Uchaguzi Tanzania 2020: ACT Kumuunga mkono Lissu kuna maana gani?

Tundu Lissu
Maelezo ya picha, Tundu Lissu
    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi

Katika mojawapo ya michapo ya kusisimua kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kuna mmoja maarufu kuhusu miaka ya mwanzoni ya Uhuru wa taifa hilo. Jenerali mmoja anadaiwa kwenda kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa jeshi jipya la Congo huru ambapo aliwaandikia ubaoni maneno yafuatayo; Jeshi kabla ya Uhuru = Jeshi baada ya Uhuru.

Ujumbe wake ulikuwa mmoja tu, kwamba hakuna kitakachobadilika kwa askari mara baada ya Uhuru wa nchi hiyo, mambo yatakuwa ni yaleyale.

Ujumbe huo wa Jenerali wa DRC unafanana kwa maana na hatua ya Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Shariff Hamad, kutangaza chama hicho kumuunga mkono kwenye kinyang'anyiro cha Urais, mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. ACT tayari kilikuwa na mgombea wake katika kinyang'anyiro hicho ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Tanzania, Benard Membe.

Maalim Seif Shariff Hamad alitangaza kumuunga mkono Tundu Lissu
Maelezo ya picha, Maalim Seif Shariff Hamad alitangaza kumuunga mkono Tundu Lissu

Ukweli ni kwamba kampeni za uchaguzi huu hazitamkosa Membe. Kuondoa siku mbili tatu za kwanza tangu chama chake kimpitishe kuwa mgombea urais, kampeni za kachero na mwanadiplomasia huyo mbobezi hazikuwa zimepata kiki ya kutosha. Kwa maana hiyo, nikiazima maneno ya Jenerali yule wa DRC, kampeni za urais wakati Membe akiwepo = kampeni bila ya Membe.

Namna Lissu alivyochukua nyota ya Membe

Hatua ya Membe kujiunga na ACT Wazalendo miezi miwili iliyopita ilizimua siasa za upinzani hapa nchini. Wakati huo, hakukuwa na uhakika endapo Lissu angerejea Tanzania na kuwania urais kama alivyokuwa ametangaza. Upinzani ulikuwa unalilia kuwa na mgombea wa kushindana na Rais John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kigogo huyo aliyefukuzwa kutoka katika chama chake alikuwa na sifa zote za kuwa kinara wa upinzani.

Watu wengi walidhani Lissu hatarejea kwa sababu za kiafya kutokana na shambulio dhidi yake lililofanywa Septemba mwaka 2017 au kwa sababu tu ya uoga wa kukamatwa kwa sababu yoyote ile. Rais huyo mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika na mbunge, alikuwa hajarejea nchini tangu mwaka 2017 na wapo walioamini kuwa kuna nafasi ndogo sana kwake kurejea nchini.

Watu wengi walidhani Lissu hatarejea kwa sababu za kiafya
Maelezo ya picha, Watu wengi walidhani Lissu hatarejea kwa sababu za kiafya

Kama Lissu asingerejea Tanzania, pasi na shaka yoyote, Membe angekuwa na nafasi zaidi hata kama Chadema ingeamua kumpitisha Lazaro Nyalandu aliyekuwa pia akitaka nafasi hiyo. Nyalandu na Membe wanafanana kwa sifa; ingawa Membe ana uzoefu na mtandao mpana zaidi, lakini tofauti yao kubwa kuelekea uchaguzi huu ilikuwa kwamba walau kachero huyo alikuwa akijulikana kama mkosoaji wa utawala wa sasa.

Maelezo ya sauti, ACT Wazalendo: CCM haitaondoka uongozini iwapo Tundu Lissu na Membe watagombea wakiwa mbal

Na hiyo ndiyo tofauti kubwa zaidi kati ya Lissu na Membe. Kwamba Lissu ni mkosoaji mkubwa zaidi wa utawala wa sasa na ipo dhana kwamba tukio lililomkuta lilisababishwa na tabia yake hiyo ya ukosoaji. Yeye alikuwa amelipia bei ya ukosoaji wake kwa damu na hiyo ni sifa ambayo hakuna mwanasiasa mwingine hapa nchini anayeweza kulinganishwa naye. Kama nyota ya Membe ilikuwa inawaka kabla Lissu hajarejea, nyota hiyo ilififia siku ile Lissu alipokanyaga nchini kutoka Ubelgiji alikokuwa akitibiwa.

Lissu pia alitumia vizuri fursa ya kufanya kampeni Zanzibar wiki mbili zilizopita. Katika Uwanja wa Kibandamaiti, Unguja, Lissu alitangaza kwamba chama chake kinamuunga kumuunga mkono mgombea urais wa visiwa hivyo katika uchaguzi huu, Maalim Seif.

