Coronavirus: Kwanini idadi ndogo ya watoto ndio wanaopata virusi hivi?

Taarifa za kwamba mtoto aligunduliwa akiwa na virusi vya corona nchini Uchina Februari 5, saa 30 tu kabla ya kuzaliwa, zilisambaa kwa haraka kote ulimwenguni.

Hicho ndo kisa cha kwanza cha mtoto mchanga kupatikana na virusi hivyo ambavyo vimesababisha vifo vya watu 900 huku wengine 40,000 wakiambukizwa wengi wao wakiwa kutoka Uchina lakini visa vya virusi hivo vimeripotiwa katika nchi zaidi ya 30.

Hata hivyo, ni watoto kidogo walioambukizwa.

Utafiti wa hivi karibuni kuhusu ugonjwa huo uliochapishwa katika jarida la Journal of the American Medical Association na kuangazia wagonjwa katika hospitali ya Jinyintan huko Wuhan - mji ambao ni kitovu cha mlipuko huo.

Utafiti huo ulibaini kwamba zaidi ya nusu ya idadi ya watu walioambukizwa virusi hivyo ni watu wazima wenye umri wa miaka 40 hadi 59 asilimia 10 pekee ya wagonjwa wakiwa ni chini ya umri wa miaka 39.

"Visa vya watoto kuambukizwa virusi vya corona ni kidogo sana," watafiti hao wameandika. Lakini kwanini iwe hivi?

Ni watoto kidogo walioambukizwa virusi vya corona

Kuna nadharia nyingi, lakini wataalamu wa afya hawana jibu muafaka kwa nini visa vya watoto kuambukizwa virusi vya corona ni vichache mno.

"kwasababu ambazo haziko wazi, watoto wameonekana ama kutopata maambukizi au kuwa nayo lakini kwa kiwango kidogo tu," Ian Jones, profesa wa magonjwa ya maambukizi katika chuo kikuu cha Reading, ameiambia BBC.

Hili huenda likamaanisha kwamba watoto wanapata maambukizi kidogo tu na kutofikia kiwango cha kuanza kuonyesha dalili na hatimaye watoto hao hawapelekwi hopsitali kwa vipimo zaidi, kulazwa au hata kuripotiwa kwa visa zaidi. Nathalie MacDermott, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha London, anakubaliana na hilo.

"Watoto ambao umri wao ni zaidi ya miaka 5 na vijana wanaonekana kuwa na mfumo wa kinga wa mwili imara kukabiliana na virusi hivyo," anasema. "Henda bado wakaambukizwa lakini maambukizi yao yanakuwa hayana nguvu sana au hata pengine yasioneshe dalili za maambukizi."

Pia hii si mara ya kwanza hili linatokea, katika mlipuko wa virusi kama vile wa Sars, ambao pia ulianzia Uchina 2003 na kusababisha vifo kwa watu karibia 800 na pia wakati huo ilibainika kwamba maambukizi ya virusi hivyo kwa watoto yalikuwa ya china.

Mwaka 2007, wataalamu kutoka Vituo vya Kudhibiti Maradhi vya Marekani, vilibaini visa 135 vya watoto kuhusiana na virusi vya Sars lakini wakasema kwamba hakuna vifo vyovyote vilivyoripotiwa miongoni mwa watoto na vijana."

Je mwaka mpya wa Uchina kulisaidia kuepusha watoto kuambukizwa virusi vya corona?

McDermott pia anafikiria kwamba watoto huenda wasiwe katika hatari kuambukizwa virusi hivyo ikilinganishwa na watu wakubwa - mlipuko huo ulianza wakati wa maadhimisho ya mwaka mpya wa Uchina ambapo shule huwa zimefungwa.

Karibia majimbo yote ya Uchina yamefunga shule na zingine zitasalia kufungwa katika muda wote wa Februari.

"Watu wakubwa mara nyingi wanakuwa kama wauguzi na kuonekana zaidi kulinda watoto wao au hata kuwaondoa kabisa iwapo itabainika kwamba kuna mmoja ambaye ameambukizwa."

