Wahamiaji 66 walio hatarini zaidi kutoka Libya wamewasili nchini Rwanda

Wahamiaji kutoka Libya wakipokelewa nchini Rwanda
Maelezo ya picha, Wahamiaji kutoka Libya wakipokelewa nchini Rwanda

Kundi la wahamiaji 66 linalojumuisha watu watu walio hatarini zaidi pamoja na watoto walio peke yao limewasili nchini Rwanda kutoka Libya, Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi (UNHCR), limesema.

Miongoni mwa watu hao ambao baadhi yao wanatoka mataifa ya upembe wa Afrika, ni mtoto wa miezi miwili mwenye asili ya kisomali aliyezaliwa katika kituo cha kuwazuilia wakimbizi nchini Libya.

Wahamiaji wa Libya wakiwa safarini kuelekea nchini Rwanda

Chanzo cha picha, UNHCR

Msemaji wa UNHCR kanda ya Afrika Charlie Yaxley ameiambia BBC nchini Rwanda kuwa shirika hilo litawatafutia stakabadhi za kuomba hifadhi wale ambao wanataka kuishi Rwanda au kuwasaidia wale wanaotaka kurejea makwao.

"Nchini Rwanda tutawapatia chakula, maji , malazi na mahitaji mengine ya muhimu. Tuna watalaamu tisa watakaowasaidia katika kupona kiwewe cha yale waliyoyapitia Libya" Yaxley amesema.

Unaweza pia kusoma:

Wahamiaji hawa wataishi katika kituo cha muda kilichopo umbali wa saa moja kwa gari kutoka mjini Kigali.

Akitoka katika kituo cha ukusanyaji wa wahamiaji cha Libya , Daniel mmoja wa wahamiaji katika kundi lilililohamishiwa Rwanda aliiambia BBC wiki iliyopita kuwa wanafurahia kuondoka Libya.

"Tulipokuwa tunaweka sahihi ya kidole tuliona barua inayosema tunaondoka kuelekea Rwanda na tukajihisi ni kama tulikuwa tunatengana na kifo "

Wahamiaji wa Libya wakiwa safarini kuelekea nchini Rwanda

Chanzo cha picha, UNHCR

Zaidi ya wahamiaji 4,500 wanashikiliwa katika mahabusu baada ya ndoto yao ya kuvuka bahari ya Mediterranean kuelekea ulaya kukatizwa..

Rwanda ilikubali kuwahfadhi wahamiaji 500 kwa ushirikiano na UNHCR, na Muungano wa Afrika ulitoa hakikisho la usafiri wao wa kutoka Libya kuelekea Rwanda , ili kuwaepusha na hatari ya kushambuliwa kwa roketina kubakwa . Haijafahamika wazi ni kwa muda gani wahamiaji hao watakuwa Rwanda na wana uhuru kwa kiwango gani kuondoka nchini humo

"Wakimbizi watakaotaka kuishi Rwanda daima watapewa ukimbizi ," alisema Olivier Kayumba,katibu wa kudumu katika wizara ya udhibiti wa masuala ya dharura na masuala ya wakimbizi .

Maafisa wanasema miongoni mwa wahamiaji hao 66 ni wanawake na watoto walio katika hali mbaya kiafya na vyombo vya habari vilidhibtiwa kuwaona.

Hatua ya kuwapeleka wahamiaji nchini Rwanda ilichukuliwa baada ya juhusi za ufadhili mbali mbali za kudhibiti wimbi la wahamiaji wanaojaribu kuingia Ulaya kupitia safari hatari ya bahari ya Mediterranean kugonga mwamba.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji linasema kuwa zaidi ya watu 45,500 waliingia Ulaya kupitia bahari ,kiwango hicho kikiwa kimepungua kwa 30% ikilinganishwa na mwaka 2018.

Wengi miongoni mwa wahamiaji wanaopitia katika bahari ya Meditteranian hukabiliwa na hatari ya kuzama

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Wengi miongoni mwa wahamiaji wanaopitia katika bahari ya Meditteranian hukabiliwa na hatari ya kuzama

Kituuo kikubwa cha kuwaokoa wahamiaji kinachoendeshwa na Umoja wa Mataifa kipo katika taifa la Niger ambako kuna njia ya wahamiaji ya kaskazini mwa Afrika kwa sasa kimefurika wakimbizi sawa na kile cha Umoja huo kilichopo katika mji mkuu wa Libya Tripoli ambacho kina jumla ya wahamiaji na wakimbizi 1,000.

Mataifa ya ulaya yamekuwa yakiwashughulikia kwa njia isiyofaa wahamiaji katika juhudi za kudhibiti wimbi la wakimbizi , na wamekabiliwa na ukosoaji kutoka kwa badhi ya mashirika ya haki za binadamu ambayo pia yaliwalaumu kwa kukubali kukubali idadi ndogo ya wahamiaji.

Wahamiaji

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wahamiaji

Ni kundi dogo tu la watu 2,900 ambao waliokolewa katika kituo cha Niger waliopata uhamiaji katika mataifa ya Ulaya na kwingineko.

Takriban wahamiaji 6,000 kutoka mataifa ya Eritrea, Ethiopia, Somalia, Sudan na mataifa mengine bado wako katika vizuizi vinavyoendeshwa na wanamgambo wa Libya wanaoshutumiwa kuwatesa. Baadhi ya wahamiaji wamekuwa wakizuiwa katika bahari ya Mediterranean na walinzi wa mwambao wa Libya wanaodhaminiwa na Muungano wa Ulaya, ambao wamekuwa wakilengwa na shutuma za mateso dhidi ya wahamiaji.

Wengi miongoni mwa wahamiaji wanatoka katika mataifa ya upembe wa Afrika yakiwemo mataifa ya Somalia, Eritrea na Ethiopia.