Coronavirus: Vidokezo vya kukabiliana na karantini kwa wale waliojitenga nyumbani

Chanzo cha picha, Getty Images
Je una wakati mgumu kukabiliana na amri ya kutotoka nje? Katika miaka ya hivi karibuni, maelfu ya watu Urusi ( zaidi ya 60,000 kati ya 2013 na 2018) walihukumiwa kifungo cha nyumbani kwa makosa ya kisiasa na mengineo.
Raia 6 wa Urusi ambao waliwahi kuwa chini ya kifungo cha nymbani walizungumza na mwanahabari wa Urusi kuhusu namna ya kuishi maisha ya kujitenga.
Muda wa kuanza kutafakari
Mwongozaji wa thamthilia Kirill Serebrennikov alihukumiwa kifungo cha nyumbani cha mwaka mmoja na nusu mjini Moscow. Ametengeza video: Namna ya kutoshikwa na kichaa unapokuwa huwezi kutoka nje.
Katika maisha ya kawaida kuna mambo mengi , simu unazopigiwa, Instagram na Facebook. Lakini kujitenga kunaweza kukukatizia haya yote.
"Ni fursa nzuri ya kujiondolea yote ambayo huenda yanakukera," anasema Kirill Serbrennikov. "Unaweza kujikita katika masuala ya msingi pekee - kama vile kujitambua wewe ni nani na kile unachotaka maishani."
Anapendekeza kuwa na kijitabu cha kuandika hata lile jambo dogo kabisa utakalofikiria.

Chanzo cha picha, Getty Images
Yulia Tsvetkova mtetezi wa masuala ya wanawake na mwelekezi wa filamu za watoto huko Siberia alikuwa chini ya kifungo cha nje kwa miezi minee sababu ni kutetea haki za wanawake na wapenzi wa jinsia moja mtandaoni.
Anasema kwamba hiyo ilikuwa ni fursa nzuri ya kutofanya chochote na wala hakuwahi kuhisi vibaya.
Tarajia kujihisi mnyonge
Sergei Fomin, aliyekuwa kizuizini kwa mwezi mmoja kabla ya kufunguliwa mashtaka na kuhukumiwa kifungo cha nyumbani mara tatu kwa kushiriki maandamano mjini Moscow, anakumbuka mipango aliyokuwa nayo baada ya kuachiliwa.
"Nilikuwa ninaenda kufanya mazoezi ya aina mbalimbali na kutengeneza ratiba yangu ya kusoma," anasema.
Lakini baada ya mwezi mmoja hilo halikuwezekana tena "Sikufanikiwa kufanya kile nilichokuwa nimepanga kila siku.
Ningeamka saa 4 asubuhi na kupumzika tu kitandani hadi saa tisa mchana, kisha ningetumia saa tatu bafuni na kurejea tena kitandani."
Yulia pia alikuwa na wakati mgumu. "Nilitamani kubadilika na kuwa kiwavi, na kujificha chini ya blanketi na kujitenga na dunia, hilo liliniogopesha," anasema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mtaalamu wa hesabu Dmitry Bogatov alihukumiwa kifungo cha nyumbani kwa zaidi ya miezi 6 mwaka 2018.
Anasema, "Ni vigumu sana kuendeleza ratiba yoyote kwasababu kawaida kuna mambo yanayotupa mwongozo kama muda wa maduka kufungwa na wa kuwa kazini. Lakini hayo yote yanakosa maana."
Natalya Sharina, aliyekuwa mkurugenzi wa maktaba ya fasihi Ukraine, alikamatwa 2015 na kupewa kifungo cha nyumbani kwa zaidi ya miezi 18.
Baada ya polisi kumvamia, kuhojiwa, kupewa kifungo cha peke yake, na kushtakiwa, akahukumiwa kifungo cha nyumbani lakini kwake hii ilikuwa kama kuwa peponi. Ingawa hilo halikuendelea kwa muda mrefu.
"Unafikiria kwamba unaweza kusoma na kusikiliza muziki, lakini ukweli ni kwamba hilo haliwezekani.
Ukosefu wa haki, hasa nikifikiria ukweli kwamba sikutenda kosa hilo. Lilinifanya kuwa na hasira sana. Unachukua kitabu ukidhani kwamba utasoma lakini huwezi kumakinika, unafungua televisheni na kila kitu kinaanza kukujia akilini."
Muda usiotarajia kwamba utakuwa huru
Baada ya kuwa chini ya kifungo cha nyumbani kwa miezi kadhaa, Natalya aliruhusiwa kwenda hospitali. Alihitaji matibabu ya uti wa mgongo baada ya kupata jeraha akiwa ndani ya gari la polisi.
Safari za kumuona daktari kidogo zilianza kumpa matumaini. "Nilienda hospitali lakini kuona wengine wakiendelea na maisha yao ya kawaida kulinifanya nihisi vizuri," anasema.
"Wakiniacha nitembee umbali wa mita 500," Yulia Tsvetkova anakumbuka, "Hilo lilikuwa linaibua hisia zangu. Ilikuwa ni kama kupata uhuru kidogo, lakini kwa muda uliosalia siku hiyo, nilikuwa mpweke sana."

