Uchaguzi Marekani 2020: Republicans wasema wako tayari kuachia madaraka iwapo watashindwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiongozi wa Republican Mitch McConnell amesema kutakuwa na "mpangilio" wa kupokezana madaraka baada uchaguzi licha ya rais kuhoji uadilifu wa mchakato huo.
Seneta huyo wa Marekani wa ngazi ya juu amesema, bila kujali ni nani atakayeshinda uchaguzi wa urais Novemba 3, ataapishwa kwa amani Januari 20.
Tamko lake linakuja siku moja baada ya Rais Trump kukataa kutoa ahadi kwamba atakubali matokeo, akisema "wacha tuone litakalofanyika".
Ametilia shaka upigaji kura kupitia mfumo wa posta, lakini maafisa wa uchaguzi wanasema ni salama.
Rais Trump kwa sasa yuko nyuma ya mpinzani wake wa Democrat Joe Biden, katika kura ya maoni ya kitaifa siku 40 kabla.
Wamarekani wengi zaidi kuliko kawaida wanatarajiwa kupiga kura kupitia njia ya posta mwaka huu kutokana na hofu ya janga la corona, na Bw. Trump amekuwa akihoji usalama wa mfumo huo wa upigaji kura.
Kila mgombea wa Urais aliyeshindwa amekubali matokeo. Ikiwa Bw.Trump atakataa kukubali matokeo ya uchaguzi, hatua hiyo itaiweka nchi katika hali ya taharuki.
Bw. Biden amesema ikiwa hilo litafanyika, jeshi huenda likamuondoa Trump kutoka White House.
Republicans walisema nini?
"Mshindi wa uchaguzi wa November 3, ataapishwa rasmi Januari tarehe 20," Bw. McConnell aliandika kwenye Twitter yake siku ya Alhamisi.
"Kutakuwa na mpangilio wa kupokezana madaraka kama ambavyo imekuwa ikifanyika kila baada ya miaka minne tangu 1792."
Wabunge wengine wa Republican, akiwemo mshirika wa karibu wa Trump Senata Lindsey Graham, pia ameahidi uchaguzi utakuwa huru na wa amani.
"Nawahakikishia utakuwa wa amani," Bw. Graham aliambia kituo cha habari cha Fox, lakini akagusia kuwa uamuzi huo huenda ukatolewa katoka Mahakama ya Juu zaidi ya nchi "Ikiwa Republicans watashindwa kukubali matokeo. Mahakama ya juu zaidi ikitoa uamuzi utakao mpa ushindi Joe Biden, Nitakubali matokeo."
Senata Mitt Romney siku ya Jumatano, alisema "mapendekezo yoyote yanayoashiria rais huenda asiheshimu dhamana hii ya katiba hayaingii akilini na haiikubaliki".
Trump alisema nini?
Siku ya Jumanne, Bw. Trump kwa mara nyingine tena alitilia shaka uadilifu wa uchagaguzi akisema kuwa hana uhakika utakuwa wa " uaminifu" akidai kwamba upigaji kura kupitia njia ya posta ni "utapeli mkubwa".
Mapema siku hiyo, Waziri wa habari wa White House Kayleigh McEnany alisema Bw. Trump "atakubali matokeo ya uchaguzi huru na wa haki".
Rais Trump aliibua mjadala mkali siku ya Jumatano alipoulizwa na mwanahabari mmoja kama atajitolea kupokezana madaraka kwa amani '' akishinda, kushindwa ama kutoka sare'' na Bw. Biden.
"Nimekuwa nikilalamika kuhusu mfumo huo wa upigaji kura," Bw. Trump alisema. "Na kwamba upigaji kura wa aina hiyo ni majanga."
Mwanahabari huyo alipomkatiza na kumwambia " watu wanaandamana", Bw.Trump alimjibu: " Futilieni mbali uchaguzi, na kutatulia - mtakuwa na amani- hakutakuwa na kupokezana madaraka kwa kweli utakuwa ni muendelezo."
Mwaka 2016, Bw. Trump pia alikataa kujitolea kukubali matokeo ya uchaguzi katika kinyang'anyiro kati yake na mgombea wa Democratic , Hillary Clinton, hatua ambayo alitaja kama shambulio dhidi ya demokrasia ya Marekani.
Hatimaye alitangazwa kuwa mshindi, licha ya kuwa hakupata kura za wengi ambazo pia bado anatilia shaka.
Democrats wamesema nini?
Spika wa Democratic bungeni Nancy Pelosi, ambaye ni mwanasiasa wa tatu mwenye ushawishi mkubwa zaidi Washington, amewaambia wanahabari siku ya Alhamisi kwamba hakushangazwa na tamko la awali la Trump.
Bi Pelosi aliongeza kuwa rais " anapenda watu wanaojitakia makuu kupitia jukumu lao serekalini", akitoa mfano wa Vladimir Putin wa Urusi, Kim Jong-un wa Korea Kaskazini na Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki.
"Lakini namkumbusha: Wewe sio Korea Kaskazini, wewe sio Uturuki wala Urusi, Bw Trump.... Kwa nini usijaribu angalau kuheshimu kiapo cha ofisi yako."
Akizungumza na wanahabari Katika eneo la Delaware, Bw. Biden alisema kwamba matamshi ya Trump yalikuwa hayana mantiki

Bwana Biden mwenyewe amelaumiwa na wahafidhina kwa kuchochea vurugu katika uchaguzi aliposema mwezi Augosti: "Kuna mtu anaamini hakutakuwa na vurugu nchini Marekani ikiwa Donald Trump atachaguliwa?"
Mwezi uliopita, Clinton alimuomba Bw. Biden mara hii asikubali kushindwa "katika mazingira yoyote" katika mbio za mwisho usiku wa uchaguzi.
Alielezea hali ambapo Warepublican wangelijaribu "kuwatumia ujumbe wapigaji kura ambao hawajapiga kura" na kutumia kundi la mawakili kupinga matokeo ya uchaguzi.
Hofu juu ya uadilifu katika uchaguzi wa Novemba huenda ikawa ngome mpya ya makabiliano makali ya kisiasa sawia na suala la iwapo kuwa na jaji mpya wa mahakama ya juu zaidi kabla ama baada ya uchaguzi.












