Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanafunzi 23 wapoteza maisha kwenye ajali ya moto karibu na mji wa Monrovia Liberia
Moto umechoma shule ya bweni katika eneo moja lililopo viungani mwa mji mkuu wa Liberia Monrovia na kuwaua watoto 23.
Moto huo unaaminika kuanza mapema alfajiri wakati wanafunzi hao walipokuwa wakilala katika bweni moja lililoshikana na msikiti.
Polisi wameambia BBC kwamba wanaendelea kusaka miili katika vifusi vya jengo hilo.
Rais George Weah ametuma ujumbe wa Twitter katika rambirambi zake kwa familia za waathiriwa
Msemaji wa Polisi Moses Carter alikiambia chombo cha habari cha 'Reuters' kwamba huenda moto huo ulisababishwa na shoti ya umeme , lakini uchunguzi unaendelea.
Maafisa waliambia AFP kwamba waathiriwa walikuwa kati ya umri wa miaka 10 hadi 20
Mwandishi wa BBC Jonathan Paye-Layleh amesema kwamba gari za dharura(Ambulance) za shirika la msalaba mwekundu tayari zimechukua miili kutoka eneo la tukio na kuna mipango ya kuizika siku ya Jumatano jioni.
Mamia ya watu walikongamana katika shule hiyo kufuatia mkasa huo.
Muhubiri Emmanuel Herbert aliyeshuhudia tukio hilo aliambia BBC kuwa aliamka na kusikia sauti ya moto huo na kupiga kengele ya kanisa ili kutafuta usaidizi.
Nilipotoka nje na kutazama eneo lote lilikuwa jekundu: Nilipotazama dirishani niliuona eneo lote limeshika moto , aliambia BBC.
Lakini alisema kwamba hakuweza kuingia katika jengo hilo kwa kuwa lilikuwa na mlango mmoja pekee ambao ulikuwa umefungwa.