Chanzo cha picha, Getty Images
Sergei alikatazwa kwenda kutembea lakini akavunja sheria mara mbili.
"Wakati mwengine saa za usiku, ningevuta kofia ya kwenye jaketi na kujifinika kichwani kisha ninatoka kwenda kununua pombe dukani. Nikitoka nilikuwa ninapata hisia zisizo za kawaida, ni kama vile nimetoroka jela."
Zungumza na uwapendao
Chini ya kifungo cha nyumbani, mara nyingi mahakama inaruhusu uongee tu na jamaa wako wa karibu. Mume wa Natalya na bintiye walimpa moyo katika kipindi chote alichokuwa amejitenga.
Baadaye, akaruhusiwa kuzungumza na simu na kutembelea marafiki. "Wanyama wa nyumba pia nao wanaweza kukufariji," anasema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mtaalamu wa teknolojia na mwanaharakati wa upinzani Alexander Litreyev alianzisha programu mtandaoni kwa jina De-anonymise kutambua maafisa wa polisi wanaopiga waandamanaji wasiokuwa na hatia.
Kifungo chake cha nyumbani ndo kimeanza. Rafiki yake Darya huja kumuangalia kila siku. "Huniletea vitu vitamu vya kula," anasema, "na kunipa moyo."
Soma vitabu kupunguza fikira
Karibu kila mmoja hutoa ushauri wa kusoma. Kirill Serebrennikov anapendekeza vitabu vya War and Peace, Don Quixote na The Kindly Ones.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pia anapendekeza kuandika mambo mengi tu unayofanya kama kumbukumbu au kujifundisha lugha mpya.
Alexander Litreyev ni mtunzi wa mashairi na anapanga vile atakavyoanzisha mradi wake mpya.
"Kile kilichoninusuru ni gemu ya draught," anasema Sergei. "Baba yangu alinunua kitabu kinachofunza namna ya kucheza na kushinda mchezo wa draught. Nilikuwa ninatumia muda wa saa tano kwa siku kutengeneza mchezo huo."

Chanzo cha picha, Getty Images
Kumbuka kuna baadhi ya watu ambao wanapitia changamoto kubwa kuliko wewe
Yulia anasema fikiria wafungwa wa kisiasa. "Najua vile mtu anavyohisi ikiwa yeye ni mfungwa wa milele. Karantini siyo kitu cha kuogopesha hivyo ukilinganisha na hicho."
Cha msingi zaidi wakati wa kujitenga, anasema Alexei Bushmakov, wakili wa Alexander, ni kufahamu kwamba hauko peke yako na kuwa haijalishi utachukua muda gani kila kitu kitakuwa sawa na utakuwa huru tena.
Pia unaweza kutazama:














