Waislamu nchini Sri Lanka wamelaumu kushinikizwa kuwachoma moto waliopoteza maisha kutokana na virusi vya corona

Jamii ya Waislamu nchini Sri Lanka imesema kuwa mamlaka inatumia janga la virusi vya corona kuwatenga kwa kuwalazimisha kuchoma wapendwa wao waliokufa hatua ambayo hairuhusiwi katika dini ya Kiislamu.

Mei 4, Fathima Rinoza, mwanamke mwenye umri wa miaka 44 wa watoto watatu kutoka jamii ya Wasilamu waliowachache wa Sri Lanka alilazwa hospitalini baada ya kushukiwa kuambukizwa virusi vya corona.

Mamlaka ilituchukuliwa kama mbwa

Fathima, ambaye alikuwa akiishi katika mji wa mkuu wa Colombo nchini Sri Lanka amekuwa na matatizo ya kupumua na mamlaka ilihofia kwamba ameambukizwa ugonjwa wa Covid-19.

Siku aliyolazwa hospitali, mume wake, Mohamed Shafeek, anasema mamlaka ilimtenga mkewe na familia yake.

"Polisi, jeshi pamoja na maafisa walikuja nyumbani kwetu hadi mlangoni," anasema. "Tulirushwa nje na wakanyunyiza dawa kila sehemu. Sote tuliogopa lakini hawakutuambia chochote. Hata mtoto wa miezi mitatu alipimwa ikiwa ana virusi na walituchukulia kama mbwa hadi katika eneo la karantini."

Familia hiyo ilizuiliwa kwa usiku mmoja lakini ikatolewa siku iliyofuata na wakatakiwa kujifungia kwa wiki mbili.

Wakati huo walikuwa wamepokea taarifa kwamba Fathima amekufa hospitalini.

Tulilazimishwa kusaini makaratasi

Kijana mkubwa wa Fathima alitakiwa kwenda hospitali kutambua mwili wa mama yake. Akaambiwa kwamba hawezi kuruhusiwa kurejea kwenye familia kwasababu kifo cha mama yake kimehusishwa na ugonjwa wa Covid-19.

Na badala yake anasema alilazimishwa kusaini makaratasi ili kuruhusu mwili wa mama yake kuchomwa moto hata indawa chini ya sheria za Kiislamu, kuchoma moto mwili wa mwanadamu kama ukiukaji wa dini hiyo.

"Aliambiwa kwamba sehemu za mwili wake zilihitajika kuondolewa ili kufanyiwa vipimo zaidi. Sehemu za mwili wanazohitaji ni za nini ikiwa alikufa kwa ugonjwa wa virusi vya corona? Anasema baba yake Shafeek, ambaye anahisi kuwa familia hiyo haikuarifiwa kikamilifu kile kilichotokea.

Familia ya Fathima imeungana na wengine wa jamii ya Sri lanka kukosoa serikali kwa kutumia janga la corona kuwatenganisha na kuwaganywa.

Muongozo wa WHO

Wanasema kuwa mamlaka inawalazimisha kuchoma moto waathiriwa ingawa chini ya mwongozo wa WHO, waathiriwa wa virusi vya corona wanazikwa.

Aprili 2019, Waislamu waliohusishwa na makundi ya eneo walilenga mahoteli na makanisa katika mji wa Colombo na mashariki mwa nchi hiyo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 250 ikiwemo raia wa kigeni.

Shambulio hilo ambapo kundi la Islamic State lilidai kuhusika, lilishtua taifa hilo. Waislamu wengi wanahisi kwamba tangu mashambulio ya kujitoa muhanga wamebadilika.

Hatari ya kuzika watu kwa njia ya kawaida

Tangu kifo cha Muislamu wa kwanza kufa kwa virusi vya corona Machi 31, mitandao wa kijamii imekuwa ikilaumu jamii ya Kiislamu kwa usambaaji wa virusi vya vya corona, hata ingawa ni vifo 11 pekee ambavyo vimerekodiwa rasmi nchini humo.

Miili yote 11, pamoja na ya wale wa dini ya Kiislamu imechomwa.

