Uganda: Mwanaharakati Stella Nyanzi afungwa miezi 18 kwa kumtusi rais Museveni

Dkt Stella Nyanzi amepatikana na hatia ya unyanyasaji wa mtandaoni

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Dkt Stella Nyanzi amepatikana na hatia ya unyanyasaji wa mtandaoni

Mwanaharakati msomi wa Uganda Dkt. Stella Nyanzi amehukumiwa kifungo cha miezi 18 jela.

Nyanzi alipatikana na hatia ya unyanyasaji wa kimtandao pamoja na mawasiliano ya udhalilishaji dhidi ya rais Yoweri Museveni na familia yake.

Dr. Nyanzi alikataa kumsikiliza hakimu akisoma hukumu dhidi yake na badala yake kufanya vurugu kwa kuvua nguo na kuonesha sehemu ya mwili wake.

Mwanaharakati huyo hakuwa mahakamani lakini hukumu dhidi yake ilitolewa kupitia video link kutoka jela.

Wakati kesi ikiendelea Bi. Stela alikataa kuomba dhamana na amekuwa katika gereza kuu la Uganda la Luzira kwa miezi minane.

Sasa atazuiliwa gerezani kwa miezi tisa zaidi.

Bi Nyanzi alishtakiwa kwa kumtusi rais Yoweri Museveni, na mkewe Janet Museveni pamoja na marehemu mama yake Museveni, Bi Esteri Kokundeka kupitia Facebook
Maelezo ya picha, Bi Nyanzi alishtakiwa kwa kumtusi rais Yoweri Museveni, na mkewe Janet Museveni pamoja na marehemu mama yake Museveni, Bi Esteri Kokundeka kupitia Facebook

Nchini Uganda Uganda, Bi Nyanzi amekua sura na sauti ya matumizi ya lugha chafu katika upinzani dhidi ya kile anachokiita serekali mbaya.

Haoni haya ya kuandika maneno ambayo wengi wanayaona kama ni ya aibu.

Nyanzi ni mtafiti wa masuala ya jamiina msomi na kabla ya kuanza kampeni yake ya matusi kupitia kwenye mitandao ya kijamii aliwa ni mwalimu katika chuo kikuu cha umma nchini Uganda cha Makerere.

Mashtaka hayo chini ya ya sheria ya matumizi mabaya ya kompyuta ni jaribio la utekelezwaji wa sheria ya uhalifu wa mtandaoni inayokosolewa.

Wengi miongoni mwa washukiwa wa unyanyasaji wa mtandaoni, wamekuwa hata hivyo wakishutumiwa kwa kumshambulia rais Museveni.

Kufikia sasa karibu watu 15 wamekamatwa kwa madai ya kumkasirisha rais Museveni tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2016.

Dr Stella Nyanzi, Mtafiti wa Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Dr Stella Nyanzi, Mtafiti wa Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda

Wengine waliokamatwa

Watu wengine waliokamatwa ni pamoja na Raymond Soufa, maarufu Peng Peng, Nasser Mugerwa pamoja na Jane Kuli, ambao walizuiliwa na polisi kwa kukiuka sheria hiyo.

Andrew Mwenda, Mmiliki wa jarida la kibinafsi, aliyepata umaarufu miaka ya 1990 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000 kwa kukosoa utawala wa Rais Museveni kwa kukandamiza vyombo ya habari anasema Waganda wana haki ya kumkosoa rais.

Bw aliandika katika mtandao wake wa Twitter: "Kukamatwa kwa Joseph Kabuleta kwa "kumkasirisha Rais" ni ushamba na hatua iyo haina nafasi katika ulimwengu wa sasa! Waganda wana kila sababu ya kumkosoa Rais. Wamemchagua awahudumie. Wanatakiwa wawe huru kumwelezea kero lao ikiwa hawajaridhishwa na jinsi anavyoongoza nchi!"

Mwaka jana, Mbunge wa Manispaa ya Mukono MP Betty Nambooze alikamatwa na kuzuiliwa kwa kukiuka sheria ya kutumia vibaya mitando ya kijamii. Inadaiwa ujumbe aliyochapisha katika mitandao ya kijamii kabla na baada ya kupigwa risasi na kuuawa kwa mbunge wa Arua Ibrahim Abiriga na ndugu yake Saidi Butele Kongo ulikua wa kichocheza.

Januari 2019: Polisi katia wilaya ya Gomba walimkamata mtu wa miaka 19 kwa kumtusi Rais Museveni. Mamlaka zilisema,Joseph Kasumba, mkaazi wa Kanoni, alimtukana rais Museveni, majina ya kumdhalilisha.

Juni 18, 2019: Andrew Mukasa, ambaye pia anafahamika kama Bajjo, alishitakiwa kwa kuchochea ghasia thidi ya utawala wa rais Museveni na kuvunja sheria ya mawasiliano.

Novemba 2017: Wakurugezi watano wa na wahariri watatu wa gazeti la Red Pepper washitakiwa kwa makosa saba ikiwa ni pamoja na ukiukaji wa sheria ya utumizi wa kompyuta, kutia dosari sifa ya rais Museveni na kumsumua kiakili ndugu yake mdogo Jenerali Henry Tumukunde.