Uchaguzi wa Tanzania 2020: Ushindani ulivyo katika kinyang’anyiro cha Ubunge

Tarehe 28 Oktoba, 2020 ni uchaguzi wa nafasi ya Urais, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani.
    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania

Siku zinajongea kabla ya mamilioni ya wapiga kura kushuka vituoni asubuhi ya tarehe 28 Oktoba, 2020. Kazi yao itakuwa ni kuwachagua wagombea wa vyama mbali mbali katika nafasi ya Urais, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani.

Ubunge ni moja ya nafasi itakayokuwa na ushindani mkubwa baada ya ile ya Urais. Vyama vitachuana kuvijaza viti vipatavyo 264 vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokea Bara na Zanzibar. Mchuano huu utakuwa mkali kwa sababu ndani ya miaka mitano Rais John Magufuli alikuja na sera juu ya uhuru wa kisiasa, sera ambazo wengine waliziona zinapendelea chama tawala dhidi ya vyama vya upinzani.

Hali ikoje majimbo ya Zanzibar?

Kwa upande wa Zanzibar, sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye wakaazi milioni moja laki tatu na ushei. Kuna jumla ya majimbo 50 ya Ubunge yalio wazi kwa ajili ya wagombea, kati ya hayo 18 yako Pemba na 32 yako kisiwani Unguja.

Dkt. Hussein Mwinyi, mgombea urais tiketi ya CCM visiwani Zanzibar

Katika chaguzi zilizopita, ukisema chama cha upinzani kwa Zanzibar, maana yake ni Chama cha Wananchi (CUF), ndicho kimekuwa chama kikuu cha upinzani kwa chaguzi zote tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa.

Na CCM kimebaki kuwa chama tawala kwa chaguzi zote. Ingawa uchaguzi wa mara hii unaashiria mambo yatabadilika; ima chama tawala kitabadilika au chama kuu cha upinzani kitakuwa chengine badala ya CUF.

Seif Sharif Hamad , mgombea wa urais Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo

Ngome kuu ya upinzani ipo katika kisiwa cha Pemba, na ngome ya chama tawala ipo kisiwani Unguja. Kule Pemba chama tawala huwa hakipati Mbunge yeyote katika chaguzi za majimbo. Yote huchukuliwa na upinzani. Kwakuwa mara hii nguvu ya upinzani inabadilika polepole na kuhamia chama cha ACT Wazalendo, kuna kusubiri kuona ikiwa upinzani utaendeleza rikodi yake ya kutoshindwa katika kisiwa hicho.

Licha ya CCM kushindwa Pemba, chama hicho hubaki kuwa na wabunge na wawakilishi wengi kwa sababu huyanyakua majimbo mengi ya Unguja, ambako kuna majimbo mengi kuliko Pemba. Aghlabu upinzani huambulia viti vichache Unguja, visivyotosha kuwafanya wabunge wake kuwa wengi kuliko wa CCM Zanzibar.

Ni yapi majimbo yenye ushindani?

Uchaguzi wa mara hii utashuhudia mchuano mkubwa katika baadhi ya majimbo kutokana na sifa za wagombea wenyewe. Baadhi ya wagombea ni wapya katika siasa lakini majina yao ni makubwa na wanaingia kupambana na wakongwe. Wegine ni wale waliohama vyama vya upinzani wanarudi tena kugombea Ubunge kwa tiketi ya CCM.

Jimbo la Kawe, litakuwa na mchuano mkali kati ya Halima Mdee wa Chadema akitetea kiti chake alichokalia kwa miaka kumi, dhidi ya Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josepahat Gwajima wa CCM. Gwajina hana uzoefu katika siasa lakini ni mtu maarufu kutokana na huduma zake za kiroho.

Gwajina hana uzoefu katika siasa lakini ni mtu maarufu kutokana na huduma zake za kiroho

Katika jimbo la Arusha Mjini pia kutakuwa na kinyang'anyiro kikubwa kati ya mwanasiasa machachari Godbless Lema wa Chadema dhidi ya aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo wa CCM. Lema ni Mbunge wa jimbo hilo kwa miaka kumi na Gambo amekuwa mtumishi wa serikali katika mkoa wa Arusha, na mara kadhaa wawili hao wametupiana maneno hadharani.

