Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Makonda ajipanga kupambana na wanaume wanaowatelekeza wanawake
- Author, Na Dinah Gahamanyi
- Nafasi, BBC News Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 2
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amepanga kuzisajiri ndoa zote za mkoa huo kwa ajili ya kukabiliana na wanaume wanaowalaghai wanawake kimapenzi.
Bwana Makonda amesema kuna mpango wa kuanzisha kanzi data ya ndoa zote zilizopo kwenye mkoa wake ili kupunguza utapeli wanaofanyiwa wanawake kwa kudanganywa kuolewa.
Kanzidata hiyo itahusisha usajili wa ndoa zote ili wanaume waliooa waweze kubainika na kuwanusuru wanawake wasitapeliwe na kuumizwa mioyo kwa kutegemea ndoa.
Makonda amesema pamoja na kanzidata hiyo atatumia mkutano wa SADC kupata uzoefu kutoka kwa nchi nyingine kufahamu namna gani wanakabiliana na utapeli wa aina hiyo.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kumekuwepo na malalamiko mengi ya wanawake kuumizwa hivyo wakati umefika wa kuanza kushughulikia.
Mkakati wake ameutanga pia kwenye ukurasa wake wa Twitter:
"Tutaanza kuangalia na kupata uzoefu kwa wenzetu wa SADC ambao kama haya wanashughulikiaje na mkutano ukiisha tutajadiliana kama mkoa tunawezeshaje usajili huo," amesema.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam amedai kwamba amekuwa akikutana na malalamiko mengi sana kutoka kwa wadada wa mkoa huo kwamba wamechoka kutapeliwa.
''Tunaompango mzuri tu wa kukutana na wadada walioumizwa, huwezi kuwa kiongozi afu unaongoza watu walioumizwa na kutapeliwa na vijana ambao wanaona raha tu, tunataka tufikie hatua mtu akioa anaandika kwenye database ya mkoa, ili mwanamke akitaka kuolewa anaangalia huyu jamaa kaoa au hajaoa'' amesema Makonda.
Makonda ameongeza kuwa, wanaoumizwa wengi ni kina dada kwa sababu wanawake wakipenda huwa wanapenda kweli na wao kuwa wahanga wakubwa wa matapeli.
Amesema atatumia mkutano wa SADC unaowajumuisha wakuu 16 wa nchi wanachama kujifunza mambo mbalimbali, ikiwemo suala la wadada kutapeliwa juu ya masuala ya ndoa, kwa kuangalia nchi zingine zinashughulika vipi na masuala hayo.
Hii si mara ya kwaza kwa mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salam, kujaribu kusaidia kutatua matatizo yanayowakumba wanawake jijini Dar es Salaam.
Mwezi Aprili mwaka 2018, Bwn.Makonda alitoa agizo kwa wanawake wanaodai kutelekezwa na wazazi wenzao kufika katika ofisi yake ili wapate kusikilizwa
Kufuatia taarifa hiyo mamia ya wanawake walijitokeza na kwenda katika ofisi yake kuelezea machungu waliyodai kupitia kutokana na kutelekezwa na wame zao.
Hatua hiyo iliibua hisia tofauti miongoni mwa Watanzani hususan katika mitandao ya habari ya kijamii, baadhi wakimkosoa na baadhi wakiafiki hatua yake ya kuwasikiliza akina mama.
naweza pia kutazama: