Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mahakama ya juu zaidi Uingereza: Kusitishwa bunge kulikuwa kinyume na sheria, jaji aamua
Uamuzi wa Boris Johnson kusitisha bunge Uingereza, ulikuwa kinyume na sheria, mahakama ya juu zaidi nchini humo imeamua.
Johnson alisitisha vikao vya bunge kwa wiki tano mapema mwezi huu, lakini mahakama imesema ilikuwa ni makosa kuwasitisha wabunge kuendelea na majukumu yao kuelekea Brexit Oktoba 31.
Spika wa bunge la wawakilishi, John Bercow amesema wabunge watarudi kwenye vikao Jumatano baada ya uamuzi huo wa kihistoria.
Rais wa mahakama ya juu zaidi Lady Hale amesema "athari za msingi wa demokrasia zilivukwa mpaka."
Baadhi ya wabunge sasa wanashinikiza waziri mkuu ajiuzulu - Downing Street imesema "kwa sasa inatafakari uamuzi huo".
Johnson alilalamika kwamba anataka bunge lisitishe vikao kabla ya hotuba ya Malkia ili aweze kueleza bayana sera zake mpya za serikali.
Lakini wakosoaji wanasema alikuwa anajaribu kusitisha wabunge kuchambua mipango yake ya Brexit na hatua hiyo ya kusitisha vikao ilikuwa ndefu mno kusubiria hotuba ya Malkia.
Akisoma uamuzi huo rais wa mahakama hiyo ya juu zaidi, Lady Hale, amesema: "Uamuzi wa kumshauri Malkia kulisitisha bunge ulikwenda kinyume na sheria kwasababu iliweza kuchangia kutatiza au kusitisha uwezo wa bunge kuendelea na majukumu yake kikatiba pasi sababu ya maana."
Lady Hale amesema uamuzi huo wa pamoja wa majaji 11 unamaanisha kuwa bunge halijasitishwa- Hatua hiyo iliyoidhinishwa haina athari yoyote.
Spika Bercow amesema wabunge wanahitaji kurudi "kufuatia uamuzi huo", na aliagiza "maafisa wa bunge la wawakilishi kutayarisha ... kurudi kuendelea kwa vikao vya bunge" kuanzia 11:30 BST Jumatano.
Mahakama pia imeshutumu muda wa kusitishwa vikao hivyo, huku Lady Hale akisema haiwezekani kutamatisha, kutokana na ushahidi uliowasilishwa mbele yetu, kwamba kulikuwa na sababu yoyote, kando na kwamba ni sababu nzuri - kumshauri Malkia kusitisha vikao vya bunge kwa wiki tano".
Athari imeshatokea
Clive Coleman, Mwandishi wa BBC wa masuala ya sheria
Hii ni sheria, katiba na bomu la kisiasa.
Pengine ni muhimu kushusha pumzi na kutambua uzito wa waziri mkuu wa Uingereza kukutikana na mahakama ya juu zaidi nchini kwenda kinyume na sheria kwa kufunga taasisi huru katika katiba, bunge, katika wakati ambapo kuna mzozo wa kitaifa.
Huenda mahakama imekosa tu kutaja kuwa Boris Johnson alikuwa na dhamira isiyo sahihi ya kutatiza ukaguzi wa bunge lakini athari imeshatokea, amekutikana kuchukuwa hatua kinyume cha sheria na kulisitisha bunge kufanya kazi yake pasi kuwepo sababu ya kisheria.
Na mahakama imetupilia mbali ushauri wake kwa Malkia na agizo la baraza uliositisha rasmi bunge.
Hiyo ina maana bunge halikuwahi kusitishwa na kwahivyo tunachukulia kuwa wabunge wako huru kuingia bungeni.
Huu ni mfano wa aina yake wa majaji walio huru, kupitia mfumo wa ukaguzi wa sheria , kusitisha hatua ya serikali kwasababu ilichofanya ni kinyume na sheria.
Hata kama u mkubwa kiasi gani, sheria ndio mambo yote - hata iwapo wewe ni waziri mkuu.
Hatua ambayo haikutarajiwa, ya aina yake na inayozusha mtikisiko - ni vigumu kukadiria, umuhimu wa kikatiba na kisiasa unaotokana na uamuzi wa leo.
Mahakama ilikuwa inatafakari nini?
Uamuzi uliotolewa baada ya kusikizwa kwa siku tatu kesi hiyo katika mahakama ya juu zaidi wiki iliyopita iliangazia rufaa za pande mbili - moja kutoka kwa mwanaharakati na mfanyabiashara Gina Miller, na ya pili kutoka kwa serikali.
Bi Miller alikuwa amekata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama kuu Uingereza kuwa kusitishwa kwa bunge ni 'jambo la kisiasa' na sio suala la mahakama.
Serikali ilikuwa imekata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya Uskotchi kuwa kusitishwa kwa bunge ni 'kinyume cha sheria' na hatua hiyo ilitumika 'kulitatiza' bunge.
Mahakama iliamua kwa faida ya rufaa aliokata Bi Miller na dhidi ya rufaa ya serikali.
Waliohusika na kesi wamepokeaje hatua hii?
Akizungumza nje ya mahakama, Bi Miller amesema uamuzi huo unatoa ujumbe mkubwa.
"Waziri mkuu huyu ni lazima afungue milango ya bunge kesho. Ni lazima wabunge warudi na wawe wakakamavu katika kuiwajibisha serikali," ameongeza
Mwanachama wa SNP Joanna Cherry, aliyeongoza kesi ya Uskotchi amemtaka waziri mkuu Johnson ajiuzulu kufuatia uamuzi huu.
"Mahakama ya juu zaidi Uingereza imeamua kwa pamoja kuwa ushauri wake wa kusitisha bunge, ushauri wake kwa Malkia, ni kinyume na sheria,"amesema.
"Msimamo wake hauwezi kutetewa na anapaswa kwa mara ya kwanza kufanya lililo sawa, na ajiuzulu."