Wasp-76b: Sayari ya mbali ambapo 'mvua hunyesha ya vyuma'

Wataalamu wa anga za juu mnamo mwezi Machi waligundua sayari ilio mbali ambapo huenda kuna mvua ya vyuma.

Huku suala hilo likionekana kama miujiza ama filamu ya sayansi , ni hali asilia ya mojawapo ya malimwengu ambayo yamegundulika.

Kwa jina Wasp -76b , sayari hiyo ipo karibu na nyota yake kubwa ambayo nyuzi joto zake zinafika zaidi ya 2,400 - likiwa ni joto linaloweza kuyeyusha chuma.

Lakini nyakati za usiku kuna baridi ya hadi nyuzi 1000 sababu inayoweza kufanya vyuma hivyo kushikana na kuanza kunyesha.

Kulingana na Dkt David Ehrenreich wa chuo kikuu cha Geneva ni mazingira ya kushangaza.

''Fikiria kuangukiwa na manyunyu ya vyuma badala yale ya maji'' , aliambia BBC.

Mtafiti huyo na wenzake walichapisha matokeo yao katika eneo hilo lisilo la kawaida katika jarida la sayansi kuhusu asilia.

Katika chapisho hilo walielezea walivyotumia darubini kubwa iliopo Uhispania kwa jina ESPRESSO kutafiti sayari ya Wasp-76b kwa kina zaidi.

Upepo wenye kasi ya 18,000 km/h

Sayari hiyo iliopo miaka 640 kutoka ardhini ipo karibu mno na nyota yake na humaliza mzunguko mmoja kwa saa 43.

Suala jingine la kuvutia ni kwamba uso wake unaoonekana ukitazama nyota hiyo , tabia ambayo wanasayansi huita tidal coupling.

Mwezi pia huonyesha uso wake.

Hii inamaanisha kwamba uso wa sayari hiyo unaoonekana wakati wa mchana huchomeka sana.

Ukweli ni kwamba eneo hilo huwa moto sana hali ya kwamba mawingu yote hutawanyika na kutoroka huku molekyuli zote zilizopo mbele yake zikijigawanya kuwa chembe za atomu.

Tofauti ya nyuzi joto kati ya maeneo yenye mwangaza na yale yasio na mwangaza hutoa upepo mkali wenye kasi ya hadi kilomita 18,000 kwa saa kulingana na kundi la Dkt. Ehrenreick.

Kwa kutumia darubini kubwa ya ESPRESSO , wanasayansi waligundua alama ya chuma kilichoyeyuka katika sayari hiyo wakati ambapo mchana unatoa fursa kwa usiku kuingia.

Lakini wakati kundi hilo lilipogundua tukio hilo alfajiri alama hiyo ya chuma ilitoweka.

Tunachofikiria ni kwamba chuma hupoa wakati wa usiku katikati ya mawingu na kushuka kama matone ya mvua.

''Vyuma hivyo huanguka kwenye safu ya ndani ya anga ambayo mwanadamu hatuwezi kutafuta na zana zetu, "anasema Ehrenreich

'Sayari ya Jupiter ina joto kali'

Wasp-76b ni sayari kubwa ilio mara mbili kwa ukubwa ya sayari ya Jupiter. Jina lake lisilo la kawaida linatoka katika mfumo wa darubini ya Uingereza ambao uligundua ulimwengu huo mpya miaka minne iliopita.

Mwanasayansi Don Pollaco wa chuo kikuu cha Warwick , ambaye ni mojawapo wa washirika wa kundi waliogundua sayari hiyo , anahoji kwamba ni vigumu kufikiria kwamba kuna ulimwengu kama huo.