Coronavirus: Kenya yatangaza kifo cha kwanza cha mgonjwa mwenye virusi vya corona

Wasafiri wanaowasili Kenya kutoka China

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Wakenya watashuhudia kupungua kwa ushuru wa ziada utapunguzwa kutoka asilimia 16% hadi 14% kuanzia Aprili 2020.
    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili

Kenya imetangaza kifo cha kwanza cha mgonjwa aliyekuwa akiugua virusi vya corona.

Mwathiriwa huyo ambaye ni raia wa Kenya mwenye umri wa miaka 66 aliaga dunia siku ya Alhamisi nyakati za mchana katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Agha Khan jini nairobi ambako alikua amelazwa.

Raia huyo ambaye alikua akiugua ugonjwa wa kisukari alikuwa amewasili nchini tarehe 13 mwezi Machi kutoka Afrika Kusini kupitia Swaziland.

maelezo zaidi

Katika taarifa yake iliotiwa saini na waziri wa Afya Mutahi Kagwe, serikali ilisema kwamba ilipokea kwa huzuni habari za kifo cha Mkenya huyo ambaye alikuwa amekutwa na virusi hivyo baada ya kupimwa.

Siku ya Alhamisi, Kenya ilithibitisha visa vingine vitatu vya coronavirus na hivyobasi kuongeza idadi hiyo kufikia visa 31.

Katika mkutano na wanahabari afisa mkuu katika wizara ya afya Mercy Mwangangi alisema kwamba visa vyote vya hivi karibuni ni vya Wakenya waliokaribiana na watu walioripotiwa kuwa na ugonjwa huo hapo awali.

Hatua hiyo inajiri baada ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta siku ya Jumatano kutangaza kisa cha kwanza cha mtu aliyepona kabisa ugonjwa wa corona.

virusi vya corona

Akilihutubia taifa Uhuru Kenyatta alisema kwamba matokeo hayo mapya ni dhihirisho tosha kwamba ugonjwa huo unaweza kukabiliwa.

Rais pia alitangaza hatua kadhaa ambazo alisema zitasaidia serikali yake kukabili janga la corona ikiwa ni pamoja na amri ya kutotoka nje kuanzia Ijumaa Machi 27 kuanzia saa moja usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi.

Orodha kamili ya watu wanaotoa huduma muhimu ambao hawatathiriwa na amri hio pia ilitolewa siku ya Jumatano.

Katika hotuba yake rais alisema kwamba ushuru wa ziada utapunguzwa kutoka asilimia 16% hadi 14% kuanzia Aprili 2020.

Rais pia alitangaza hatua ya kupunguza mshahara wake na naibu wake kwa asilimia 80 huku mawaziri wake wakipunguza mshahara wao kwa asilimia 30.

Maelezo ya video, Coronavirus: Utajuaje kuwa umeathirika na virusi?

Ramani ya hali ya coronavirus duniani

Mtu aliyevaa barakoa

Chanzo cha picha, Getty Images

Mlipuko wa virusi vya corona unaosababisha ugonjwa wa Covid-19, ulitokea katika mkoa wa Hubei nchini China.

Tayari virusi hivyo vimesambaa katika mabara yote duniani isipokuwa Antarctica.

Kufikia sasa kinachojulikana ni kuwa Covid-19, ni ugonjwa ambao unaathiri mfumo wa kupumua wa binadamu.

Dalili zake ni pamoja na homa kali, kukohoa ambako baada ya wiki moja muathiriwa anakabiliwa na tatizo la kupumua.

Unaweza kufuatilia kwenye ramani ifuatayo kufahamu zaidi kuhusu hali ya maambukizi na vifo vilivyotokana na ugonjwa huo duniani