Dkt. Sugath Samaraweera, mtaalamu mkuu wa serikali wa magonjwa ya kuambukiza, anasema sera ya serikali inahitaji wote wanaokufa kwa ugonjwa wa Covid-19 kuchomwa moto pamoja na wale wanaoshukiwa kufa kwa ugonjwa huo, kwasababu kuzikwa kwa njia ya kawaida kunaweza kuathiri mfumo wa maji.

Dkt. Samaraweera anasema wataalamu katia wizara ya afya walianza kutekeleza sera hiyo kwa manufaa ya jamii.

Lakini wanaharakati wa Kiislamu, viongozi wa jamii na wanasayansi wameomba serikali ya Sri Lanka kufikiria tena umauzi huo.

'Nchi pekee'

Sri Lanka ndio nchi pekee miongoni mwa 182 ambapo waathirika wa dini ya Kiislamu wanaokufa kwa ugonjwa wa Covid-19 wanachomwa mto, kulingana na ombi la kupinga sera hiyo mahakamani lililowasilishwa na Ali Zahir Moulana, aliyekuwa waziri na mgombea katika uchaguzi mkuu ujao.

Moulana aliiambia BBC Sinhala, jamii ya Kiislamu itakubali uamuzi wa serikali ikiwa kuna ushahidi wowote au hatua ya kisayansi inayothibitisha kwamba mazishi ya kawaida ni hatari kwa afya ya jamii.

Maoni yake yanaungwa mkono na kiongozi mkuu wa Kiislamu Sri Lanka ambaye anasema ni wazi kuwa hakuna ushahidi wowote wa kisayansi au misingi ya kiafya unaopendekeza miili ya waliokufa kwa corona kuchomwa moto, na uamuzi wa serikali unazingatia ajenda yake potovu ili kuendelea kugawanya zaidi nchi hiyo kwa misingi ya kikabila.

Sheria tofauti

Siku hiyo hiyo ambayo Fathima alikufa, Abdul Hameed Mohamed Rafaideen, 64, alikufa katika nyumba ya dada yake huko mjini Colombo.

Baba huyo wa watoto wanne ambaye alikuwa anafanyakazi alikufa kwa matatizo ya kupumua.

Kijana wake mdogo, Naushad Rafaideen, ameiambia BBC kwamba jirani yake kutoka jamii ya waliowengi ya Sinhala, pia nae alikufa siku hiyo hiyo.

Kwasababu ya hatua za kusitishwa kwa usafiri wa eneo moja hadi jingine, maafisa polisi wa eneo waliitaka familia yake kupeleka mwili wa jirani yake, pamoja na wa baba yake hadi hospitalini.

Wakiwa kweye chumba cha kuhifadhi maiti, daktari alimwambia Naushad haruhusiwi kushika mwili wa baba yake kwasababu ya hatari ya ugonjwa wa Covid-19, hata ingawa haikuwa wazi kama virusi vya corona ndio chanzo cha kifo chake.

Hofu ya kukosolewa

Naushad, ambaye hawezi kusoma alitakiwa kusaini makaratasi ambayo yaliruhusu serikali kuchoma mwili wa baba yake.

Naushad anasema hakujua kile ambacho kingemtokea ikiwa angekosa kusaini makaratasi hayo, lakini aliogopa kukosolewa na familia yake pamoja na jamii ikiwapo angekataa kufanya hivyo. Lakini jirani yake alichukuliwa tofauti.

"Mtu mwigine ambaye mwili wake pia ulipelekwa hospitalini familia yake iliruhusiwa kumzika kwa njia ya kawaida huku ikipata fursa ya kumuaga mpendwa wao, anasema, na kuelezea vile mwili huo ulipelekwa makaburini ambapo jamii yake iliruhusiwa kumuaga kwa mara ya mwisho.

Naushad pekee na jamaa wake kidogo tu ndio walioruhusiwa kuhudhuria pale baba yake alipochomwa moto.

Wakati huohuo, karibia wiki sita baada ya kifo cha mke wake, Shafeek bado anapitia wakati mgumu kukabiliana na kile kilichotokea.

Wataalamu wa matibabu wanaopima watu virusi wanasema kuwa Fathima hakupatikana na virusi vya corona kama ilivyosemekana na hospitali, na kufanya familia yake kuchanganyikiwa zaidi.

"Sisi Waislamu huwa hatucho mtu anapokufa," anasema Shafeek. "Kama walijua kwamba hana corona, kwanini walimchoma?"