Kwa hiyo anafikiria kwamba hilo huenda likabadiliko kadiri virusi hivyo vinapoendelea kusambaa na kuongeza uwezekano wa jamii kuwa katika hatari ya kupata maambukizi".

Hata hivyo, hadi kufikia sasa kusambaa kwa haraka kwa ugonjwa huo hakujahushishwa sana na kuongezeka kwa visa vya watoto.

Kwa mara nyingine tena katika maambukizi ya virusi vya Sars watafiti waliochunguza visa vya watoto walibaini kwamba wale wenye umri wa chini ya miaka 12 wana uwezekano mdogo zaidi wa kuhitaji matibabu hospitalini.

Je virusi vya corona vina athiri zaidi watu wakubwa kuliko watoto?

Ingawa ni watoto kidogo tu waliothibitishwa kuambukizwa, wataalamu wa tiba hawajahitimisha kwamba hili ni kwasababu wao hawawezi kuambukizwi.

Maelezo ambayo yanaonekana kujitokeza kwa sasa ni kwamba mlipuko wa virusi vya corona unahusishwa na kuambukiza zaidi watu wazima ikilinganishwa na watoto kama vile ugonjwa wa tetemaji.

"Hili huenda lina ukweli zaidi kuliko ile dhana ya kwamba watoto wana mfumo wa kinga imara zaidi kukabiliana na virusi vya corona," Andrew Freeman, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukizwa katika chuo kikuu cha Cardiff, ameiambia BBC.

"Huenda ikawa mamlaka haiwafanyii vipimo watoto ambao hawaonyeshi dalili zaidi ya wale wanaonesha dalili kwa mbali," amesema.

Christl Donnelly, mtaalamu wa masuala ya takwimu za usambaaji wa magonjwa kutoka chuo kikuu cha Oxford na Imperial College London, anakubaliana na hilo na kutoa mfano wa mlipuko wa ugonjwa wa Sars huko Hong Kong.

Vipi kwa walio na maradhi tayari?

Watu wakubwa wenye maradhi tayari mfumo wao wa kinga una pambanana maradhi mfano, wenye

kisukari, ugonjwa wa moyo wanaonekana kuwa katika hatari zaidi ya kuambukizwa virusi kama hivi.

"Ugonjwa wa matatizo ya kupumua ambao hujitokeza mtu akishapata maambukizi ya virusi vya corona unaathiri sana watu wenye mfumo dhaifu wa kinga kwasababu tayari wako katika hali mbaya ya kiafya," Ian Jones ameelezea.

"Hilo linatokea kwa wanaopata mafua makali na matatizo mengine ya kupumua."

Ilibainika kwamba karibu nusu ya waathirika waliofanyiwa uchunguzi katika hospitali ya Jinyintan tayari walikuwa na maradhi mengine.

Lakini si watoto wanajulikana kwa kusambaza maambukizi ya virusi?

Watoto kawaida wanakuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya virusi na mara nyingi huchukuliwa kama wasambazaji wakubwa', kulingana na Ian Jones.

"Wao husambaza magonjwa ya mfumo wa kupumua kama vile ambavyo mtu yeyote mwenye mtoto katika shule ya chekechea anavyofahamu," anasema.

Kwa hiyo tunaweza kutarajia idadi kubwa ya watoto kuambukizwa - lakini hali ni tofauti kwa sasa.

Huenda ikawa watoto wana mfumo imara wa kinga kukabiliana na virusi, au makali ya virusi vyenyewe inakuwa kidogo kwa watoto ikilinganishwa na watu wakubwa, na hivyo basi watoto hawapelekwi kupata matibabu, hawafanyiwi vipimo wala kusajiliwa.

Utafiti zaidi unastahili kufanywa ili kupata uelewa wa mlipuko huu dhidi ya watoto.

Lakini pia huenda ikawa watoto wametegwa kabisa na kuwa katika uwezekano mdogo wa kupata maambukizi kwa kufunga shule, na kuwekwa katika mazingira mazuri.

Na hilo litafahamika watoto wote watakaporejea shuleni nchini uchina.