Al-Shabab: Wakaazi wawaokoa wenzao katika uvamizi wa wapiganaji hao Mandera Kenya

Kulikuwa na kihoja wakati wa makabiliano kati ya wakaazi na wapiganaji wa al-Shabab katika eneo la Kutulo kaunti ya Mandera.
Kulingana na gazeti la The Standard nchini Kenya takriban wapiganaji watatu wa kundi hilo kutoka Somalia walivamia kituo kimoja cha ujenzi wa hospitali wakiwasaka raia wasio wa eneo hilo.
Lakini kabla ya wao kuwasili , wakaazi waliwaambia wafanyakazi 20 waliokuwa katika eneo hilo la ujenzi- wengi wao wakiwa raia kutoka maeneo mengine ya Kenya kuondoka eneo hilo.
Kulingana na gazeti hilo maafisa wa polisi pamoja na watu walioshuhudia wanasema kwamba kulikuwa na takriban wafanyikazi 20 katika eneo hilo.
Lakini wakati wapiganaji hao walipokuwa wakielekea katika eneo hilo, wakaazi waliwafuata na kuwaelezea kwamba hakukuwa na raia wasio wa eneo hilo.

Waliwafuata wapiganaji hao waliokuwa wakielekea katika eneo la ujenzi ambapo waliwakosa wajenzi hao, lilisema gazeti hilo.
Wapiganaji walifyatua risasi lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa kabla ya kutoroka, kwa mujibu wa kamishna wa kaunti hiyo Mohamed Birik aliyekuwa akizungumza na gazeti la The Standard.
Aliongezea kwamba kitendo cha wakaazi hao kiliokoa maisha ya wengi.
Kulingana na gazeti hilo wafanyakazi waliokuwa wamelengwa baadaye walioondoshwa na kupelekwa hadi kituo kimoja cha polisi katika eneo la Elwak huku kukiwa na hofu ya mashambulizi zaidi.
Kisa hicho kinajiri huku kukiwa na shinikizo la kufungua timbo katika eneo hilo.

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Kenya Fred Matiangi mwezi uliopita aliwahakikishia viongozi wa Mandera kwamba timbo za eneo hilo zitafunguliwa hivi karibuni lakini kwa mpangilio.
''Sio lengo la serikali kukandamiza ama kuangamiza uchumi wa Mandera. Waiswasi wetu ni uhaba wa usalama wa kutosha katika timbo hizo'', alisema matiangi.
Serikali ilitangaza kufungwa kwa timbo mnano tarehe 4 Mwezi Mei 2018 baada ya wachimbaji wanne kuuawa na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa al-Shabab katika eneo la timbo ya Shimbiri Fatuma kusini mwa Mandera.
Juhudu za muungano wa timbo hizo na serikali ya kaunti kuvirai vyombo vya usalama kufungua timbo hizo ziliambulia patupu.
Mahakam kuu iliondoa marufuku hiyo lakini hatma ya biashara hiyo bado haijulikani.
Gavana wa eneo hilo Ali Roba alikua na wasiwasi kwamba kufungwa kwa mpaka wa Kenya na Somalia tangu 2014 kumepunguza kasi ya ukuaji wa uchumi na kuinyima kaunti hiyo takriban shilingi bilioni 3 za mapato.












