Mtoto Mila amebuniwa dawa yake mwenyewe na wanasayansi

Patient and doctor

Chanzo cha picha, Boston Children's Hospital

Mtoto wa kike mwenye ugonjwa hatari wa ubongo amepewa dawa ya kipekee ambayo ilibuniwa kwa ajili yake peke yake.

Mila Makovec, ambaye ana umri wa miaka nane amekuwa anasumbuliwa na ugonjwa hatari ambao hautibiki .

Chini ya mwaka mmoja , madaktari wa watoto katika hospitali ya Boston waliamua kutengeneza dawa inayoweza kutumika kwenye vina saba vya mtoto huyo peke yake kwa ajili ya kuokoa maisha yake.

Kwa sasa mtoto huyo ana endelea vizuri ingawa bado hajapona bado.

Ugonjwa huo wa nadra , ni upi?

Ugonjwa huu ni nadra sana kwa mtu kuupata na huwa unamfanya mtu kuwa na wasiwasi au mshtuko na mara nyingi hupelekea mtu kufa.

Ugonjwa anaosumbuiwa na mtoto huyo huwa unatokea kwa watu wachache sana katika umri wa kati ya miaka 5-10. Kuna aina nyingi za ugonjwa huu na mtu anaweza kupona mpaka anapofika miaka 20.

Ugonjwa huu hatari uhathiri ubongo na mfumo wa seli za neva na hata macho.

Mila alianza kuugua akiwa na miaka mitatu kipindi ambacho mguu wake wa kulia ulipoanza kupinda.

Mwaka mmoja baadae, alihitajika kusogeza kitabu kwa karibu kabisa na macho kwa sababu alianza kuwa na uhafifu wa kusoma na alianza kutembea kiajabu.

Alipofika miaka sita, Mila alikuwa kipofu na aliongea kwa tabu sana na alikuwa anashtuka sana.

Matibabu

Familia ya Mila walifahamu kuwa huo ni ugonjwa unaathiri maumbile hivyo wakaanza kampeni iitwayo - Mila's Miracle Foundation - kwa matumaini kuwa mtoto wao atapona.

"Nilikuwa katika mlo wa jioni, mimi na mke wangu akanionesha picha ambayo ilikuwa imewekwa na rafiki yake kwenye Facebook kuwa familia hiyo ilikuwa inatafuta msaada," Dkt. Timothy Yu aliiambia BBC.

Daktari huyo alikutana na Mila kwa mara ya kwanza mwezi Januari mwaka 2017.

Timu ya madaktari huko Boston walifanya uchunguzi wa vina saba vya Mila na kubaini sehemu ya kipekee katika mwili inayosababisha ugonjwa huo.

Baada ya kuona matokeo ya utafiti huo , wanasayansi waliona kuwa inawezekana kumtibu.

Presentational grey line
Presentational grey line

Hivyo wakaamua kubuni dawa ambayo waliijaribu kwa Milla na wanyama wa maabara na kuthibitishwa kwa ajili ya matumizi na mamlaka ya dawa na chakula nchini Marekani.

Mila alianza kutibiwa na dawa inayoitwa Milasen tarehe 31 Januari mwaka 2018.

Kwa kawaida dawa huwa inachukua muongo au nusu ya muongo kutoka maabara na kuanza kufanyiwa majaribio kwa wagonjwa.

Lakini timu ya wanasayansi hao wa Marekani wameweza kufanikiwa ndani ya mwaka mmoja tu.

"Tulipomaliza na kuangalia nyuma, tulishangazwa sana na kujivunia kazi tulioifanya. Mara nyingine ni vyema kuwa mwerevu zaidi kwa sababu maisha ya mtoto yalikuwa hatarini na tulikuwa tunafanya kazi kwa bidii ili kila mtu afanye kazi katika upande wake kwa haraka," Dkt Yu alisema.

"Hatuna uhakika kama kuna dawa aina hii iliwahi kubuniwa kabla", aliongeza Dkt Yu.

Drug

Chanzo cha picha, Boston Children's Hospital

Dawa hii itamsaidia vipi Mila?

Dawa hii haiwezi kutibu athari zote ambazo Mila amezipata.

"Kwa mwaka wa kwanza tulianza kuona maendeleo kidogo ," Dkt Yu aliiambia BBC.

Ugonjwa huu kupona kwake sio rahisi.

Presentational grey line

Familia yake iliripoti kuwa ameanza kupata nafuu kwa kusimama vizuri na kumeza chakula.

Kuna dalili kuwa katika mwaka wake wa pili wa matibabu kutakuwa na maendeleo makubwa zaidi kama Mila ataendelea kuangaliwa kwa ukaribu.

"Tunadhani kuwa tiba yake inaenda polepole na tuna matumaini kuwa inaweza kumpa nafuu," Dkt. Yu alisema.

Vilevile daktari anaamini kuwa kama ugonjwa kama huu utatokea kwa mtu mwingine, itakuwa rahisi kupatiwa tiba mapema na kuweza kuweka utofauti mkubwa.

Injection

Chanzo cha picha, Boston Children's Hospital

Gharama ya dawa hii?

Watafiti hawawezi kusema ni kiasi gani cha fedha wametumia kutengeneza dawa hiyo.

"Tusingeweza kuchukua hatua ya kuitengeneza kama tusingeona njia nzuri ya kuifanya dawa hii ipatikane kwa urahisi.Wazo la dola milioni kwa ajili ya mamilionea halipo kwa kile tunachokifanya", Dkt. Yu alisema.