sio makumi ya mamilioni ya madola mwaka mmoja baada mwingine ".
Pia inaongeza kwamba rais ana jukumu binafsi kwa zaidi ya dola milioni 300 za mkopo zinazotakiwa kulipwa katika kipindi cha miaka minne.
Aidha gazeti la Times linadai kwamba baadhi ya wafanyabiashara wa rais Trump wamepokea pesa kutoka kwa washawishi, maafisa wa kigeni na wengine wakitafuta mikutano ya ana kwa ana au kupata upendeleo fulani kutoka kwa rais.