Evariste Ndayishimiye: Aapishwa kuwa rais mpya wa Burundi na kuvionya vyama vya upinzani

Burundi imemuapisha rais mpya wa taifa hilo , Evariste Ndayishimiye, katika hafla iliofanyika mbele ya raia wa taifa hilo na baadhi ya viongozi kutoka mataifa tofauti.

Akizunguma baada ya kula kiapo hicho , rais Evariste amesema kwamba atapatia kipaumbele haki za kibinadamu.

''Mataifa ya kigeni hayafai kunikumbusha kuhusu hilo kwa kuwa ndio suala nitakalolipa kipaumbele''. alisema rais huyo mpya.

Amevionya vyama vya upinzani kwamba havitapata nafasi nchi humo , akihoji 'ni kwanini mtu apinge serikali'.

Evariste Ndayishimiye vilevile aliviomba vyombo vya habari na wanaharakati wa haki za kibinadamu kushirikiana na serikali kukabiliana na matatizo yanayokumba taifa hilo, la sivyo vitaonekana kufanyiakazi watu wengine na sio raia wa Burundi.

''Kila mtu anafaa kuwa huru kuzungumzia kuhusu mawazo aliuonayo na changamoto zinazokumba taifa''.

''Hakuna mtu anapaswa kuamini kwamba mwanasiasa yeyote ana uwezo zaidi'', alisema.

Bwana Ndayishimie aliongezea kwamba Burundi inapenda majirani wema.

Kwa muda wa kipindi cha miaka mitano iliopita , mtangulizi wake Pierre Nkurunziza alikuwa amekosana na jirani yake wa kaskazini Paul Kagame wa Rwanda - uhusiano ulioathiri vibaya raia wa mataifa yote mawili.

''Tofauti iliopo kati ya mataifa haifai kutatuliwa kulingana na kiwango cha uwezo bali kupitia mazungumzo ya heshima kutoka pande zote'', alisema.

Kiongozi huyo aliwashutumu baadhi ya viongozi wa upinzani kwa kuwa vibaraka wa wakoloni.

Katika kiapo chake rais huyo ameapa kulinda katiba ya Burundi, kuheshimu umoja wa raia wa taifa hilo, kutoa haki kwa wote mbali na kutetea mipaka ya taifa hilo.

Kiapo hicho kinatokana na kifungu cha 107 cha katiba ya nchi hiyo

Sherehe hiyo iliofanyika katika uwanja wa kandanda wa Ingoma katika mkoa wa Gitega imefanyika wakati ambapo taifa hilo limeathirika na mlipuko wa virusi vya corona.

Rais Evariste baada ya kumaliza kula kiapo alikagua gwaride la kijeshi na baadaye kutoa hotuba .

Muda mchache kabla ya kula kiapo rais Evariste aliombewa na baadhi ya maaskofu ambao walimtaka kufungua milango ya uhusiano mwema na mataifa mengine.

Mbali na kwamba baadhi ya wageni hawakuvalia barakoa, raia wengi waliohudhuria hafla hiyo hawakuvaa kifaa hicho cha kuwalinda dhidi ya corona.

Hatahivyo shirika la msalaba mwekundu liliandaa maji na sabuni kwa raia wote waliokuwa wakiingia katika uwanja huo kuosha mikono yao.

Maelfu ya raia wa Burundi wamefurika katika uwanja huo wakisubiri kuapishwa kwa rais huyo kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wa taifa hilo Pierre Nkurunziza.

Makamu wa rais wa Tanzania bi Samia Suluhu na aliyekuwa rais wa taifa hilo jakaya Mrisho Kikwete wamehudhuria katika hafla hiyo ya kihistoria

Je rais Evariste Ndayishimiye ni nani?

Ni matokeo ambayo yalikuwa yanatarajiwa. Tume ya uchaguzi ilimtangaza Meja Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais .

Evariste ameachukua nafasi ya Rais Pierre Nkurunziza mbaye ameliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kwa miaka 15.

Watu wengi wamekuwa wakijiuliza Ndayishimiye ni nani? mwanasiasa huyo ni mtu wa karibu wa Nkurunziza na amekuwa Katibu Mkuu wa Chama tawala CNDD-FDD tangu mwaka 2016.

Alizaliwa mwaka wa 1968 katika mkoa wa Gitega, eneo la kati mwa taifa hilo.

Uhusiano wa Ndayishimiye na CNDD-FDD

Bwana Ndayishimiye ni miongoni mwa waliokuwa waasi wa CNDD-FDD waliojiunga na kundi hilo baada ya kunusurika katika mauaji ya kikabila ya wanafunzi Wahutu katika chuo kikuu cha Burundi mwaka 1995, kufuatia mauaji ya rais Melchior Ndadaye mnamo mwaka wa 1993.

