Iran imesema video yao inaonyesha 'ndege haikudunguliwa' kama inavyodaiwa

Iran imetoa picha kwenye vyombo vya habari ikikana madai ya Marekani kuwa imedungua ndege isiyo na rubani ya Iran katika eneo la Ghuba.

Televisheni ya taifa imesema inaonyesha meli za kivita katika eneo hilo, na zilipigwa picha na ndege hiyo hiyo baada ya muda ambao Marekani ilitangaza kuwa ilidungua ndege hiyo.

Pamoja na Iran kukana, raisi wa Marekani, Donald Trump amesema ''hakuwa na shaka'' ndege isiyo na rubani ilidunguliwa.

Picha za video zinaonyesha nini?

Video inaonyesha picha za rangi nyeupe na nyeusi za meli za kivita zikitembea ndani ya maji, ikionyesha muda, tarehe na eneo la kijiografia.

Televisheni ya taifa ya Iran imesema kuwa picha hizo zilichukuliwa na ndege isiyo na rubani inayodaiwa kudunguliwa wakati ikiwa angani usawa wa karibu na meli ya kijeshi ya Marekani.

Jeshi la Iran, ambalo lilichapisha picha za video, limesema picha hizo zilirekodiwa ''kabla na hata baada ya Marekani kutoa madai hayo''

Lakini picha hizo zina mashaka, anasema mwandishi wa masuala ya kidiplomasia Paul Adams.

Anasema baadhi ya picha zinaonekana kupigwa picha na helikopta ya Iran ambayo ilikuwa pia kwenye eneo hilo.

Marekani inasemaje?

Raisi wa Marekani Donald Trump amesema jeshi la maji la Marekani limetungua ndege isiyo na rubani ya Iran katika eneo la mpaka kati ya ghuba ya uajemi na ghuba ya Oman.

Amesema meli ya jeshi lake ''ilichukua hatua ya ulinzi'' siku ya Alhamisi baada ya ndege hiyo kusogea kwa takriban mita 914 karibu na chombo hicho.

''Ndege hiyo ilishambuliwa mara moja..baaa ya kupuuza wito wa kusimama.

Iran haraka ilitupilia mbali madai ya Trump, huku afisa mmoja wa juu akisema kuwa huenda walilenga ndege yao wenyewe kimakosa.

''Nina wasiwasi kuwa Marekani iliishambulia ndege yao wenyewe kimakosa! ''Naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran. Abbas Araqchi aliandika kwenye ukurasa wa tweeter siku ya Ijumaa.