Wagombeaji urais Tanzania

  • Anawania awamu ya pili na ya mwisho madarakani.
  • Kampeni yake imejikita kati mafanikio yake kwenye sekta za madini, ujenzi wa miundombinu, elimu bure na mapambano dhidi ya rushwa.
  • Awamu yake ya kwanza pia imekosolewa kwa ukandamizaji wa haki za binadamu.
  • Ni mgombea wa chama tawala ambacho kipo madarakani toka uhuru, hivyo anatarajiwa kushinda uchaguzi huu.
  • Magufuli, 60, alichaguliwa Bungeni mara ya kwanza 1995 na kupata umaarufu akihudumu katika wizara ya ujenzi alipopata jina la utani la tingatinga.
  • Alimiminiwa risasi na wasiojulikana Setemba 2017, japo amenusurika shambulio hilo limemuacha na majeraha ya kudumu.
  • Alirejea Tanzania mwezi Julai 2020 baada ya miaka mitatu ya ughaibuni ili kugombea urais kupitia chama kikuu cha upinzani Chadema.
  • Kampeni yake imejikita kwenye kuheshimu haki za binadamu na kukuza uchumi wa watu.
  • Mwanasheria na mtetezi wa haki za binadamu alichaguliwa kuwa mbunge mwaka 2010 na 2015 na kuhudumu kama mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani.
  • Alituhumiwa ndani ya CCM kuwa alikuwa na mipango ya ‘kumhujumu’ Magufuli kwenye uchaguzi wa ndani ya chama 2020.
  • Sasa ni mgombea wa ACT, ambacho kimeweza kukua kutoka kuwa chama kidogo mpaka moja ya mihimili ya upinzani kwa kipindi kifupi.
  • Kachero mstaafu, alihudumu kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya rais mstaafu Jakaya Kikwete toka 2007 mpaka 2015.
  • Mwanasiasa mwandamizi wa upinzani ambaye amegombea urais katika chaguzi zote kasoro mwaka 2015.
  • Alikuwa kinara wa upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 na 2005.
  • Ushawishi wake ndani ya upinzani umepungua baada ya migogoro ya ndani ya CUF iliyolazimisha kundi hasimu kwake kujitoa chamani.
  • Profesa Lipumba ni moja ya wasomi maarufu wa uchumi nchini Tanzania ambapo alisoma shahada zake za juu kutoka chuo kikuu maarufu cha Stanford, Marekani.

Kwa kufanya hivyo, Lissu aliua ndege wawili kwa jiwe moja; kwanza alionyesha kwamba chama chake kiko tayari kwa ushirikiano wa vyama ambao umekuwa ukililiwa na wafuasi wengi wa vyama vya upinzani hapa nchini lakini pia aliweka mpira mezani kwa ACT ili uchezwe - na kulikuwa na mambo mawili tu ya kufanya; ama kukataa ofa hiyo ya ushirikiano na kuonyesha ubinafsi au kuikubali kwa nao kuachia ngazi kwenye kinyang'anyiro cha urais wa Tanzania.

Katika mkutano wake kule Donge, Unguja, inaonekana Maalim Seif na ACT Wazalendo wameamua kuucheza mpira. Wameamua kuucheza kwa kumtoa sadaka Membe na kurasmisha uhusiano wa vyama hivyo kwenye kampeni za mwaka huu.

Ni moshi au moto?

Mara baada ya Maalim Seif kutangaza uamuzi wa kumuunga mkono Lissu katika mkutano wa hadhara na habari hizo kusambazwa kupitia mitandao ya kijamii, Membe alitoa taarifa kupitia mtandao wa twitter na kusema kwamba yeye ndiye mgombea wa ACT Wazalendo na jambo hilo halijabadilika.

Kauli hiyo ya Membe inaonesha mambo mawili, mosi kwamba hatua hiyo ilifikiwa pasipo kumtaarifu mapema au pengine alitaarifiwa lakini hakubaliani na hatua hiyo. Jibu lolote kati ya majibu hayo mawili, linaonesha kuna tatizo linalohitaji kutatuliwa.

Tangu taarifa hizo zitoke, nimejaribu kuwatafuta kuzungumza na viongozi waandamizi wa chama hicho na wasaidizi wa Membe na picha ambayo ninayo kwa sasa ni kwamba Membe hakuambiwa kuhusu uamuzi huo na inawezekana kabisa kwamba amelisikia kwa mara ya kwanza kupitia mitandaoni.

Inaaminiwa kuwa huenda Membe hakufahamishwa mapema juu ya suala la kumuunga mkono Lissu kama mgombea wa urais

Chanzo cha picha, BBC

Maelezo ya picha, Inaaminiwa kuwa huenda Membe hakufahamishwa mapema juu ya suala la kumuunga mkono Lissu kama mgombea wa urais

Kama huo ndiyo ukweli, maana yake ni kwamba chama hicho kimelifanya jambo hili vibaya hata kama lina faida kubwa katika upinzani. Membe ni mwanasiasa mbobezi ambaye uwepo wake katika upinzani unaongeza nguvu na uzoefu; mambo mawili yanayohitajika sana nyakati. Kitendo cha kumuengua katika kinyang'anyiro pasipo kumpa taarifa mapema kinamvunjia heshima na kumdogosha.