Baadae kundi la CNDD-FDD lilibadilishwa na kuwa chama cha kisiasa ambacho kilianza kushiriki katika mazungmzo ya amani mjini Arusha Tanzania mwaka wa 2000 na kuafikiana kuhusu usitishwaji wa vita.

Wakati kundi la waasi la CNDD-FDD lilipojiunga na serikali mwaka wa 2003, Ndayishimiye tayari alikuwa amepandishwa cheo cha Meja Jenerali, na alihamishwa aende kuhudumu katika makao makuu ya jeshi la taifa.

Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES

Ndayishimiye aliteuliwa waziri wa usalama wa ndani na usalama wa umma nchini Burundi baada ya rais Nkurunziza kushinda uchaguzi mkuu wa 2005, na badaye kuhamishwa hadi ofisi ya rais mwaka 2007 ambapo alihudumu kama mshauri wa kijeshi.

Msimamo wa kadri

Wachanganuzi wa siasa za Burundi wanasema kwamba Jenerali Ndayishimiye ni mtu mwenye msimamo wa kadri asiyekimbilia mambo.

Wakati wa mzozo uliokumba Burundi mwaka wa 2015 kufuatia jaribio la mapinduzi, jenerali Ndayishimiye ni miongoni mwa viongozi wachache waandamizi jeshini ambao hawakutajwa katika orodha ya wale waliohusika katika uhalifu dhidi ya binadamu na mashirika ya kimataifa.

Kuna wale ambao pia wanasema Jenerali Ndayishimiye hatabiriki katika misimamo yake.

Mdadisi wa kisiasa na mwandishi wa vitabu nchini Burundi David Gakunzi anasema tabia ya kutotabirika huenda ikawashawishi wapinzani kumuunga mkono shingo upande.

"Kwa mfano, Ndayishimiye mwanzo alipinga uamuzi wa Rais Nkurunziza wa kutaka kugombea urais kwa muhula wa tatu mwaka wa 2015 ingawa badaye alibadilisha nia na kumuunga mkono" anasema Gakunzi.

Changamoto zinzomabili rais Evariste

Rais mpya wa Burundi Jenerali Evariste Ndayishimiye anachukua rasmi mamlaka ya urais nchini Burundi leo baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi urais mwezi huu. Lakini je ni changamoto zipi atakazokabiliana nazo kama kiongozi mpya?.

Jenerali Evariste Ndayishimiye anachukua nchi yenye mgawanyiko mkubwa kutoka kwa kiongozi wa zamani Pierre Nkurunziza ambaye alifariki mwezi huu. Nchi ya Burundi inakabiliwa na migawanyiko tofauti, ikiwemo ya ukabila baina ya Watuhu na Watutsi, mgawanyika wa kisiasa baina ya serikali na upinzani. Swali ni je Ndayishimiye atafanikiwa kuitatua migawanyiko hii ambayo ilishindwa kutatuliwa na mtangulizi wake aliyeiongoza Burundi kwa miaka 15?.

Kujumuisha wapinzani serikalini

Evariste Ndayishimiye alipata ushindi kupitia chama tawala cha CNDD-FDD kwa 68.72% ya kura.

Tume ya uchaguzi ilisema kuwa hasimu wake mkuu Agathon Rwasa wa chama (CNL), alipata 24.19% ya kura.

Bwana Rwasa aliwasilisha mashtaka mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo, lakini mahakama ya Burundi iliidhinisha ushindi wa Bwana Ndayishimiye

"Tutasahau kipindi kibaya kilichopita ambacho hakistahili kuwa jela yetu, Evariste Ndayishimiye salisema Ndayishimiye wakati wa kampeni za urais nje ya jiji kuu Bujumbura. Aliwahakikishia wafuasi wake kwamba atafanya kila awezavyo kutatua matatizo yanayosababisha mizozo inayolizonga taifa hilo dogo la Afrika Mshariki.

Jenerali Ndayishimiyeatakuwa na kibarua cha kuungana na Rwasa pamoja na wapinzani wengine kutoka vyama vya upinzani vipatavyo 40 kwa kwa ajili ya kuleta umoja na mshikamano wa Warundi wote bila kujali ukabila wala siasa kinyume na mtangulizi wake.

Mzozo wa wakimbizi

Ndayishimiye pia anarithi nchi yenye mzozo mkubwa wa wakimbizi uliosababishwa na vita na ghasia za mauji za muda mrefu nchini Burundi.

Ghasia za kisiasa na kiusalama pamoja na mzozo wa kiuchumi uliosababishwa na Burundi kuwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa zimewalazimisha zaidi ya 350,000 kukimbilia nchi jirani na wengine 110,000 ni wakimbizi wa ndani ya nchi.

