Trump amkosoa balozi wa Uingereza kuhusu barua pepe zilizovuja

Donald Trump

Chanzo cha picha, Reuters

Rais wa Marekani Donald Trump amemkosoa balozi wa Uingereza ambaye alisema kwenye barua pepe zilizovuja akiukosoa utawala wa Trump.

Trump alisema: ''Balozi hajaitumikia vyema Uingereza, nawaeleza.''

Barua pepe za Kim Darroch zilisema kuwa ''haina ustadi na kuna mgawanyiko'' ndani ya Ikulu ya Marekani.

Waziri wa biashara Liam Fox ameiambia BBC kuvuja kwa barua pepe hizo ni jambo lililokosa ''maadili, lisilo la weledi na lisilo la kizalendo.''

Amesema yeyote aliyesababisha kuvuja kwa barua pepe hizo ni jambo ambalo ''kwa makusudi'' linakandamiza mahusiano ya kiulinzi na usalama na Marekani, ''uhusiano muhimu tulionao''.

Wakati Ofisi ya mambo ya nje ikianzisha uchunguzi kuhusu chanzo cha kuvuja kwa barua pepe siku ya Jumapili, Trump amewaambia wanahabari kuwa ''hatujapendezwa na mtu huyo na hajaitumikia vyema Uingereza''.

''Hivyo ninaelewa na ninaweza kuzungumza vitu kumhusu lakini sitajisumbua.''

Uchunguzi umeanza

Mamlaka zimeanza kufanya uchunguzi kuhusu barua pepe zilizovuja zilizotoka kwa Balozi wa Uingereza mjini Washington ambayo imedai kuwa utawala wa Trump si ''stadi''

Mwenyekiti kamati ya mambo ya nje Tom Tugendhat amesema kuwa tukio la kuvuja kwa barua pepe hizo si jambo dogo, na yeyote aliyehusika lazima ashtakiwe.

''Wanadiplomasia lazima waweze kuwasiliana katika hali ya usiri'' aliiambia BBC.

Sir Kim Darroch

Chanzo cha picha, PA Media

Ofisi ya mambo ya nje imesema kuvuja kwa barua pepe siku ya Jumapili ni jambo ''ufitini'' lakini hakukana kuhusu ukweli wa barua pepe hizo.

Ikulu ya Marekani haijasema lolote kuhusu kilicho kwenye barua hizo, lakini barua hizo huenda zikaleta mushkeli kwenye mahusiano kati ya Marekani na Uingereza.

Katika ujumbe wa barua pepe, Balozi wa Uingereza Kim Darroch amesema Ikulu ya Marekani ''haiwezi kufanya kazi ipasavyo'' na ''imegawanyika'' chini ya utawala wa Trump.

''Hatuamini kama utawala huu utakuwa sawasawa'': ''haifanyi kazi ipasavyo; ina mgawanyiko; haina ustadi katika kushughulikia masuala kidiplomasia'', alisema.

Amehoji kama kuna siku Ikulu ya Marekani ''itakuwa na uwezo''.

Bwana Tugendhat ameiambia BBC kuwa kitendo cha kuvuja kwa barua pepe hizo kichunguzwe- lakini alimtetea Bwana Kim.

Kazi ya balozi wa Uingereza ni kutetea maslahi na matakwa ya watu wa Uingereza'' na si masuala ya Marekani'', alisema.

Liam Fox

Ingawa Bwana Kim alisema Trump ''alishangazwa'' na ziara yake nchini Uingereza mwezi Juni, balozi alisema utawala wake utaendelea kuwa wa kujipendele wao: ''Hii ni ardhi ya Marekani kwanza''.

Tofauti kati ya Marekani na Uingereza kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, uhuru wa vyombo vya habari, na hukumu ya kifo, ni vitu vitakavyojitokeza wakati nchi hizo zikitafuta kuimarisha mahusiano ya biashara baada ya Brexit, barua pepe hizo zimeeleza.

Kiongozi anayeunga mkono mpango wa Brexit, Nigel Farage, amemkosoa bwana Kim kutokana na alichokiandika, akisema kuwa balozi huyo ''hafai kabisa kwa kazi hiyo'' akisema ''Ni vyema iwapo ataondoka mapema''.

Hatahivyo, Waziri wa sheria David Gauke anasema ni muhimu kwa wanadiplomasia kueleza ''ukweli na kutoa ushauri wa wazi na kweli kwa nchi yao''.

Alisema: ''Si jambo jema kuwa barua pepe zimevuja, lakini tutegemee mabalozi wetu kutuambia ukweli kwa namna wanavyouona.''