Sarafu mpya: Matumizi ya noti ya zamani ya shilingi 1000 Kenya kufikia kikomo

New Kenyan notes

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sarafu mpya zilizinduliwa kutimiza masharti ya katiba, kukabiliana na ufisadi na fedha ghushi

Zaidi ya dola milioni 600 ya noti ya zamani ya shilingi elfu moja nchini Kenya hazijarudishwa saa kadhaa kabla ya muda wa mwisho wa matumizi ya fedha hizo kuwadia.

Benki Kuu ya Kenya inatafakari zilipo fedha hizo huku ikishinikiza watu kuzibadilisha na sarafu mpya ya shilingi elfu moja iliyotolewa na serikali mwezi Juni mwaka huu.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha Televisheni nchini Kenya kuelekea mwisho wa oparesheni hiyo, Gavana wa Benki Kuu ya Kenya Dkt. Patrick Njoroge amesema 70% fedha hizo hazijarudishwa.

Inakadiriwa kuwa noti milioni 152.7 kati ya noti milioni 217.6 za noti ya shilingi elfu moja ya zamani bado zipo katika mzunguko wa fedha.

Lengo la kuondoa sarafu hiyo katika matumizi ni kukabiliana na uhalifu wa kifedha,kwa mujibu wa mtandao wa Haki wa masuala ya ulipaji ushuru barani Afrika ambao ulisema kuwa "Kenya imekua ikipoteza takriban dola milioni 400 kila mwaka, kuanzia mwaka 2011, kupitia biashara haramu."

Tarehe 31 mwezi Mei mwaka 2019 Serikali ya Kenya ilitoa notisi ya kusitisha utumizi wa sarafu hiyo kuanzi Oktoba mosi.

New Kenyan notes

Chanzo cha picha, Getty Images

Kufuatia hatua hiyo Sarafu mpya ya shilingi 1,000 ilizinduliwa mwezi Juni na wateja walipewa miezi minne kubadilisha noti za zamani.

Gavana wa Benki Kuu ya Kenya Patrick Njoroge amesema hatua hiyo inalenga kukabiliana na ulaji rushwa na kufunga mienya inayochangia uhalifuwa kiuchumi.

Thamani ya noti ya shilingi 1,000 iki juu nchini Kenya na kwa mujibu wa Bw. Njoroge, Shilingi hiyo ya Kenya ni sawa na dola ya Marekani katika kanda ya Afrika Mashariki kutokana na jinsi inavyotambuliwa.

Sarafu zingine zitaondolewa kadiri muda utakavyosonga mbele.

Sarafu ya zamani ya shilingi 1,000 imeondolewa ili kukabiliana na ubadhirifu wa fedha na utakatishaji wa fedha

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sarafu ya zamani ya shilingi 1,000 imeondolewa ili kukabiliana na ubadhirifu wa fedha na utakatishaji wa fedha

Mahakama ilifutilia mbali ombi la kurefusha muda wa mwisho wa matumizi ya sarafu ya shilingi 1000.

Siku za hivi karibuni wafanyibiashara wameripoti matumizi makubwa ya noti hizo kwa pesa taslimu ikiwa ni pamoja na kununuzi wa gari la kifahari la aina ya Mercedes Benz.

Baa moja imewapatia fursa wateja wake kubadilisha noti hiyo ya zamani ya shilingi elfu moja kwa ''kuandaa hafla ya kuaga sarafu hiyo".