Hofu wilayani Musanze nchini Rwanda baada ya shambulio la waasi

Kumekuwa na wasiwasi miongoni mwa wakaazi wa wilaya ya Musanze kaskazini mwa rwanda baada ya washambuliaji kuwaua watu 14 wiki iliyopita.
"Hali ni mbaya, tunaogopa sana wanaweza kurudi na kuwaua waliotoroka, hatulali tena", Isaac Niyonshuti, mfanyabiashara katika eneo la Kabazungu ameiambia BBC.
Washambuliaji hao - wanoashukiwa kuwa wafuasi wa Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR) walivishambulia vijiji katika na mbuga ya taifa ya Volcanoes National Park - ilio maarufu kwa sokwe wa milimani wanaopatikana huko.
Vikosi vya usalama nchini vinasema viliwaua waasi 19 na kuwakamata wafuasi watano katika operesheni iliofanyika mwishoni mwa juma.
Maafisa wanasema waasi hao walitekeleza shabulio hilo siku ya Ijumaa wakati wakitafuta chakula.
Jana jumapili katika mazishi ya baadhi ya wahanga, mkaazi mwingine wa Kabazungu amesema washambuliaji walikusanyika katika eneo hilo kabla ya kuanza kupora mali katika maduka ya biashara.

Amewaambia waombolezaji namna mumewe alivyouawa:
"Walirudi kwetu, wakaanza na mumewangu walimpiga kwa shoka dogo kichwani na pia watoto wangu wawili waliokuwa nyuma yake.
Nilipenya kati kati yao na nikakimbilia kichakani, Nilikaa usiku kucha huko na alfajiri nikarudi kuupata mwili wa mumewangu uwanjani kwenye ua.
Niliarifiwa kwamba watoto wangu wangalai hai lakini walijeruhiwa vibaya na walipelekwa hospitalini Kigali."
Maafisa wamewaambia wakaazi kwamba wasiwe na wasiwasi kwasababu jeshi limerudisha amani.
Baada ya shambulio hilo, Bosi inayohusika na utalii nchini - Rwanda Development Board, imesema vikosi vya usalama vimerudisha utulivu na huduma za kitalii zitaendelea kama kawaida katika mbuga hiyo ya kitaifa.
Kitu gani kilichofanyika wakati wa shambulio la Ijumaa?
Washambuliaji waliojihami waliidhisha mashambulio kwa kutumia visu, mapanga na mawe katika wilaya hiyo ya Musanze.
Wakati idadi ya waliouawa ikiwa imetajwa kuwa watu wanane awali, maafisa sasa wanasema watu 14 wameuawa.
Eneo hilo limelengwa na waasi wa Hutu nchini rwanda walioendesha shughuli zao katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika siku za nyuma.
waasi hao wanalijumuisha kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR) ambalo viongozi wake wanatuhumiwa kuhusika katika mauaji ya kimbari nchini mnamo 1994 ya watu wa kabila la Tutsi na Wahutu wenye misimamo ya kadri.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kumekuwa na muitikio gani?
Polisi nchini rwanda wanasema walifanikiwa kuwasaka na kuwakamata baadhi ya wahusika na shambulio hilo.
"Vikosi vya usalama vilifanikiwa kuwafuata magaidi , na kuwaua 19 kati yao na kuwakamata watano," Polisi wamesema katika taarifa rasmi.
Maafisa wa idara ya utalii wamesema wageni wote katika eneo hilo wapo salama.













