Wachuuzi wa mpakani mwa Uganda kupatiwa chanjo dhidi ya virusi vya Ebola

Wafanyakazi wa huduma za afya wamepatiwa chanjo dhidi ya virusi vya Ebola

Chanzo cha picha, Getty Images

Mamlaka za Uganda ziko kwenye mchakato wa kuwatambua watu ambao huenda wameambukizwa na mwanamke mmoja ambaye alionyesha kuwa na dalili za Ebola kwenye soko la Uganda juma lililopita, kabla ya baadae kupoteza maisha mjini Beni, nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa afisa wa afya ya wilaya, mwanamke huyo alitapika sokoni hapo eneo la Mpondwe lililo kwenye mpaka wa Uganda alhamisi juma lililopita-kabla ya kurejea DR Congo na kupoteza maisha kutokana na Ebola.

Alisema kuwa alivuka mpaka kuingia Uganda akitokea Congo kupitia njia ya mpaka isiyo rasmi.

WHO na wizara ya afya nchini Uganda zimethibitisha kuwa mwanamke huyo, muuza samaki alipoteza maisha kutokana na virusi vya Ebola.

Takribani wachuuzi wa samaki 600 na wabadilishaji wa fedha katika soko la mpaka wa Mpondwe wametambulika na watapatiwa chanjo.

Mwezi Juni, kulikuwa na vifo vya watu wawili vilivyothibitishwa kusababishwa na virusi hivyo magharibi mwa Uganda, karibu na mpaka. Tangu wakati huo hakukuwa na ripoti nyingine yeyote kuhusu kuwepo kwa ugonjwa huo nchini humo.

Tukio la hivi karibuni limeongeza hatari ya ugonjwa huo kusambaa Uganda, lakini mamlaka zinasema hazitafunga soko la mpakani kwa sasa.

Zaidi ya watu 6,000, wengi wao wafanyakazi wa afya, wamepatiwa chanjo nchini Uganda tangu mwezi Novemba mwaka 2018.

Tangu mlipuko wa Ebola kutokea Dr Congo, zaidi ya watu 2,000 wameripotiwa kuwa na virusi na watu zaidi ya 1,500 wamepoteza maisha.