Katika jimbo la Mbeya Mjini aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson wa CCM atakuwa na kibarua kikubwa cha kupambana na mgombea wa Chadema Joseph Mbilinyi. Kihistoria Mbilinyi ndiye Mbunge aliyepata kura nyingi kuliko wabunge wote katika uchaguzi wa 2015. Amekikalia kiti hicho kwa vipindi viwili.

Kwa wale waliohama vyama vya upinzani na kujiunga na chama tawala, baadhi yao wamepewa nafasi ya kugombea tena Ubunge. Mmoja wao ni Mwita Waitara wa CCM. Aliwahi kuwa Mbunge wa Chadema jimbo la Ukonga mwaka 2015. Mwaka 2018 alihamia CCM. Atachuana na John Heche wa Chadema katika jimbo la Tarime Vijijini.

Frank Mwakajoka wa Chadema atatetea kiti chake katika jimbo la Tunduma dhidi ya David Silinde. Silinde aliwahi kuwa Mbunge wa Chadema katika jimbo la Momba. Mwaka huu alijiunga na CCM na hivyo atapambana na Mwakajoka kupitia chama hicho.

Jimbo la Kawe, litakuwa na mchuano mkali kati ya Halima Mdee wa Chadema akitetea kiti chake

Chanzo cha picha, FCEBOOK/MDEE

Kuganyika kwa upinzani ni ahueni kwa CCM?

Vyama vya upinzani vilijizolea Wabunge wengi zaidi katika uchaguzi wa 2015 kulinganisha na ule wa 2010. Mavuno hayo yalikuja baada ya kwenda katika uchaguzi chini ya mwamvuli wa Ukawa ama kwa kirefu Umoja wa Katiba ya Wananchi.

Dalili zinaonesha umoja huu hautokuwepo katika uchaguzi huu. Yumkini kila chama kitapambana kivyake katika ngazi ya Ubunge. Ingawa hilo halitoifanya CCM kushusha pumzi. Nguvu ya Chadema bado ni kubwa Tanzania Bara. Mgombea wake wa Urais Tundu Lissu amethibitisha kupitia mikutano yake ya kampeni kwamba chama hicho bado kiko hai kisiasa na kwa wafuasi. Kwa upande mwengine nguvu ya ACT Wazalendo inakuja kwa kasi kila uchao huko visiwani.

Zanzibar ndiko ambako chama kikuu cha upinzani cha CUF kimeporomoka kiushawishi. Sio tena ile CUF iliyokuwa ikivuma Unguja na Pemba na kuitetemesha CCM. Anguko hilo limekuja baada ya mgogoro wa ndani uliokikumba chama hicho na kupelekea kugawika mapande na hatimae viongozi wake wa ngazi ya juu kuachana.

Nimemuuliza Dk. Muhidin Shangwe, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ikiwa kupoteza nguvu kwa CUF Zanzibar na kuibuka chama kichanga cha ACT Wazalendo kama mbadala wa upinzani visiwani, kutatoa ahueni kwa CCM katika uchaguzi huu?

Profesa Ibrahimu Lipumba,Mwenyekiti wa chama cha siasa cha CUF Tanzania

"Hilo halitoleta ahueni yoyote kwa CCM. Wapinzani wa CCM Zanzibar wanataka chama tawala kiondoke madarakani kwa sababu ya ajenda kuu mbili. Moja, kuna kundi fulani katika jamii ya Zanzibar linajiona kubaguliwa na kuonewa chini ya CCM, kwa sababu za kihistoria tangu Mapinduzi na Uhuru".

Dk. Shangwe anaifafanua ajenda ya pili kwa kusema, "shauku ya kuifanya Zanzibar kuwa huru na kujiamulia mambo yake kama ilivyokuwa kabla ya Muungano. Hivyo chama chochote hata ukikipa jina la jiwe kama kitasimamia ajenda hizo kitapata uungwaji mkono mkubwa dhidi ya CCM".

Ni rahisi kusema ACT Wazalendo kimefanikiwa kuzisimamia ajenda hizo chini ya mgombea wake wa Urais Maalim Seif Sharif Hamad. Ndio maana picha kubwa ya uchaguzi huu, inaonesha mpambano mkali haupo katika Urais tu, hadi Ubunge.