SportPesa na Betin: Kampuni za kamari zasitisha huduma zao Kenya

SportPesa na Betin: Kampuni za kamari zasitisha huduma zao Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images

Kampuni za kamari SportPesa na Betin zimesitisha operesheni zake nchini Kenya kufuatia mzozo wa muda mrefu kuhusu ulipaji wa kodi na serikali ya Kenya.

Kenya imeziwekea kampuni hizo kodi ya asilimi 20 katika shughuli zake zote.SportPesa, na Betin zinadhibiti asilimia 60 ya sekta ya kamari nchini Kenya , ikimaanisha kwamba maelfu ya wafanyakazi huenda wakapoteza kazi zao.

Kampuni hizo za kamari zilisema mbali mbali kwamba zimeamua kuchukua hatua hiyo baada ya kodi ilizowekewa kufanya biashara yao kuendelea.

Walisema kwamba kodi hiyo waliowekewa baada ya nyengine kuhusu mshindi imeathiri pakubwa faida yao.

SportPesa, ambayo ndio kubwa zaidi nchini Kenya kutokana na ufuasi pia ilisema kwamba kuna ukosefu wa uelewa kutoka kwa serikali kuhusu jinsi mapato katika sekta hiyo hupatikana hatua iliozua mkwamo katika mazungumzo.

Kamari ni biashara ya mabilioni ya dola barani Afrika, na utafiti unaonyesha idadi kubwa ya wacheza kamari wakicheza kwenye Ligi ya Primia ya Uingereza ambayo ina ufuasi mkubwa barani .

Sportpesa, ambayo ilianza nchini Kenya ilipata pesa za kutosha na kupanuka hadi nchi nne ikiwemo Uingereza, ambapo iko na mikataba ya udhamini na timu ya Everton na Hull City.

Sportpesa pia ni mshirika rasmi wa betting wa Kiafrika wa ligi ya La Liga na ina mkataba na Timu ya Mashindano ya Mchezo wa magari ya langalanga kwa jina Formula 1.

Mnamo mwezi Julai zaidi ya kampuni 25 za kamari zilipokonywa leseni zao za kufanya kazi na serikali, kwa tuhuma za kutolipa ushuru.

Kenya pia imekuwa ikizikamata kampuni za kamari zisizo halali , ikizifunga na hata kuwafukuza wakuu wa kampuni hizo kwa kukiuka vibali vyao vya kufanya kazi.

Leseni zao bado hazijapeanwa tena. Uchunguzi wa kieneo ulibaini kwamba Kenya ina idadi kubwa zaidi ya wachezaji kamari barani Afrika wenye umri chini ya miaka 35.

Wakenya zaidi ya nusu milioni wamepigwa marufuku na wadeni wao na serikali inaamini kwamba wengi walikopa pesa ili kucheza kamari.

Utafiti unasemaje kuhusu kamari Kenya?

Vijana katika kituo cha kucheza kamari cha Betin jijini Nairobi, baadhi wanasema hawana ajira
Maelezo ya picha, Vijana katika kituo cha kucheza kamari cha Betin jijini Nairobi, baadhi wanasemaukosefu wa ajira ndio sababu inayowafanya wacheze

Mchezo wa kamari unaendelea kuenea barani Afrika haswa miongoni mwa mashabiki wa soka. Ni biashara sasa iliyo na thamani ya mabilioni ya dola kwa kampuni zinazoendesha biashara hii, lakini si vile kwa wanaocheza, amebaini mwandishi wa BBC Ferdinand Omondi.

Alipotembelea Katika chumba kimoja katikati mwa jiji la Nairobi, aliwapata vijana kadhaa wakiwa wamesimama wakitizama televisheni kwa umakini, huku wakiwa wameshilia risiti mikononi. Walikuwa ndani ya chumba cha kucheza kamari, kwa ajili ya kujaribu bahari yao.

