Sahar Tabar: Nyota wa Instagram wa Iran aliyekamatwa kwa 'kukufuru'

Chanzo cha picha, Instagram
Nyota wa Instagram raia wa Iran ambaye aliyeweka mtandaoni picha inayomuonesha jinsi alivyofanya juhudi kufanana mwigizaji filamu wa Marekani Angelina Jolie amekamatwa, ripoti zinasema.
Sahar Tabar alikamatwa kwa tuhuma za kukufuru na kuchochea ghasia, Shirika la habari la Tasnim liliripoti.
Tabar aligonga vichwa vya habari kimataifa baada ya picha zake kupata umaarufu katika mitandao ya kijamii.
Japo ilidaiwa kufanya upasuaji wa kiurembo mara 50, baadhi ya picha hizo zilikua zimefanyiwa ukarabati.
Sahar Tabar ni nani?
Ni mwanamke wa miaka 22 ambaye alizua gumzo katika vyombo vya habari duniani baada ya kuweka mtandaoni picha na video ambazo zinazomuonesha akifanana na Angelina Jolie.
Muonekano wake wa kutisha ulizua hofu kuhusu idadi ya upasuaji aliyofanyiwa kufanana na nyota huyo wa Marekani.

Chanzo cha picha, Instagram
Lakini baada ya kupata ufuasi mkubwa katika mtandao wa Instagram,Bi Tabar aligusia kuwa muonekano wake ulitokana na picha zake kufanyiwa ukarabati wa kidijitali -hali iliyomfanya aonekana alivyokua.
Tunafahamu nini kuhusu kukamatwa kwake?
Maafisa wa mahakama walimkamata Tabar baada ya watu kuwasilisha malalamiko dhidi yake, Tasnim iliripoti.
Analaumiwa kwa kukufuru , kuchochea ghasia, kumiliki mali kiharamu, kukiuka maadili ya mavazi ya nchi na kuwasahwishi vijana kufanya ufisadi.
Akaunti yake ya Instagram imefutwa.
Anajiunga na orodha ndefu ya washawishi wa Iran wa mtandaoni na mwanablogu wa mitindo ambao wamekiuka sheria.
Ripoti ya kuzuiliwa kwake imezua hisia kali mitandaoni baadhi ya watu wakiishtumu serikali kwa hatua hiyo.
Wengine walihoji makosa anayodaiwa kutekeleza wakisema laiti angelichukuliwa hatua kwa ubadhirifu wa fedha au mauaji.












