Uchaguzi Tanzania 2020: Safari ya ACT kutoka 'chama kichanga mpaka nguzo ya upinzani' katika miaka sita

Seif Sharif Hamad
Maelezo ya picha, Wanachama wakuu wa ACT Wazalendo Tanzania
    • Author, Markus Mpangala
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania

Majina mawili ya wanasiasa ndani ya chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, Bernard Kamilius Membe na Maalim Seif Sharrif Hamad yanatarajiwa kuidhinishwa na Kamati Kuu ya chama hicho kugombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar leo Agosti 5 mwaka huu wa 2020 ili kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 28 Oktoba.

Majina hayo yana mvuto na haiba kisiasa nchini Tanzania, hali ambayo inaweka chama hicho katika mjadala wa taswira ya sasa na ile ya baada ya uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na udiwani wa mwaka 2015 na kushuhudia kikiambulia nafasi moja ya kiti cha ubunge kutokana na ushindi wa Zitto Kabwe katika jimbo la Kigoma Mjini, pamoja na kupata madiwani na kuongoza Halmashauri ya Kigoma-Ujiji.

Hata hivyo kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu ACT Wazalendo kimeimarika kwa kiasi kikubwa na kuwa na wanasiasa wenye hadhi ya juu ambao wanaweza kutamba kwenye medani ya siasa na kuwashinda wapinzani wao badala ya kutegemea ushawishi na haiba ya mwanasiasa mmoja.

Mpaka mwaka 2014 ACT Wazalendo hakikuwa maarufu kisiasa nchini Tanzania. Taswira ya chama hicho ilibadilika mara baada ya kuwapata wanasiasa wawili wakubwa Zitto Kabwe na Profesa Kitila Mkumbo.

Upepo ukaanza kunukia uturi na kuwavutia baadhi ya wanasiasa wa ndani ya upinzani na chama tawala CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na udiwani wa mwaka 2015.

ACT imetoka kuwa chama kichanga kilichokosa wanasiasa wenye majina makubwa na ndani ya miaka sita ya uhai wake katika siasa kimefanikiwa kuvutia wanasasa, wafuasi na wanachama.

Licha ya changamoto za ndani na nje zikiwemo kutojulikana, utata wa itikadi na falsafa ya chama ikihusishwa na CCM, wigo wa wafuasi kuwa hafifu na uhaba wa rasilimali hivyo kuwahitaji baadhi ya vijana kufanya kazi kwa kujitolea, hivi leo chama hicho kimepiga hatua mbele.

ACT wana siri gani kupaa kisiasa?

bendera
Maelezo ya picha, Bendera ya chama cha ACT ikipepea

Uthabiti wa baadhi ya viongozi wake hasa Zitto Kabwe na Ado Shaibu ambao wamekuwa wakisimama kidete kukosoa serikali hasa pale ambapo vyama vingine vinaufyata.

Doroth Semu, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo amemwambia mwandishi wa makala haya, "tangu mwanzo hadi sasa na tuendako, tunaendelea kuamini na kuwa na nia ya dhati ya kuona mabadiliko ya kweli ya maendeleo kwa mwananchi wa Tanzania.

ACT Wazalendo imekuwa ikiishi ndoto yake hata katika hali ya chama kichanga. Imani katika utaifa kwanza na uzalendo unaona uwezo mkubwa na utajiri ndani ya Mtanzania.

Misimamo thabiti ya kile inachoamini., kusemea bila ubaguzi na kutoa suluhisho mbadala kwenye masuala yanayowagusa wananchi.

Sisi tuna uongozi imara, tuna imani ya kufanikiwa zaidi ya hapa tulipo kwa sababu hatuna uwoga wa kujaribu yale ambayo hayajazoeleka kwenye siasa kwa kufanya uamuzi wa kuzingatia tafiti na kuamini kwenye kukuza uongozi wa vijana na wanawake kuwapa fursa na kuwaendeleza pamoja na kujitofautisha na vyama vingine kimawazo na utendaji.

Maelezo ya video, Zitto Kabwe: Serikali inatafuta sababu za kukifuta chama cha ACT Wazalendo

Alipoulizwa nini tafsiri ya ujio wa Membe na Maalim Seif, alisema, " Membe na Seif wanatutambulisha wazi ACT Wazalendo ni chama makini.