Ni mfano mwingine wa namna vyama vya upinzani nchini vinavyoshindwa kujifunza namna ya kuishi na viongozi wakubwa wanaotoka CCM kuhamia upinzani. Kwenye uchaguzi wa mwaka 2015; Chadema ilikuwa na mawaziri wakuu wastaafu wawili katika kampeni zake lakini wote wamerejea CCM na hawazungumzii vizuri uzoefu waliokutana nao walipokuwa katika chama hicho kikuu cha upinzani.

Katika hali ya kawaida, uamuzi wa mgombea kujiondoa katika kinyang'anyiro ulipaswa kutangazwa na mgombea mwenyewe kama ambavyo uamuzi wa kukubali matokeo ya uchaguzi unavyofanywa na mgombea kabla ya chama chake.

Ingawa ni vigumu kuona ikitokea, lakini napiga picha ya Membe kuendelea na kampeni zake za urais kana kwamba chama chake hakijasema chochote. Mwanasiasa huyu anatokea katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania ambako chama hicho kina ushawishi mkubwa na kama akiamua kufanya kampeni zake huko tu ambako ndiko anakotoka jambo lililo

Maelezo ya sauti, Msajili wa vyama Tanzania: Miungano ya vyama inapaswa kuwasilishwa kwa msajili wa vyama mi

Kwa vyovyote itakavyokuwa jina la Membe litakuwepo katika karatasi za kupigia kura kwenye uchaguzi huu na kwa vyovyote vile, ana ushawishi wa kiasi fulani kuhusu nini kitakwenda kutokea siku ya upigaji kura. Ni jambo la kufuatilia kujua ni kwa namna gani ACT na Chadema watalishughulikia jambo hili.

Siku chache zijazo, umma wa Watanzania utafahamu kama hatua hii ya sasa italeta moshi tu ndani ya ACT Wazalendo au moto kamili unaweza kuwaka.

Nafasi ya upinzani itakuwaje baada ya ACT kuiunga mkono Chadema?

Katika mahojiano yake na kipindi cha AMKA na BBC leo asubuhi, Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Nassor Mazrui, alisema kwamba kuna mazungumzo yanaendelea baina ya chama chake na Chadema kuhusu namna ya kushirikiana kuelekea Oktoba 28 mwaka huu, siku ambayo kura za kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani zitapigwa.

Hatua ya ACT kumuunga mkono Lissu inamaanisha kwamba Chadema itapata kura nyingi zaidi katika uchaguzi wa mwaka huu kuliko Wazalendo. Kura hizo nyingi zina maana ya kupata wabunge wengi wa Viti Maalumu na pengine ruzuku kubwa zaidi baada ya uchaguzi. Kwa sababu hakuna utafiti wa wazi uliofanyika hivi karibuni kuhusu nafasi za vyama kwenye uchaguzi huu, hakuna uhakika hasa ni kwa asilimia kiasi gani upinzani utashinda au kushindwa katika uchaguzi huu.

Namna pekee ya ACT Wazalendo , hasa kwa upande wa Tanzania Bara kufaidika na uamuzi wa kumuunga mkono Lissu ni kwa kufanya makubaliano na Chadema kwenye kugawana kanda na kuhakikisha Membe yuko nao pamoja katika hatua zinazofuata kuanzia sasa. Chadema na ACT vina wafuasi wa aina tofauti katika maeneo tofauti hapa nchini.

Njia mojawapo ya kufanya ni kwa Chadema kuiachia ACT kuwania ubunge na udiwani katika majimbo ya mikoa iliyo Kusini mwa Tanzania, Kanda ya Ziwa Magharibi na Pwani; huku wakiachiana majimbo ya Dar es Salaam kwa kutegemea nani ana nguvu katika eneo husika.

ACT, kwa upande wao, wanaweza kuwaunga mkono wagombea wa Chadema kwenye majimbo na kata zilizo katika maeneo ya Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kati. Kwa kufanya hivyo, Chadema na ACT Wazalendo watapunguza gharama za kampeni na kuweka nguvu katika maeneo ambayo wanaweza kushinda.

Pasipo makubaliano ya namna hii, ACT Wazalendo inaweza kumaliza uchaguzi huu ikiwa na matokeo yanayofanana au kukaribiana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambapo ilipata mbunge mmoja tu; Zitto Kabwe.

Jambo pekee la kufuta machozi ni kwamba inaweza kuongeza idadi ya wabunge na wawakilishi wake kutoka Zanzibar. Maana kubwa zaidi ni kwamba, mwaka 2025 italazimika tena kumuunga mkono mgombea wa Chadema kwa sababu ndiyo bado kitabaki kuwa chama kikuu cha upinzani hapa nchini; kwa mbali sana.