Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Gianna Bryant: Aliyekuwa na kipaji katika mchezo wa kikapu alikufa pamoja na babake
Kama binti ya Kobe Bryant - bingwa wa mpira wa kikapu mara 5 - Gianna Bryant alikuwa na kibarua kigumu cha kufanya ili kufikia ubora wa baba yake.
Kama baba yake, msichana huyo mwenye umri wa miaka 13 pia naye alikuwa mchezaji mzuri wa mpira wa kikapu. Kwa usaidizi wa baba yake kama kocha wake, Gianna alikuwa na matumaini kwamba siku moja angekuwa mchezaji wa kulipwa.
Bryant alikuwa na imani kubwa kwamba Gianna angefuata nyayo zake, na kila wakati alikuwa akizungumzia ndoto yake ya kutaka binti yake kuwa mrithi wake katika mchezo wa kikapu kwa wanawake.
Lakini kwa bahati mbaya, hakupata fursa ya kuona ndoto hiyo ikitimia.
Inasemekana kwamba Bryant na Gianna walikuwa wanaenda kushiriki mchezo wa mpira wa kikapu Jumapili wakati helikopta yao ilipoanguka katika mji wa Calabasas, magharibi mwa Los Angeles. Hakuna aliyenusurika kwenye ajali hiyo.
Wawili hao walitarajiwa kushiriki mashindano ya mchezo huo miongoni mwa vijana katika chuo cha michezo cha Mamba, Thousand Oaks, kulingana na vyombo vya habari vya Marekani.
Gianna alikuwa anashiriki kama mchezaji na Bryant kama kocha wake.
Kuhudhuria michezo hiyo pamoja ilikuwa jambo la kawaida na kufanya uhusiano wao kuwa wa karibu zaidi.
Binti wa pili kati ya binti zake wanne, Gianna alikuwa na ndoto ya kufuata nyayo za baba yake. Katika mahojiano, Bryant alisema binti yake amenuia kuchezea timu ya wanawake ya mchezo wa mpira wa kikapu ya Chuo Kikuu cha Connecticut.
Timu hiyo iliweka picha ya wawili hao kwenye mtandao wao wa Twitter.
Bryant alisema baada ya kustaafu 2016, alijiondoa kwenye mchezo huo lakini binti yake akarejesha tena shauku yake juu ya mpira wa kikapu.
"Siku mimi nilipoketi hapo, unajua kama mchezaji yeyote yule, na kama mtu anayehusika moja kwa moja. Ilikuwa kwa kwa ajili yake - alikuwa akifurahia," Bryant aliliambia shirika la BET katika mahojiano ya hivi karibuni.
Baada ya kustaafu, Bryant alitumia muda mwingi akiwa na familia yake - mke wake Vanessa, na binti zake wanne - Gianna, Natalia, Bianka na Capri.
Lakini inasemekana kwamba Gianna alikuwa na uhusiano wa kipekee na babake.
Upendo wa Bryant kwa binti yake, ambaye pia anfahamika kama Gigi, kunajitokeza wazi katika wasifu wake kwenye mitandao ya kijamii.
Video moja iliyokuwa katika mtandao wake wa Instagram inamuonesha akicheza na binti yake Gigi".
Nyota huyo aliyekuwa akiichezea timu ya Los Angeles Lakers, 41, amekuwa akifunza timu ya shule ya msingi ya Gianna tangu alipostaafu.
Video inayomuonesha Bryant akitoa ushauri kuhusu mchezo wa mpira wa kikapu ilisambaa katika mitandao ya kijamii wiki chache zilizopita.
Picha za Bryant akifunza timu ya mpira wa kikapu ya Gianna Jumamosi iliyopita katika chuo cha michezo cha Mamba - siku moja kabla ya ajali.
"Alikuwa na bango akiwa anachora wachezaji huku akizungumza na wachezaji," mtu mmoja aliyekuwa hapo ameliambia gazeti la New York Post.
Mkuu wa mchezo huo Adam Silver alisema Bryant alikuwa na mapenzi ya dhati ya kurithisha upendo wake juu ya mchezo huo kwa Gianna".
Bryant alikuwa na imani na uwezo wa binti yake. Mwaka uliopita, alimuarifu mwandishi wa gazeti la Los Angeles Times kwamba jina la familia yake lilikuwa salama mikononi mwa Gianna.
Akiwa anamuotesha Gianna, Bryant alimueleza binti yake kama "mtu wa kipekee".
Siyo tu kwamba Bryant alimuunga mkono binti yake, pia alichangia katika maendeleo ya mchezo huo kwa timu za wanawake.
Pia alivutia nadhari katika ligi ya wanawake ya mchezo wa kikapu tangu kuanzishwa kwake 1996, na kuongeza umaarufu wake.
kwa sasa, timu 12 zinashiriki ligi hiyo ambayo mashindano yake huanzia Mei hadi Septemba. Lakini kama ilivyo katika michezo mingine ya kulipwa, malipo ya wanawake ni ya chini mno ikilinganishwa na mishahara ya wenziwao wa kiume.
Katika siku za hivi karibuni, ligi ya wanawake ya mchezo wa kikapu ilishughulikia tatizo hilo na kukubali kuongeza mishahara kwa ushirikiano na chama kinachowakilisha wachezaji.