Waridi wa BBC: Miriam Mawira alizaliwa bila mikono, hutumia miguu yake kufanya kazi zake

Chanzo cha picha, Miriam Mawira
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
Miriam Mawira ni mwanamke wa miaka 33, mwenye ari ya kuishi maisha yake na amejitahidi sana kutimiza ndoto zake za tangu utotoni.
Japo alizaliwa bila mikono yote miwili, Maryam hutegemea miguu yake kufanya kile ambacho mikono yake ingepaswa kufanya .
Ni mama wa mtoto mmoja na pia yeye ni mfanyakazi katika kampuni mmoja ya mawasiliano nchini Kenya.
Miriam anajitokeza kama kielelezo chema miongoni mwa watu walio na ulemavu kwani kazi anazomudu kuzifanya hata wale ambao wana mikono huenda hawawezi.
Kwa mfano Miriam ni mama ya Mtoto mmoja wa kiume, na pale uhusiano wake na baba ya mtoto ulipokwisha basi Miriam amelivalia njuga jukumu la malezi ya mwanae.
Kwa hiyo mara nyingi yeye huhakikisha kuwa ameandaa chakula kwa kutumia miguu yake.
Pengine huenda unajiuliza je haya yanawezekana? Lakini Miriam anafanya majukumu mengi ya nyumbani kwa kutumia miguu yake
Miriam aliongezea kusema kuwa "Maisha bila mikono si rahisi lakini kila siku ninajipa nguvu ya kusonga mbele"

Chanzo cha picha, Miriam Mawira
Maisha yake ya mapenzi
Miriam alikutana na mpenzi wake miaka 5 iliyopita, na baada ya muda mapenzi yao yalinoga na wakachukua uamuzi wa kuanza kuishi pamoja kama Mume na Mke . baada ya muda alishika mimba na akajifungua mtoto wake wa kiume ambaye kwa sasa ana miaka 5.
Miriam anasema "Katika ule uhusiano wangu wa kwanza na baba ya mtoto wangu nilihisi kana kwamba alikuwa ananilea mimi na mtoto wangu "
Hali hii Miriam anaielezea kuwa alihisi kana kwamba alikuwa mzigo kwa mume wake na kwa hiyo uhusiano wao au mahaba yao ulianza kuwa na doa na ikawa ngumu kusuluhisha mivutano ya kila mara.
Japo miriam anasema kuwa ni kawaida kwa wanandoa kukosana lakini katika uhusiano wao walikosana pia kutokana na maumbile yake.
Miriam anasema kuwa wakati mwingi mumewe ilibidi ampakate mtoto wao wakati huo akiwa mchanga na aliona kana kwamba mashemeji zake hawakupendelea hilo.
"Sikutaka kuwa mzigo kwa mtu yeyote kwa hiyo nilionelea kuondoka kwenye uhusiano huo na kuendelea na maisha yangu bila mpenzi wangu "Miriam aliongeza.

Chanzo cha picha, Miriam Mawira
Na baada ya miaka miwili ya kuishi pamoja uhusiano wao ulikwisha.
Na je ana maoni gani kuhusu kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa mara nyingine?
Miriam alisema kuwa anaona kana kwamba ni vigumu kwake , kwani hata wakati huu ambapo yeye hana mchumba wala mpenzi kila mwanaume anayekutana naye huuliza maswali mengi kuhusu uwezo wa Miriam kuwa mke nyumbani na kuhimili majukumu ya nyumbani
"Wengi wananiuliza sasa wewe nikikuoa utapika vipi au utafanya kazi za nyumbani kivipi"? Miriam akaongezea
Japo kwake Miriam yeye hufanya kila aina ya kazi, kwa mfano kufua nguo zake , kupika , kula na pia kuandika , yeye anajionea fahari kuwa mama ambaye anatumia miguu yake kufanikisha kila jukumu
"Mimi ni mwanamke mshupavu, sina tabia ya kuketi tu na kutafuta watu kunihurumia,watu hunitazama kwa macho ya huruma na wengine kunikejeli lakini hilo halijakuwa kizuizi cha maisha yangu kuendelea"
Miriam alieleza kuwa alikuwa na uoga wa kushika mimba kwani alihisi kana kwamba hangekuwa na uwezo wa kujifungua kama wakina mama wengine, kwa hio alipoelezwa ana mimba alishtuka mno, anasema hatua ya kushika mimba na kujifungua ilimpa ujasiri wa kuwa yeye ni mwanamke mwenye nguvu

Chanzo cha picha, Miriam Mawira
Unyanyapaa katika mwa jamii
Miriam anakiri kuwa unyanyapaa katika jamii upo , tangu akiwa mtoto mdogo anasema kuwa wanafunzi wenzake walikuwa wanamuuliza kwanini yeye huacha mikono yake nyumbani , kwa hiyo walimtenga kwa kuwa alikuwa tofauti na wao.
Miriam anasema kuwa watu wazima nao walikuwa wanamtazama kama mtu wa kutisha , na hawakuwa wanaficha hisia za mshangao na hali ya kumuonea huruma kila alipopita, kwa hiyo ilikuwa jambo la kawaida watu kunong'onezana kila mara alipopita.
Miriam anamshukuru mama yake mzazi kwani alimfundisha kutumia miguu yake kufanya majukumu ya nyumbani.
Anasema kuwa kama mama mlezi wa mtoto bila usaidizi wa baba mtoto changamoto ni nyingi
"Wakati mwingine najikuta kwenye jangwa la kukosa mapenzi na uungwaji mkono katika malezi na nina hisi vibaya , lakini nimefaulu kusonga mbele kwani mwana wangu sasa ametimiza miaka mitano " anasema Miriam.

Chanzo cha picha, Miriam Mawira
Miriam anajivunia sana mwanae kwani anampenda jinsi alivyo, Miriam anakiri kuwa uwepo wa mwanae ni tosha kwake kuwa anaweza yote, Miriam anasema kuwa licha ya mwanae kufahamu kuwa hana mikono yeye humsaidia kila wakati na anamuona kama zawadi kutoka mbinguni
"Mwanangu anafahamu sina mikono kama kina mama wengine, lakini anajua mimi niko duniani kwa ajili yake, kwa hiyo anaponikumbatia mimi huhisi furaha isiyo na kifani "
Miriam anatoa ushauri kwa watu wanaoishi na ulemavu, kujikubali na pia kujiendeleza licha ya changamoto nyingi ambazo huandamana na watu wa hali hizi.












