Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Jinsi msako wa watu waliokaribiana na wagonjwa unavyofanyika duniani
Mamilioni ya watu Uingereza hivi karibuni watahitajika kuanza kutumia programu za kwenye simu kufuatilia mienendo yao ili kupunguza usambaaji wa virusi vya corona.
Serikali imesema inaendeleza mipango ya kuajiri kundi la watu 18,000 kufuatilia wale walioambukizwa virusi vya corona.
Katibu wa kamati hiyo Robert Jenrick anasema kila mmoja atakuwa na jukumu la kufuatilia mienendo ya wengine kwa kupakua programu hiyo ya taifa itakayozinduliwa wiki chache zijazo.
Sasa je programu hiyo inafanyaje kazi, unahitajika kushiriki na kipi kinatokea kwa taarifa zako?
Kufuatilia walioathirika ni nini?
Hii ni njia inayotumiwa kupunguza maambukizi ya virusi vya corona. Huwa inatumika kwa kliniki za afya ya ngono, iwapo wagonjwa walioambukizwa wanahitajika kuwasiliana na yeyote yule ambaye aliwahi kufanya mapenzi naye.
Kwa janga la corona, kunamaanisha kufuatilia mtu yeyote ambaye amekuwa na mawasiliano na aliyeambukizwa na kumtaka ajitenge.
Mara nyingi hilo linafanyika kwa kupigia simu marafiki na familia za mgonjwa ambao watabainika kupitia programu hiyo inayoonesha mahali mtu alipo.
Tofauti na inavyotokea katika kliniki za afya ya ngono, inaweza kuwa vigumu kubaini ni nani ambaye umekuwa naye karibu sana kiasi cha uwezekano wa kumuambukiza virusi vya corona.
Na wanasayansi hawakubaliani moja kwa moja na suala la uliokuwa nao karibu.
Shirika la Afya Duniani linapendekeza kutokaribiana kwa umbali wa mita moja, huku serikali ya Uingereza ikipendekeza umbali wa mita mbili.
Ushauri wa kisayansi unasema kwamba sekunde mbili za umbali wa mita moja ni hatari kama ilivyo kukaa na mtu kwa dakika moja umbali wa mita mbili.
Umbali ambao utabainika na programu hiyo, hivyo basi utashindwa kugundua wengi walio kwenye hatari hiyo, kama vile muda uliotumika wakati wa kutangamana na ukaribu wa watu waliokuwa wanawasiliana na je walikuwa sehemu gani? ndani au nje, sehemu wanapopata kiwango kizuri cha oksijeni au la.
Hayo ni baadhi ya masuala ambayo yatazua mijadala baadae.
Kufuatilia wale waliowasiliana tayari kunatumika vilivyo na nchi kadhaa ikiwemo Hong Kong, Singapore na Ujerumani.
Uingereza inapanga kuanzisha programu yake ya kufuatilia waliowasiliana na mwathirika pamoja na timu itakayofanyakazi hiyo katikati ya Mei.
Kufuatilia waliowasiliana na mwathirika kutatekelezwa vipi Uingereza?
Timu ya watu 18,000 itajumuisha wafanyakazi wa umma na wahudumu wa afya 3,000, na wengine 15,000 kujibu simu zinazopigwa.
Mfumo huu wa simu utatumika kwa pamoja katika programu ambayo watu watahitajika kuipakua kwenye simu zao za smartphone.
Kwa kutumia Bluetooth, programu hiyo inafuatilia moja kwa moja pale watumiaji watakapotangamana.
Ikiwa mtumiaji ataanza kuonesha dalili za virusi vya corona, itakuwa jukumu lake kuruhusu programu hiyo kujulisha wahudumu wa afya.
Kujitambulisha kwake, huenda kukatuma tahadhari kwa watumiaji wengine ambao walikuwa na mawasiliano naye, na kuwataka watu hao kujiweka katika karantini au kwenda kupimwa.
