Virusi vya corona: Wanyama wa mwituni wanavyokatiza mitaa ambayo watu wake wanajifungia ndani kuzuia kusambaa kwa Covid-19

Katika baadhi ya majiji ulimwenguni, mitaa yake ipo kimya kabisa na hakuna watu wanaopita na kufannya shughuli zao kama kawaida.

Wote hao wapo ndani wakipisha kasi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Wanyama wa mwituni wameingia katika baadhi ya mitaa hiyo. Baadhi yao wakisaka chakula huku wengine wakifurahia kutokuwepo kwa watu.

Paa hao wameingia mitaani kutafuta chakula kwasababu watalii waliokuwa wakiwalisha hawaendi tena katika makazi yao ya asili Mbuga ya Wanyama ya Nara.

India ndiyo nchi iliyotangaza marufuku kubwa zaidi ya watu kutotoka nje duniani: watu bilioni 1.3 wanatakiwa kukaa nyumbani kwa siku 21. Barabara hazina wapitao na hawa ng'ombe wakachukua nafasi hiyo kujivinjari jijini New Delhi.

Ngedere pia wameingia mitaani nchini India na kuzoa mabaki ya chakula wanayokutana nayo.

Farasi hawa wa mwituni taratibu waliingia katika mitaa ya mji wa Srinagar, kaskazini mwa India 'wakisherehekea' kutokuwepo kwa watu.

Nchini Israel, hususani katika jiji la Haifa, ngiri (nguruwe mwitu) wanajivinjari mitaani ambapo watu wanaokatiza ni wachache mno.

Wakaazi wa Uingereza ambao wapo ndani kutokana na janga la corona, hawawezi kufaidi kutembea mtaani kakama mbuzi hawa waliopigwa picha katika mji wa Llandudno.

Mji wa Llandudno upo katika pwani ya Wales, magharibi mwa nchi hiyo.

Katika jiji la Venice, bila ya uwepo wa watalii na meli kubwa za kifahari za wasfiri, maji yamekuwa safi zaidi na bata huyu anaonekana kufaidi kuogelea bila bughudha katika mitaa yake inayozungukwa na kuunganishwa na maji.

Puma (Simba wa milimani wa Amerika) huyu anayekadiriwa kuwa na mwaka mmoja, alionekana katika mitaa ya jiji la Santiago, mji mkuu wa Chile. Mamlaka nchini humo zinaamini simba huyo ametokea katika milima inayozunguka jiji hilo.