Coronavirus: Tanzania yathibitisha kifo cha kwanza cha mgonjwa wa corona

Serikali ya Tanzania imethibitisha kifo cha kwanza cha mgonjwa wa corona, kilichotokea alfajiri ya siku ya Jumanne tarehe 31 mwezi Machi mwaka 2020.

Mgonjwa huyo alifariki katika kituo cha matibabu ya wagonjwa wa COVID-19 kilichopo Mloganzila jijini Dar es Salaaam.

Marehemu ni mwanaume mtanzania mwenye miaka 49 ambaye pia alikuwa akisumbuliwa na maradhi mengine.

Hapo jana Waziri wa afya nchini humo Ummy Mwalimu alitangaza wagonjwa wapya watano wa virusi vya corona inayofikisha idadi ya wagonjwa nchini humo kufikia 19.

Kwa mujibu wa taarifa ya waziri Ummy, wagonjwa hao wapya watano wote ni raia wa Tanzania.

Wagonjwa wawili ni kutoka visiwani Zanzibar na watatu kutoka Dar es Salaam.

"Kazi ya kufuatilia watu wote wa karibu waliokutana na wagonjwa hawa inaendelea (contact tracing). Aidha tunawataka wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhai ili kujikinga na ugonjwa huu," ameeleza Bi Mwalimu.

Taarifa ya wizara ya Afya ilibainisha kuwa kati ya wagonjwa hao wawili (mwanamke mwenye miaka 21 na mwanaume mwenye miaka 49) walikuwa wakifuatilia hali zao na watatu (mwanaume mwenye miaka 49) "alikutana na raia wa kigeni kutoka miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi."

Taarifa zaidi kuhusu coronavirus:

Wagonjwa visiwani Zanzibar

Waziri wa Afya wa Zanzibar Hamad Rashid ametoa taarifa kuhusu mwendendo wa maraadhi ya corona visiwani humo.

Wizara imethibitisha kuwa na wagonjwa wawili, wa kwanza mwanamke raia wa Tanzania mwenye miaka 75 ambaye ameambukizwa kutoka nje ya Tanzania.

Mgonjwa wa pili ni mwanamke mwenye miaka 43 ambaye aliingia nchini Tanzania juma lililopita.

Awali, Waziri Ummy alisema kwa wagonjwa wa Zanzibar taarifa zao zitatolewa na waziri wa Afya wa visiwa hivyo Bw Hamad Rashid.