Brigid Kosgei: Aliacha shule, mama wa watoto mapacha na aliyeweka rekodi kwenye riadha

Wanariadha mara nyingi wana kitu kinachowasukuma kufanikiwa, na kwa mbio za marathon za wanawake hata kuweka rekodi ni matokeo ya msukumo alioupata Brigid Kosgei alipokuwa akipitia kipindi kigumu utotoni.

''Nikifikiri kuhusu nilikoanzia na changamoto tulizopitia tulipokuwa tunakua, ninajiambia siwezi kurudi kwenye maisha yale yale na hicho kilinisukuma kufanya vizuri , ''mwanariadha huyu aliambia BBC.

Miaka minne tangu aliposhiriki kwa mara ya kwanza mbio za marathon, ambazo alishinda, Kosgei kwa sasa ni mwanamke mwenye mbio zaidi katika historia kwa umbali wa kilometa 42.2

Juma lililopita katika mji wa Chicago nchini Marekani, alivunja rekodi iliyowekwa na muingereza Paula Radicliffe aliyoiweka miaka 16 iliyopita.

Kukimbia kwenda shuleni

Alikuwa mmoja kati ya watoto saba waliolelewa na mama pekee katika kaunti ya Elgeyo -Marakwet, mji katika bonde la ufa ambao umewatoa wakimbiaji maarufu wa nchini Kenya.

Na kama ilivyo kwa wakimbiaji wengine wa Kenya kabla yake, Kosgei aligundua kuwa anaweza kukimbia akiwa shule ya msingi, ambapo alikuwa akikimbia kwenda darasani nyakati za asubuhi.

''Shule yangu ilikuwa umbali wa kilomita 10 kutoka nyumbani na wakati mwingine kuepuka kuchelewa nilikua nakimbia, nikiwa njiani nilikutana na wakimbiaji wakiwa mazoezini na kujisemea mwenyewe: 'ninaweza kuwa kama wao' alisema.

Alianza kushindana kwa umbali wa kati akiwa shuleni na ingawa hakuchaguliwa kuwakilisha nchi yake, kipaji chake hakikuwa na shaka.

Baada ya kuongezwa kwa karo ya shule ilikuwa changamoto kwa mama yake, Kosgei aliamua kukatisha masomo yake mwezi Januari mwaka 2012 katika mwaka wake wa mwisho.

''Nilipofika kidato cha tatu, malimbikizi ya madeni yalikua zaidi ya pauni 1,200. Mama yangu alijaribu kunishawishi niendelee na shule naye atakopa fedha kulipa deni nilimwambia: ''kwa muda gani utaendelea kukopa?''

Kupata watoto

Lakini sasa akiwa na miaka 17, aliutilia maanani mchezo wa kukimbia- kazi ambayo iliiwezesha familia kuwalipia karo ndugu zake wadogo.

Alianza kufanya mazoezi na rafiki yake wa kiume Mathew Kosgei, ambaye kwa sasa ni mumewe. Mwaka mmoja baadae alikua mapumzikoni baada ya kujifungua watoto mapacha.

Lakini uzazi haukumfanya akatishe nia yake. Mwaka 2015 alianza alipoishia, wakati huu aliingia kwenye kambi ya mafunzo si mbali na makazi yake, kambi iliyokuwa chini ya mwalimu wake.

Kambi hizo nchini Kenya zinatoa mazingira ambapo wakimbiaji wanapata nafasi ya kujikita zaidi na mafunzo bila kuingiliwa.

Msimu wake sasa umepita lakini amerekodiwa kuwa mkiambiaji wa kwanza mwanamke wa marathon kwa mwaka 2019. Mwaka ujao amedhamiria kushiriki michuano mikubwa zaidi ya Olimpiki.

Kwa sasa anaelekea kijijini kumtembelea mama yake, ambaye amemnunulia kiwanja na nyumba kutokana na faida aliyopata aliposhinda michuano kadhaa awali, pia atatumia muda huo akiwa na mumewe na watoto.