Wameona nia ya dhati ya ACT kuwavusha Watanzania, sera, maono tangu kuasisiwa kwake kimejenga mwelekeo ambao umejionesha jinsi tulivyowapa nafasi ya kushiriki siasa bora zenye kujikita katika ufanisi,"

Ni 'majeruhi wa kisiasa' wenye maarifa

Zitto Kabwe, Ismail Jussa Ladhu, Nassoro Moyo, Maalim Seif, Bernard Membe wote wanaunganishwa na historia moja katika siasa; wameondoka kwenye vyama vya zamani sababu ya migogoro.

Membe

Chanzo cha picha, Membe/Twittter

Maelezo ya picha, Membe aliyejiunga na chama cha ACT-Wazalendo

Zitto Kabwe alifukuzwa uanachama wa Chadema, Bernard Membe alifutwa uanachama wa CCM, wakati Maalim Seif alifukuzwa CCM kisha akaamua kukihama Chama cha Wananchi (CUF) alichoasisi kutokana na mgogoro wa uongozi kati yake na Profesa Ibrahim Lipumba ambaye alirejea katika nafasi ya uenyekiti kwa kile kilichoitwa 'kinyume cha sheria' ya chama hicho.

Maalim Seif aliambatana na kundi lake; Nassoro Mazrui, Salim Bimani, Mbarala Maharagande, Joram Bashange, Ismail Jussa Ladhu, Mhonga Ruhwanya, Fatma Fereji, Eddy Riyami, Theopista Kumwenda, na Mwajabu Dhahabu.

Membe aliponzwa na nia ya kutaka kumpinga Rais Magufuli ndani ya CCM, huku Zitto Kabwe akiingia kwenye mgogoro sababu ya kuutaka uenyekiti wa Chadema dhidi ya Freeman Mbowe.

Maarifa yao katika siasa na uwezo mkubwa wa uongozi ndio msingi wa mafanikio waliyonayo ACT kwa sasa. Ni chama kinaochoongozwa na wenye kujua namna ya kuzichanga karata za kisiasa kwa mazingira ya Tanzania.

Maalim Seif
Maelezo ya picha, Maalim Seif

Nyota yang'ara Zanzibar

Chama hicho kwa sasa kimeongeza ushawishi katika siasa za Zanzibar na nyota yake hakika inang'ara. Wiki moja baada ya Maalim Seif kuhamia ACT Wazalendo vyombo vya habari viliripoti kuwa wanachama wa CUF jijini Tanga, kutoka Kata 27 na matawi 96 na baadhi ya wabunge wa zamani wamejiunga na chama hicho kipya.

Hekaheka zinazoendelea visiwani Zanzibar kwa sasa zimetoa dalili za wazi kuwa ACT-Wazalendo kinakwenda kushika hatamu katika siasa za upinzani Zanzibar.

Sehemu ya kwanza ni majimbo ya uchaguzi yaliyoko visiwani Pemba na duru za kisiasa zinabashiri kuwa kitazoa viti vingi vya Wawakilishi hasa visiwani Pemba.

ACT na demokrasia ya upinzani

ACT imekwepa mtego wa kubinya demokrasia ya ndani baada ya kufanya uchaguzi mnamo Machi 14 mwaka huu na kuwaibua washindi halali kuliko vyama vingine.

Uchaguzi huo ulionesha taswira nzuri ya demokrasia ndani ya chama hicho baada ya kinyang'anyiro cha nafasi mbalimbali kuwahusisha vigogo kuanzia nafasi za juu ya uongozi. Mojawapo wa nafasi ambayo ilitengeneza taswira yao ni kinyang'anyiro cha nafasi ya Kiongozi wa Chama iliyowahusisha Ismail Jussa Ladhu dhidi ya Zitto Kabwe.

Upande wake Maalim Seif Hamad aliwania nafasi ya Mwenyekiti wa Chama akichuana na Jeremiah Maganja.

Hali ni tofauti kwenye chama kikuu cha upinzani cha Chadema ambacho kimekuwa kikiingia kwenye migogoro kila linapofika suala la uchaguzi wa ndani hususani nafasi ya mwenyekiti.

Uchaguzi uliopita wa ndani wa Chadema ulishuhudia mgogoro kati ya wanasiasa wawili Cecil Mwambe (aliyekuwa Mbunge wa Ndanda) na Frederick Sumaye (aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu na mwenyekiti wa chama hicho kanda ya Pwani), wote wamehamia CCM huku wakilalamikia ukosefu wa demokrasia ndani ya Chadema.

Vilevile vyama kama vile CHAUMA kwa muda mrefu kinaongozwa na Hashim Rungwe, UDP kinachoongozwa na John Momose Cheyo pamoja na TLP chini ya Augustine Mrema wakiwa kama wenyeviti wa kudumu.