Senegal uso kwa uso na Algeria

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshambuliaji wa Senegal Sadio Mane amesema kama atalazimika kushinda kombe la mataifa Afrika kwa kuicha medali yake ya ligi ya mabingwa Ulaya aliyoipata na timu yake ya Liverpool yuko tayari kufanya hivyo.
Senegal inatafuta kunyakua taji la Afcon kwa mara ya kwanza ambapo itakutana na Algeria kwenye fainali jijini Cairo.
Mane aliisaidia Liverpool kupata ushindi wa ligi ya mabingwa dhidi ya Tottenham kwenye fainali ya tarehe 1 mwezi Juni, na pia ana magoli matatu katika mechi tano alizoanza kwenye michuano ya kombe la mataifa Afrika.
''Tunajua haitakuwa rahisi lakini ni kawaida, ni sehemu ya mchezo wa kandanda. Algeria ni timu nzuri, nina matumaini ya ushindi.''
Kocha wa Algeria Djamel Belmadi amesema timu yake ''itapambana'' na kunyakua ubingwa kwa mara ya pili.
''Kwa watu wa Algeria, ninataka kusema: Mimi si mwanasiasa, si mfanya kiini macho wala mchawi, '' aliongeza.
''Lakini tutapambana kama tulivyopambana kufikia kwenye hatua hii.''
Senegal na Algeria zilikutana kwenye hatua ya makundi, kwenye michuano hiyo mwaka 1990, Algeria ikiibuka na ushindi wa 1-0.
Taarifa kubwa kutoka kwenye timu ya Senegal ni kuwa nyota anayecheza nafasi ya ulinzi Kalidou Koulibaly atakosa mchezo huo baada ya kupewa kadi ya pili ya njano wakati wa mchezo dhidi ya Tunisia.
Ni fainali ya tano tangu mwaka 1998 kuwakutanisha makocha wazawa kutoka Afrika.
Kocha wa Senegal Aliou Cisse na wa Algeria Belmadi wote walizichezea timu zao za taifa mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Chanzo cha picha, AFP
Timu hizi zilifikaje fainali?
Algeria imekuwa timu bora kwenye michuano hii, ikiwa kwenye kundi lililokuwa na timu za Senegal, Kenya na Tanzania.
Waliifunga Guinea 3-0 katika hatua ya 16 bora na Ivory Coast kwa mikwaju ya penati katika hatua ya robo fainali.
Senegal, ilinyakua alama sita katika hatua ya makundi, baada ya kushinda mechi dhidi ya Uganda na Benin na kufuzu fainali kwa kuifunga Tunisia kwa goli la kujifunga kwenye muda wa nyongeza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Senegal inaweza kuandika historia?
Pamoja na Senegal kuwahi kufikia hatua ya robo fainali michuano ya kombe la dunia, haijawa moja kati ya timu 14 kuwa mabingwa wa Afrika.
Walifika fainali michuano ya Afcon mara moja mwaka 2002 na kupoteza mchezo kwenye hatua ya mikwaju ya penati walipocheza na Cameroon. Cisse, kocha wao mkuu wakati huo alikosa penati muhimu siku hiyo.
Algeria imecheza kwenye fainali mbili, zote dhidi ya Nigeria na kupoteza mwaka 1980 na kushinda mwaka 1990.

Chanzo cha picha, Getty Images