Kwa wale wasio na simu za smartphone, huenda wakatumia mkanda maalum wa kuvaa kwenye mkono kama ilivyo kwa nchi kadhaa yenye kubaini wale wanaokiuka hatua ya kusalia ndani.
Je itasaidia kutamatisha hatua ya kusalia ndani?
Kufuailia waliowasiliana inasaidia katika kulegeza masharti kwa nchi kadhaa kunapojumuisha hatua nyengine.
Korea Kusini haikuwahi kuchukua hatua za kusalia ndani na hilo liliwezeshwa na hatua yao ya awali ya kufuatilia waliowasiliana, pamoja na upimaji wa halaiki.
Sio kwamba taifa hilo lilitaka raia kukumbuka mienendo yao tu lakini pia lilitumia kadi za kufanya manunuzi, CCTV na ufuatiliaji wa simu za mkononi kutambua mahali raia alipokuwepo.
Baada ya kubainika kwa karibia visa 900 kwa siku, sasa ikaanza kupima hao wanaobainika kwa siku.
Ikiwa mtindo huo utatumika, kufuatilia waliowasiliana kunaweza kusaidia katika ulegezaji wa masharti Uingereza, ingawa hakuna uhakika kwamba ufuatiliaji huo unaweza kufikia ilivyokuwa kwa Korea Kusini.
Serikali ya Uingereza ilijaribu kufuatilia watu waliowasiliana kabla njia hiyo haijahakikishwa kufanikiwa wakati wa mlipuko wa virusi vya corona, kabla hakujawa na watu wengi waliathirika.
Hata hivyo, kwasababu ya hatua ya kusalia ndani, hilo likiwa linamaanisha watu wamepunguza safari, itakuwa rahisi kufuatilia waliowasiliana.
Kufuatiliana kwa njia ya simu unaweza kuhitaji nguvu kazi nyingi na kuchukua muda mwingi: wafuatiliaji watu walioambukizwa huko Ireland wamesemekana kufanikiwa kupiga simu karibia 40 kwa mtu mmoja aliyeambukizwa.
Programu hiyo ya kwenye simu ni rahisi lakini kwa virusi hivyo kuangamizwa kabisa itategemeana na utumiaji. Wataalamu wanashauri karibia asilimia 80 ya watumiaji wa smartphone ikiwa ni asilimia 60 ya idadi yote ya watu, watahitajika kuitumia kwa kiasi kikubwa.
Ukilinganisha na karibia asilimia 67 ya watumiaji wa smartphone Uingereza ambao wamepakua programu ya WhatsApp kwenye simu zao.
Pia watu wanahitajika kuwa wazi na kuarifu wahudumu wa afya pale wanapoanza kuonesha dalili za virusi vya corona.
Serikali inaweza kufanya nini na taarifa zangu?
Sio kila mmoja anafurahishwa na hata hiyo ya serikali kuwa mtu wa kwando anapewa ruhusa ya kufuatilia taarifa zako. Makundi ya kutetea haki za kiraia yanasema serikali inastahili kuchukulia hatari iliyopo kwa umuhimu mkubwa na wale isifanye iwe lazima kwa mtu kupakua programu hiyo kama moja ya masharti ya yeye kuwa miongoni mwa waliolegezewa masharti na kuruhusiwa kurejea kazini.
''Mamilioni ya watu kama sisi wanahitaji kuamini programu hiyo, na kufuata ushari inayotoa, ,'' kulingana na wabunifu wa programu hiyo upande wa huduma ya afya. ,
Inasemekana taarifa inayokusanywa itatumika tu kwa sababu za kiafya na utafiti na pia inaweza kufutwa muda wowote mtu anapotaka kufanya hivyo.
Pia kampuni za mawasiliano kama Google zimesema kwa upande wao, programu hio itakuwa vigumu kuvamia na wavamizi wa kimtandao au mamlaka kuitumia kutambua watu binafsi.