Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Je ni tiba zipi nne ambazo WHO inazifanyia utafiti kutibu virusi vya corona?
''Mpango mahsusi wa kuokoa maisha,'' hivi ndivyo Shirika la Afya Duniani WHO linavyoelezea juhudI zake mpya za kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona (Covid-19).
Kufikia tarehe 23 mwezi Machi, zaidi ya watu 350,000 walikuwa wameambukizwa virusi vya corona katika mataifa 170 duniani huku watu 16,000 wakiripotiwa kufariki.
Na idadi hiyo inaendelea kuongezeka kila uchao.
Bila tiba ama chanjo ambayo imeonekana kukabili virusi vya corona madaktari kwa sasa wanaweza kufanya kazi kupunguza makali ya dalili za ugonjwa huo.
Kwasababu hiyo , WHO imeanzisha mpango wa mshikamano 'solidarity' ambapo mataifa kumi yatafanyia uchunguzi jinsi dawa nne zinavyoweza kutibu Covid-19.
Lengo ni kukusanya data zaidi kwa wakati mfupi ili badala ya kuanza kutengeneza dawa mpya, mchakato unaoweza kuchukua miaka kadhaa, washiriki wa utafiti huo wataona iwapo dawa hizo zinazotumika kukabiliana na magonjwa mengine zitaweza kuzuia makali ya virusi vya corona.
Na ijapokuwa baadhi ya dawa hizi zinapatikana sokoni, madaktari wanasisitiza kwamba hazifai kutumiwa bila ya ushauri wa mtaalamu.
Nchi za Argentina, Bahrain, Canada, Ufaransa, Iran, Norway, Afrika Kusini, Uhispania, Uswizi na Thailand zimejiunga kufanya utafiti huo ambapo wanatarajia kwamba wagonjwa wengi watashiriki.
"Umuhimu wa utafiti kama huu ni kwamba unaweza kusajili wagonjwa kwa haraka," anaeleza Daktari George Rutherford ambaye ni Profesa wa takwimu za kibaiolojia katika Chuo Kikuu cha Carlifonia nchini Marekani.
"Iwapo kwa mfano nilikuwa nikifanyia majaribio haya katika maabara yangu, ningekuwa na wagonjwa wawili au watatu kwa siku, lakini kutokana na ushirikiano wa vituo kadhaa unaweza kuwa na wagonjwa 100 kwa siku,'' ameongezea.
Hiyo ni njia bora ya kuweza kufanya kazi kwa haraka.
Bi Ana Maria Henao Restrepo, mtafiti idara ya chanjo na kinga ya kibaiolojia kutoka WHO anasema kwamba mradi huo unafanywa kwa haraka zaidi.
Kulingana naye WHO inatarajia kuwa na nakala na data ya utafiti huo kuanzia wiki ya mwisho ya mwezi Machi.
Profesa Rutherford anasema kwamba iwapo hakuna matatizo ya kimpango, utafiti kama huo unaweza kutoa matokeo katika kipindi cha mwezi mmoja.
Sambamba na utafiti huo wa kimataifa , WHO imesema kwamba wanasayansi kutoka maeneo mbalimbali ya dunia wanafanyakazi ya kutengeneza takriban chanjo 20 za virusi vya corona.
Utafiti wa matumaini
Ili kuanzisha utafiti huo, jopo la watalaam wa WHO lilichagua tiba nne ambazo wanazithamini kuweza kukabiliana na virusi vya corona.
Waliangazia mbinu iliotumika kama vile habari kuzihusu na upatikanaji wake.
Tiba hizo zina dawa mchanganyiko ambazo zimetumika kutibu Ebola, Malaria au HIV.
Tiba hizo zitatumika bila mpangilio, ikitegemea upatikanaji wake katika kila hospitali kwa wagonjwa wa virusi vya corona.
Baada ya tiba kuanza, madatari watachunguza jinsi wagonjwa wanavyoendelea, ikiwemo siku watakazoondoka hospitalini ama iwapo atashindwa kupona.
Rutherford anasema kwamba katika tafiti kama hizi, lengo ni kuanzisha tiba katika awamu za kwanza za ugonjwa kabla ya mgonjwa kuingia katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Daktari huyo anaunga mkono mradi huo wa solidarity, lakini anaonya kwamba kufanya kazi na vituo tofauti katika mataifa kadhaa wakati mmoja inaweza kusababisha ugumu fulani.
Tiba nne
1.Remdesivir:
Licha ya kutengenezwa ili kutibu Ebola dawa ya remdesivir haikuonekana kuwa nzuri. Hata hivyo, inaonekana kuwa na uwezo dhidi ya virusi vya corona kulingana na vipimo vya seli zilizopandwa katika maabara.
Pia kuna ripoti zinazoonesha kwamba imekuwa na faida kubwa kwa wagonjwa wa Covid-19, lakini hiyo haitoshi kuthibitisha kuwa dawa hiyo ni nzuri.
''Kati ya dawa zilizojumuishwa katika mradi wa Solidarity, remdesivir inaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na virusi vya corona katika vipimo vya maabara," Stephen Morse, mkurugenzi wa mpango wa magonjwa ya kuambukiza katika Chuo Kikuu cha Columbia (EE) aliambia BBC.
2. Cloroquina/hidroxicloroquina
Chloroquine ilitumika kwa miaka mingi kutibu ugonjwa wa malaria hadi pale vimelea ambavyo husababisha ugonjwa huo vilipotengeneza usugu dhidi ya dawa hiyo.
"Iwapo inaweza kutibu, haimaanishi kuwa itafanya kazi dhidi ya Covid-19," anasema Rutherford.
Dawa hii inaweza kutumika kupitia kinywa lakini pia hutoa athari za maumivu kama yale ya kuumwa na kichwa, kuhisi kizunguzungu, kupoteza hamu ya kula, kuumwa na tumbo, kuhara, kutapika na kutokwa na upele katika ngozi, kulingana na Maktaba ya Kitaifa ya Tiba nchini Marekani.
Hatari yake ni kwamba ni rahisi kuipata na muonekano wake katika habari kuhusiana na virusi vya corona umesababisha kesi za sumu kuripotiwa.
3. Ritonavir na lopinavir
Mchanganyiko wa dawa hizi mbili umetumika kwa matibabu ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Wataalam waliozungumza na BBC wanakubali kwamba mchanganyiko huu haujaonyesha matokeo ya kutia moyo dhidi ya coronavirus.
"Lakini ni busara kujaribu tena," anasema Rutherford.
4. Ritonavir/lopinavir
Tiba ya nne kupimwa na Solidarity ni mchanganyiko wa ritonavir na lopinavir pamoja na interferon-beta, molekyuli ambayo husaidia kudhibiti uchochezi na imeonekana kuwa bora kwa wanyama walioambukizwa na ugonjwa wa kupumua wa Mashariki ya Kati (MERS).
Wataalamu wanaonya kuwa ni muhimu kuwa waangalifu wakati zinapotumika kwani; ikiwa zinatumika katika hatua za mwisho mwisho zinaweza kukosa ufanisi au hata kusababisha madhara zaidi kuliko faida kwa mgonjwa.
Sasa ni suala la wakati gani matokeo hayo yatapatikana kwa mradi huo wa mshikamano, lakini kulingana na Morse ni "hatua moja kubwa iliyopigwa" .