Tanzania: Magufuli awasamehe wabunge waliomzungumzia vibaya

Magufuli

Chanzo cha picha, AFP

Rais Magufuli amesema amewasamehe wabunge January Makamba na William Ngeleja baada ya sauti zinazodaiwa zao kusambaa mitandani wakiwa wanamzungumzia vibaya rais.

Akizungumza na wataalamu wa ujenzi hii leo amesema kuwa ana uhakika kuwa sauti zile zilikuwa zao lakini amefikiria na kuwasamehe.

"Siku za hivi karibuni kuna watu walinitukana na kuthibitisha kuwa sauti zile ni zao, nikawa nakaa nafikiriaa, nikasema hawa wakipelekwa katika kamati ya siasa, adhabu itakuwa kubwa nikasema ngoja ninyamaze lakini wakajitokeza wawili wakaniomba msamaha...

Nilijiuliza... kila siku mimi huwa naomba msamaha kwa Mungu , kwa ile sala ya "tusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe wengine", nikaona hawa waliokuja kuniomba msamaha nisipowasamehe nitabaki na maumivu makubwa hivyo nikaamua kuwasamehe.

Hawa waliokuja kuniomba msamaha na kutoa kweli katika dhamira yao ni Januari Makamba na William Ngereja.

Niliwasamehe na kusahau" Magufuli aeleza.

Rais Magufuli akiwa na mbunge wa Bumbuli, January Makamba mwaka 2015

Chanzo cha picha, Makamba FACEBOOK

Maelezo ya picha, Rais Magufuli akiwa na mbunge wa Bumbuli, January Makamba mwaka 2015

Januari Makamba ambaye ni mbunge wa CCM jimbo la Bumbuli na William Ngereja ambaye ni mbunge wa Sengerema kupitia chama hicho ni miongoni mwa viongozi ambao sauti zao zilisikika mitandaoni zikimzungumzia vibaya rais Magufuli.

Magufuli

Chanzo cha picha, William Ngereja/TWEETER

Maelezo ya picha, Rais Magufuli akimsikiliza Ngereja

Hata hivyo Magufuli hajasema lolote kwa wengine ambao sauti zao zilidaiwa kusikika kama amewasamehe au bado.

January Makamba, aliyehudumu katika nafasi ya Waziri wa Mazingira na Muungano nchini Tanzania toka kuingia madarakani kwa Rais John Pombe Magufuli ametimuliwa kazi mara baada ya sauti yake kuvuja mitandaoni ikisikika kumsema vibaya.

Kupitia mtandao wa Twitter, Makamba ameandika: "Ni kweli nimeyapokea mabadiliko yaliyofanywa kwa moyo mweupe kabisa kabisa. Nitasema zaidi siku zijazo." Huku akiambatanisha maneno hayo na picha yake na rais msaafu Ally Hassan Mwinyi wakiwa wanaangua kicheko.