Ndayishimiye hajahusishwa na unyanyasaji wa miaka ya hivi karibuni unaodaiwa kutekelezwa chama cha CNDD-FDD dhidi ya wale wanaoonekana kuwa ni wakasoaji wake. Hata hivyo hakuingilia kati kuzuwia ghasia zilizoikumba Burundi kufuatia uchaguzi wenye utata uliomuweka madarakani mwaka 2015 .

Wakimbizi wa Burundi watasubiri kuona iwapo Meja Ndayishimiye atatoa mazingira salama yatakayowawezesha kurejea na kuishi tena nchini mwao.

Atatakiwa kuwaridhisha majenerali ndani ya CNDD-FDD

Moja ya changamoto kubwa ya urais anayotarajiwa kukabiliana nayo kushughulikia maslahi ya watu binafsi ndani ya chama tawala cha CNDD-FDD. Ushindi wa Ndayishimiye wake umetokana na historia yake ya kijeshi katika CNDD-FDD.

Alishinda kwasababu alikua ni mgombea wa chama tawala kwa kupata uungaji mkono wa baadhi ya majenerari wenye usemi ndahi ya chama.

Ikizingatiwa kuwa hakuwa chaguo la mtangulizi wake Pierre Nkurunziza, kama rais ambaye chaguo lake lilikuwa ni Pascal Nyabenda- Spika wa bunge, itamlazimu Meja Ndayishimiye kuwarai wafuasi wa mtangulizi wake ambao walikua na chaguo la mtu mwingine kwa misingi ya kuepusha mpasuko ndani ya CNDD-FDD.

Atakabiliwa na changamoto ya kufahamu na kushughulikia maslahi na ushindani tofauti kwa ajilio ya mamlaka na pesa ndani ya chama.

Huenda ikawa vigumu kwa Ndayishimiye kutekeleza sera zake, hususan pale zitakapokuwa kinyume na maslahi ya Majenerali.

Mzozo wa Uchumi

Tangu mwaka 2015, Burundi imeshuhudia kuzorota kwa uchumi. Viwango vya umaskini vimepanda hadi kufikia 74%. Burundi kwa sasa ni nchi ya tatu maskini zaidi duniani.

Ndayishimiye atatakiwa kushughulikia viwango vya juu vya ukosefu wa ajira na umaskini mkubwa. Wahisani wengi wa kimataifa wamesitisha msaada wao wa Burundi baada ya uchaguzi wa 2015, jambo lililosababisha uhaba mkubwa wa fedha za kigeni.

Atatakiwa kurejesha uhusiana na mataifa ya Ulaya pamoja na Marekani ambayo yaliiwekea Burundi vikwazo kutokana na ukiukwaji wa haki za binadamu uliofuatia ghasia zilizoibuka wakati na baada ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2015.

'' Ninadhani atatakiwa kutuma ujumbe kwamba anataka kufanya mabadiliko ya kiutawala utawala bora nchini mwake, kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kuheshimu haki za binadamu ..ninamaanisha atatakiwa kuonyesha kuwa anataka kutoa fursa ya kisiasa, uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari. Nafahamu kuwa baada ya kifo cha Nkurunziza itakua ni vigumu kwake kuachana kabisa na mambo aliyoyafanya Nkurunziza mara moja...atatakiwa kufanya mabadiliko haya taratibu. Iwapo atafanya hivyo ninauhakika Muungano wa Ulaya utataka kufanya kazi na yeye naamini. Anasema Filip Reytjens, mtaalamu wa masuala ya maziwa makuu.

Kurejesha mahusiano na nchi jirani

Rais mpya Evaristre Ndayishimiye atatakiwa kurejesha uhusiano mwema na taifa jirani la Rwanda ulioharibika enzi ya mtangulizi wake Pierre Nkurunziza.

Nchi mbili zimekua zikishutumiana kila moja kuhatarisha usalama kwa kuwahifadhi wapinzani wan chi zao.

Licha ya kutegemeana kiuchumi na kuwa na historia zinazofanana, uhusiano wa nchi hizi mbili ni wa kihistoria kwani zilikua ni himaya moja kabla ya mkoloni.

Burundi inaishutumu Rwanda kwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi lililofeli mbali na kumuhifadhi mshukiwa mkuu wa mapinduzi hayo.

Baada ya kifo cha Bwana Nkurunziza Rais wa Rwanda Paul Kagame alituma rambirambi kwa Warundi uliokua ni ujumbe wake wa kwanza wa umma kwa nchi hiyo jirani tangu uhusiano wa Rwanda na Burundi ulipoingia dosari mwaka 2015.

Wataalamu wanasema viongozi kutoka nchi hizo mbili sasa wana fursa ya kuboresha mahusiano ya nchi zao na hivyo kuendeleza biashara na matembezi ya raia wan chi hizo ambao wameathirika na uhasama wa viongozi wao.