Mara nyingi mchezo wa kamari huchezwa kwa timu za kandanda za bara Ulaya , lakini kwa sasa msimu uko likizoni. Katika televisheni ni michezo ya kandanda bandia iliyotengenezwa kwa kompyuta, ambapo wachezaji wanakuwa ni vibonzo, lakini bado wanakamari wanacheza kutambua mshindi baina ya timu mbili bandia.

Katika televisheni nyingine kuna mashindano ya vibonzo vya mbwa , lakini wachezaji hawajali, wanaendelea kubahatisha, anasema Omondi ambaye alitembelea kituo kimoja cha Kamari jijini Nairobi.

Asilimia 75 ya wakenya walio na umri wa chini ya miaka 35 wamewahi kucheza kamari
Maelezo ya picha, Asilimia 75 ya wakenya walio na umri wa chini ya miaka 35 wamewahi kucheza kamari

Dommie, ni kijana ambaye hana kazi hufika kwenye kituo cha kamli kujaribu bahati yake: ''Sisi kama vijana tunajaribu kutafuta kazi hatuna, tumekuja kupata pesa ya rahisi hapa, sio eti nanajua nitapata nini, hii ni kubashiri tu''

Ahadi ya kupata ushindi mkubwa ndio kivutio kikubwa Zaidi kwa wachezaji hawa. Utafiti uliofanywa na kampuni ya Geopoll unaonyesha kwa taifa la Kenya ndilo linaloongoza barani afrika kwa wachezaji kamari. Asilimia 75 ya wakenya walio na umri wa chini ya miaka 35 wamewahi kucheza kamari.

Tanzania ni miongoni mwa nchi tano zinazoongoza kwa mujibu wa utafiti huo. Wengi wanacheza kwa urahisi kwa njia ya simu. Mmoja wao ni Justin Sanyo, ambaye anasema kuwa, japo ni mwanasayansi aliye na mshahara wake, hawezi akakosa kutenga kiasi cha mshahara wake kucheza kamari.

''Baadhi yetu wamechukua mchezo wa kamari kama kazi, na kwa wengine ni tabia ya kila siku. Ila tunafahamu kwamba kamari ni biashara, na wenye makampuni wanataka tupoteze fedha ili wapate faida. Kwa hivyo tahadhari ukiwa unacheza, uchague kwa makini sana timu utakazofanya nazo kamari''.

Kwa kuwa uwezekano wa kupoteza pesa ni mkubwa kuliko wa kuzipata, kwa wasio na kazi kama Dommie, ni kuhatarisha hela zao kidogo walizo nazo. Alipoulizwa ikiwa ataweza kuuacha mchezo huo alisema: '' Huu ni mchezo ambao nimejiingiza, lakini usipende mtoto wako ajiingize kwenye mchezo huu, au mtu wako. Mimi nimesoma niko na vyeti vyangu vimelala nyumbani, wakinipatia kazi mimi nitaacha, lakini sasa nitaachacje mchezo huu wakati ninakuja kubahatisha''.

Wachezaji kamari wameufanya mchezo huu kuwa biashara ya thamani ya mabilioni ya dola Afrika na ulimwenguni.
Maelezo ya picha, Wachezaji kamari wameufanya mchezo huu kuwa biashara ya thamani ya mabilioni ya dola Afrika na ulimwenguni.

Wachezaji kamari wameufanya mchezo huu kuwa biashara ya thamani ya mabilioni ya dola Afrika na ulimwenguni. Sasa serikali pia zinataka haki zao kwa njia ya kodi.

Nchini Kenya makampuni ya kamari hutozwa asilimia 30 ya mapato kama kodi, lakini katika bajeti ya nchi iliyosomwa hivi karibuni, serikali imeongeza kodi nyingine ya asilimia kumi kwa kila hela ilayowekwa kama kamari ama dau.

Kumaanisha kuwa mchezaji atatozwa hata kabla hajashinda chochote. Ikiwa hatua hii itawavunja moyo wachezaji au la, ni swala la kusubiriwa.