Korea Kaskazini na Korea Kusini zafyatuliana risasi baada ya Kim Jong-un kuonekana hadharani

Picha ya DMZ

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Haijulikani ni nini haswa kilichosababisha vurumai hiyo

Milio ya risasi zilizofyatuliwa na Korea Kaskazini ililenga kituo cha mpakani cha Korea Kusini katika mji wa mpakani wa Cheorwon, kulingana na jeshi la Seoul. Hakuna majeraha walioripotiwa upande wa korea kusini.

Ikijibu, Korea Kusini ilifyatua raundi mbili za risasi na kutoa onyo kulingana na taarifa ya jeshi la taifa hilo. Haijulikani ni nini haswa kilichochochea ufyatulianaji huo.

Wakuu wa jeshi la Korea Kusini walisema kwamba walikuwa wakijaribu kuwasiliana na Korea Kaskazini kupitia nambari yao ya jeshi ili kubaini chanzo cha tukio hilo.

Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano kwamba jeshi la Korea Kaskzini limefyatulia risasi Korea Kusini.

Eneo hilo la mpakani lenye ulinzi wa hali ya juu liliundwa baada ya vita vya Korea mwaka 1953 ili kutawanya mataifa hayo mawili.

Katika kipindi cha miaka miwili, serikali ya Korea imejaribu kuleta amani katika eneo hilo la mpakani.

Kujaribu kuondoa hofu ya kijeshi mpakani ndio mojawapo ya makubaliano yaliofikiwa kati ya kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un na rais wa Korea Kusini Moon Jae-in katika mkutano uliofanyika Pyongyang mwezi Septemba 2018.

Ufyatulianaji huo wa risasi unajiri siku moja baada ya bada ya Kim Jong Un kuonekana hadharani, kufuatia kile kilichotajwa kuwa kutoonekana kwa takriban wiki tatu hatua iliozua uvumi kuhusu kifo chake.

Korea Kaskazini imefyatua risasi katika eneo la mpakani lenye ulinzi mkali ambalo linagawanya mataifa hayo mawili.