Iran yatangaza kuvunja mkataba wa nyukilia wa mwaka 2015

Iran imetangaza kuvunja mkataba kuhusu kiwango cha urutubishaji wa madini ya urani, mkataba uliowekwa mwaka 2015.

Naibu waziri wa mambo ya nje, Abbas Araqchi amesema Iran bado inataka kutekeleza mkataba huo lakini ameyashutumu mataifa ya Ulaya kwa kutotimiza wajibu wao.

Marekani ilijiondoa kwenye makubaliano hayo mwaka 2018.

Tangu wakati huo ikaweka tena vikwazo dhidi ya Iran.

Mwezi Mei Iran iliongeza urutubishaji wa urani, ambayo inaweza kutengeneza mafuta na silaha za nyukilia.

Akizungumza na waandishi wa habari, Bwana Araqshi amesema Iran itaanza shughuli za kurutubisha madini ya urani zaidi ya asilimia 3.6 ndani ya saa chache, kwa ajili ya vinu vyake vya umeme vya Bushehr

Bwana Araqchi amesema Iran itaendelea kupunguza utekelezaji wake kwa mkataba wa mwaka 2015 kila baada ya siku 60, mpaka pale mataifa yote yaliyosaini mkataba- China,Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Uingereza watakapochukua hatua ya kuilinda Iran dhidi ya vikwazo kutoka Marekani.

Tangazo hilo limekuja siku moja baada ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuzungumza na rais wa Iran Hassan Rouhani akieleza mashaka yake makubwa kuhusu kitakachotokea iwapo makubaliano yatakiukwa.

Bwana Rouhani ametoa wito kwa mataifa ya Ulaya kuchukua hatua haraka kunusuru makubaliano hayo.

Lakini amesisitiza kuwa wako tayari kwa mazungumzo ya kidiplomasia, kama vikwazo vitaondolewa.

Kwanini Iran imeongeza viwango vya urutubishaji?

Mapema mwezi Mei, Trump aliweka shinikizo zaidi kwa Iran kwa kuidhinisha upya marufuku kwa matiafa yanayonunua mafuta kutoka kwa Iran.

Hatua hiyo ilinuiwa kusitisha kipato kikuu kwa serikali ya Iran.

Rais wa Iran Hassan Rouhani alitangaza kuwa nchi yake inarudi nyuma katika ahadi zake katika makubaliano hayo.

Hii ikiwa ni pamoja na kutotiii sheria kuhusu akiba yake ya urutubishaji mdogo wa madini ya Uranium kiwango kilichowekwa kikwa ni - 300kg na tani 130 - na kusitisha uuzaji wa akiba ya ziada katika mataifa ya nje.

Rouhani pia aliyapatia mataifa hayo ya Ulaya siku 60 kulinda mauzo ya mafuta ya Iran. Iwapo yatashindwa kufanya hivyo , Iran itakiuka masharti ya urutubishaji Uranium na kusitisha uundwaji upya wa kinu cha Arak, ambacho mafuta yake yaliotumika yana plutonium yalio na uwezo wa kuunda mabomu.

Kurutubisha madini ya Urani

Hifadhi ya madini ya urani ilipunguzwa kwa asilimia 98, mpaka kilogramu 300 kiasi ambacho hakitakiwi kuongezeka mpaka mwaka 2031. madini yanayotakiwa kurutubishwa yanapaswa kuwa asilimia 3.67.

Mwezi Januari mwaka 2016, Iran ilipunguza uzalishaji kwenye vinu vyake vya Natanz na Fordo, na kusafirisha tani chache za madini ya urani kwenda Urusi.

Hakuna shughuli yeyote ya urutubishaji itakayoruhusiwa kwenye vinu vya Fordo mpaka mwaka 2031, na eneo hilo litabadilishwa kuwa kituo cha nyukilia, fizikia na teknolojia.Kutazalishwa kemikali kwa ajili ya kutengeneza dawa kwa ajili ya kilimo,viwanda na sayansi.

Iran imekuwa ikitengeneza kinu chake cha nuklia katika mji wa Arak.

Mataifa yenye nguvu duniani awali walitaka Arak isiendelee na shughuli hiyo,kwa sababu ya ongezeko la hatari.Chini ya mkataba wa nyukilia waliokubaliana mwaka 2013, Iran ilikubali kutoendelea na uzalishaji.

Iran iliahidi kubadili mfumo wa vinu vyake ili visiweze kutengeneza silaha zozote mpaka mwaka 2031.

Wakati wa makubaliano, rais wa Marekani wa wakati huo, Barack Obama alieleza matumaini yake kuwa Iran itazuiwa kutengeneza mradi wa nyukilia kwa siri.Iran ilisema imeridhia kukaguliwa na kutazamwa kwa karibu namna wanavyotekeleza makubaliano hayo.

Waangalizi wa Shirika la nguvu za Atomiki duniani, wameendelea kuifuatilia Iran na maeneo wanayofanyia kazi za urutubishaji na kujiridhidha kuwa hakuna madini yanayopelekwa kwenye sehemu nyingine kwa siri kutengeneza bomu.

Mpaka mwaka 2031, Iran itakuwa na siku 24 za kukubaliana na maombi ya IAEA kufanya uchunguzi wao, ikiwa itakataa tume yenye wanachama wanane -ikiwemo Iran- itatoa uamuzi kuhusu suala hilo.Na itaamua kuhusu hatua za kuchukua, ikiwemo kuiwekea vikwazo tena.