Ni kwanini Tanzania imesimamisha biashara katika Kambi ya wahamiaji ya Nduta?

wakimbizi
Maelezo ya picha, Eneo ambalo wakimbizi walikua wakifanya biashara

Mamlaka nchini Tanzania wamepiga marufuku kwa masuala yoyote ya kibiashara kufanyika ndani ya kambi ya Nduta, iliyopo kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, inayohudumia zaidi ya wahamiaji 73,000 kutoka Burundi.

Wafanyabiashara ambao ni wakimbizi wanasema kuwa walipewa muda mchache sana wa kujiandaa na kuvunjwa kwa maeneo yao, wanasema kuwa waliambiwa wafanye hivyo kutokana na zoezi la kuondoka kambini linaloendelea.

Masoko haya ni sehemu ya kuwapa kipato wakimbizi hawa na kuwasaidia kwenye matumizi madogo madogo.

Wakimbizi wanasema, kitendo hiki pamoja na kuvunjwa kwa soko lao kubwa mwishoni mwa wiki, ni sehemu ya kuwataka waondoke katika kambi hiyo.

''Hatujui tutaishi vipi. Tunaishi kwa kufanya biashara ndogo ndogo za kuuza na kununua, wanafanya hivi watushinikiza turudi nyumbani.'' Mkimbizi mmoja kutoka kambi hiyo aliiambia BBC, bila kutaka kujulikana.

Unaweza pia kusoma:

Tanzania iliachana na mpango wake wa kutaka kuwarudisha wakimbizi hao nchini kwao baada ya Umoja wa Mataifa kuonesha wasi wasi.

Baadhi ya wakimbizi wamerudi nchini kwao bila kulazimishwa huku wengine wakiwa na hofu juu ya usalama wao iwapo watarudi.

kambi
Maelezo ya picha, Vibanda hivi vilivunjwa mwishoni mwa juma na mamlaka nchini Tanzania

Dana Hughes, msemaji mkuu wa UNHCR, kwa upande Afrika mashariki ameiambia BBC hawana taarifa yoyote kuhusu kubomolewa kwa soko la wakimbizi la nduta, lakini hilo haliwezi kuwa suala jipya wala kushangaza.

kwa upande wa serikali ya Tanzania, waziri wa mambo ya ndani Kangi Lugola amesema kuwa hana taarifa ya tukio lakini atafatilia kwa kina.

''kwa kweli sina Taarifa ya suala hili , nitazungumza na Mkurugenzi wa kambi ili kujua nini kinaendela''

Wiki iliyopita , UNHCR ilitoa ilitoa taarifa ikilaumu serikali ya Tanzania kwa kuwalazimisha wakimbizi kurudi bila wenyewe kutaka.

vitu
Maelezo ya picha, baadhi ya vitu vilivyovunjwa

Tanzania kwa sasa inawangalia zaidi ya wakimbizi 200,000 kutoka Burundi wanaoishi katika kambi za Nyarugusu, Nduta na Mtendeli mkoani Kigoma.

Unaweza pia kusoma:

Wengi wao waliondoka nchini Burundi mwaka 2015 baada ya machafuko ya kisiasa baada ya Rais Pierre Nkurunziza kufanikiwa kubadilisha katiba ili kuruhusu mihula mitatu ya Urais.