Udumavu wa watoto umekithiri katika mkoa wa Iringa Tanzania, kulikoni?

Chanzo cha picha, Eric Lafforgue/Art in All of Us
- Author, Halima Nyanza
- Nafasi, BBC Swahili
Mkoa wa Iringa nchini Tanzania umekuwa ukihimiza lishe bora kwa mama wanaonyonyesha, katika jitihada za kupunguza udumavu wa kiasi kikubwa unaoshuhudiwa mkoani humo.
Elimu hiyo inatolewa kama njia moja wapo ya kulikabili tatizo. Kutokana na kwamba hali ya unyonyeshaji katika manispaa ya Iringa kwa ujumla siyo ya kuridhisha
Takwimu za mwaka 2017/18 kutoka mkoa huo zinaonesha kuwa kina mama wanaonyonyesha watoto wao mara tu baada ya kujifungua ni asilimia 53, huku wale wanaonyonyesha miezi sita mfululizo bila kumpa mtoto chakula kingine chochote ni asilimia 35.
Na walio wengi wakichanganya kwa kumpa mtoto vyakula vingine ikiwemo uji na ugali.

Afra Mtuya ni mratibu msaidizi wa Afya ya uzazi na mtoto manispaa ya Iringa, anasema utamaduni pia unachangia kutokana na kwamba wanapata elimu ila baadhi yao wanaamini kuwa mtoto akilia tu ni njaa inamsumbua na sio kitu kingine chochote.
Na hilo anaongeza ni hata kama mtoto ana tatizo lingine.
Ametolea mfano pia tabia ya baadhi ya kina mama kuwapa watoto vyakula tofauti ili wasiweze kusumbua, mfano hata pombe ya kienyeji ya ulanzi inayopewa mtoto ili asisumbue kutokana na kwamba akinywa atalala muda wote.
Amesema watoto kutopewa lishe inayostahili imechangia pia kupanda kwa asilimia ya hali ya udumavu katika manispaa hiyo.

Taarifa nyingine kuu leo:

Katika kipindi cha mwaka 2018 hali ya udumavu ilikuwa ni asilimia 43, lakini kwa sasa imepanda hadi kufikia asilimia 47.
Mtoto akikosa chakula kinachostahili kuna hatari kubwa ya kupata udumavu na magonjwa mbalimbali hususan ya tumbo.
Katika kuhakikisha tatizo hilo linaondoka, wahudumu wa afya na lishe bora katika enoe hilo wamekuwa wakibuni mbinu tofauti ikiwemo kutoa elimu kwa jamii, kuanzia ngazi ya kaya,.
Hilo ni kwa kuwaelimisha kina mama kuhusu umuhimu wa kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama tu katika kipindi cha miezi sita toka kuzaliwa.
Aidha Bi Mtuya anasema wamekuwa wakielimisha baadhi ya kina mama kuondoa imani kwamba mtoto akinywa maziwa ya mama peke yake kwa miezi sita, hashibi.


Faida za maziwa ya mama kwa mwana:
Shirika la afya duniani WHO linapendekeza mama kote duniani kuwanyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza ya uhai wao.
Hilo WHO linasema litachangia ukuwaji wa kisawasawa wa watoto na kuimarika kwa afya zao. baada ya miezi hiyo sita, inashauriwa mzazi kuendelea kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama hadi anapotimia miaka miwili huku akimuongezea vyakula vyepesi vyenye lishe bora.
Baadhi za faiada wanazotaja wataalamu wa afya za kumyonyesha mtoto maziwa ya mama:
- Ni chanzo cha lishe bora kwa watoto
- Hupunguza hatari ya kushikwa na magonjwa
- Hushinikiza uzito wenye afya
- Yana uwezo wa kumfanya mtoto awe mwerevu
- Humsaidia mama kupunguza uzito mwilini
- Mama wanaonyonyesha wamo katika hatari ndogo ya kuugua msongo wa mawazo
- Pia huokoa muda na pesa

''Tunamtengenezea mazingira ya mama mwenye kuweza kushiba ili aweze kutoa maziwa yatakayomtosheleza mtoto wake, kwa vile mama ana shughuli nyingi zinazomfanya asitulie na kuweza kumyonyesha mtoto wake akashiba.
''Ndio maana haamini kama mtoto wake anaweza kushiba...'' Anasema Afra.
Katika kuhakikisha pia tatizo hilo linaondoka, Watendaji wa mitaa na kata katika manispaa hiyo wamesaini mikataba kutokomeza udumavu katika maeneo yao, ili kuhakikisha kila mtoto anapozaliwa, mzazi anafuata kanuni za afya, kuhakikisha kuwa mtoto wake ana kuwa vizuri.















