Coronavirus: Nchi za Afrika zilivyochukua hatua kudhibiti virusi

Chanzo cha picha, AFP
Mataifa kadhaa ya Afrika zimeweka mazuio ili kupambana na ueneaji wa virusi vya corona.
Afrika Kusini ilitangaza kuwa ni janga la kitaifa na kutangaza marufuku ya safari za kutoka nchi zilizoathiriwa na virusi, huku Kenya nayo ikiweka zuio kama hilo.
Hatua hizo ni jaribio la kuzuia mlipuko wa virusi katika bara hilo lenye mifumo duni ya kiafya.
Takribani chi 27 mpaka sasa zimeathirika na virusi.
Benin, Liberia, Somalia na Tanzania ni nchi zilizoripoti kuwa na wagonjwa wa kwanza wa virusi hivyo.
Morocco imefunga maeneeo ya kuoga yaitwayo hammam, migahawa ya vinywaji na vyakula, majumba ya sinema na misikiti baada ya kuripotiwa kuwa watu 28 wamepata maambukizi tangu mlipuko huo ulipojitokeza.
Kwa ujumla watu 350 wamegundulika kuwa na virusi barani Afrika. Watu saba wamepoteza maisha wengine 42 wamepona, Shirika la afya duniani (WHO) lilieleza.
Wengi wa wagonjwa hao walikuwa wametoka nchi za Ulaya na Amerika ya Kaskazini.
Kilichotokea Afrika Kusini
Afrika Kusini imeweka vizuizi vikali zaidi kwa raia wake tangu kumalizika kwa sheria ya utawala wa watu weupe- wachache baada ya kuripoti maambukizi ya watu 62.
Katika hotuba yake kwa taifa Jumapili, Rais Cyril Ramaphosa alitangaza janga la kitaifa.
"Hapo awali, ni watu ambao walikuwa wamesafiri kutoka nchi, haswa kutoka Italia, nchi ambayo ilikuwa imeathiriwa na virusi hivyo,'' alisema.
"Na sasa tunashughulika na maambukizi ya ndani ya nchi ," Bwana Ramaphosa alisema.

Hatua zilizochukuliwa
- Kufungwa kwa karibu mipaka 35 kati ya 72 nchini Afrika Kusini , sambamba na bandari mbili kati ya nane.
- Kuwazuia raia wa kigeni kutoka nchi nane ikiwemo Uingereza na Marekani kuingina Afrika Kusini tangu Jumatano.
- Imeshauri kuepuka safari zisizo za lazima nchini humo.
- Kufungwa kwa shule zote mpaka mwishoni mwa mapumziko ya sikukuu ya Pasaka.
- Kupigwa marufuku kwa mikusanyiko ya watu ya zaidi ya watu 100.

Chanzo cha picha, AFP
Nchini Kenya
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa watu wawili wamepatikana na virusi vya corona, watu hao wanaelezwa kuwa ni wale waliotangamana na mgonjwa wa kwanza, ambao kwa sasa wametengwa katika chumba maalum kilichopo katika hospitali kuu ya kitaifa ya Kenyatta, kwa mujibu wa rais Kenyatta.
Idadi hii inafanya idadi ya visa vya coronavirus nchini Kenya kufikia watu watatu. Hata hivyo amesema wagonjwa wako katika hali nzuri na hilo linawapa matumaini.
- Akizungumza na umma wa Wakenya moja kwa moja kupitia televisheni rais huyo amesema masomo katika shule zoe yamesimamishwa mara moja.
''Shule za msingi na sekondari zitafungwa kuanzia Jumatatu na za bweni zitafungwa ifikapo Jumatano'' , amesema rais Kenyatta.
- Vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu zitafungwa ifikapo Ijumaa na pale inapowezekana waajiriwa wanapaswa kuruhusiwa kufanya kazi majumbani kwao ili kuepukana na maambukizi ya coronavirus.
- Amesema watu wote wanaoingia Kenya raia au wageni watatakiwa kujitenga kwa muda wa siku 14 na yeyote atayekuwa na joto la juu la mwili ajipeleke kwenye kituo cha afya.
- Kulingana na tamko la rais huyo ni raia wa Kenya tu na wakazi wa kigeni wenye vibali halali halaliya kuishi nchini humo watakaokubaliwa kuingia nchini Kenya kwa muda wa siku 30 zijazo ili kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Nchini Tanzania
Serikali imetangaza kuwa na mgonjwa wa kwanza wa virusi vya corona ambaye aliingia nchini Tanzania kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro.
Serikali imetangaza mazuio kadhaa kwa nia ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona
Watanzania wasiokuwa na safari za lazima wanashauriwa kwa sasa kusitisha safari zao kwenye nchi zenye maambukizi
- Taasisi zote zikiwemo shule, hoteli, maduka ya biashara, nyumba za kulala wageni, makanisa, misikiti, ofisi za umma na binafsi, vituo vya kutolea huduma za afya, taasisi za fedha, vyombo vya usafiri pamoja na maeneo ya mikusanyiko ya watu kama vile masoko, viwanja vya michezo na vituo vya abiria kuweka vifaa vya kunawia mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni au maji yenye dawa kwa ajili ya kuhakikisha usafi wa mikono.
- Kuweka maji yenye dawa ya chroline katika mageti ya kuingia katika hifadhi zote kwa ajili ya kusafisha mikono ya watalii na waongoza wageni.
- Kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono
- Kukumbatiana , kubusu, kuepuka kushika pua, mdomo na macho.
- Hospitali zote nchini za serikali na zisizo za serikali kuweka zuio la idadi ya watu ambao wanakwenda kuwaona ndugu zao. Kwa maelekezo ya waziri ni kwamba wageni wa kumuona mgonjwa wasizidi wawili kwa siku kwa kila mgonjwa mmoja.
- Wananchi wametakiwa kutoa taarifa kwa vituo vya afya iwapo watamuona na mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Covid- 19.
Kinachoendelea katika nchi nyingine barani Afrika
Nchi nyingine za Afrika zimetangaza hatua za kudhibiti maambukizi ya virusi kama:
- Ethiopia - kufungwa kwa shule zote na kuzuia mikusanyiko ya umma na shughuli za michezo.
- Ghana - kuzuia mikusanyiko na safari kutoka nchi zenye rekodi ya visa vya zaidi ya 200 vya maambukizi ya virusi vya corona.
- Tunisia - kufungwa kwa mipaka yote na kupiga marufuku mikusanyiko ya ibada misikitini.
- Algeria - kupigwa marufuku kwa safari za kutoka na kwenda Ulaya.
- Msumbiji -kupigwa marufuku kwa mikusanyiko ya zaidi ya watu 300.
- Morocco and Djibouti - kupigwa marufuku kwa safari zote za ndege za kimataifa.














